
KIUNGO wa zamani wa Azam FC, Kipre Junior, amevunja mkataba na MC Alger ambayo ilikuwa inataka kuingiza mchezaji mwingine kwenye nafasi yake ya wachezaji wa kigeni, huku ikielezwa huenda akarejea kwa mabosi wake wa zamani, Azam FC.
Kipre ambaye aliichezea Azam kwa misimu miwili, huku akiacha rekodi ya kufunga mabao 12, mawili mwaka wa kwanza na 10 mwaka wa pili.
Inaelezwa kuwa taarifa ya Kipre kuvunja mkataba ilipomfikia kocha wa kikosi hicho, Rhulani Mokwena, alibariki uamuzi huo, huku kiungo huyo pia akikubaliana na uongozi wa klabu hiyo kuondoka.
Taarifa za ndani zililiambia Mwanaspoti kuwa, Kipre ameondoka ili kupisha usajili wa mchezaji mwingine wa kigeni ndani ya kikosi hicho.
HESABU ZA AZAM
Hapo awali Azam ilikuwa na hesabu za kumrudisha kiungo huyo kabla ya dirisha dogo la usajili kufungwa, lakini ikajikuta imechelewa.
Wakati Kipre anaenda MC Alger, alikuwa na makubaliano na klabu hiyo kwamba endapo ataachana na Waarabu hao, basi timu ya kwanza kwenda itakuwa Azam FC.
Kabla ya kuondoka Azam, Kipre alikuwa miongoni mwa mastaa wa Ligi Kuu kutoka Ivory Coast waliokuwa wanakiwasha kwa kiwango cha juu, huku tetesi zikisema Simba pia ilihitaji huduma yake wakati anakaribia kuachana na matajiri hao wa Chamazi.
Kiungo huyo ameachana na MC Alger ikiwa kinara kwenye Ligi ya Algeria ikiwa na pointi 36 katika mechi 15, huku akiacha rekodi ya kufunga mabao manne katika misimu miwili.