
KOCHA Mkuu wa Pamba Jiji, Francis Baraza amesema hakuna mchezaji aliyesajiliwa kikosini kula bata, bali kila mmoja anapaswa kutimiza wajibu wake ili kuwa na uhakika wa namba, akisisitiza kuwa hana staa kwenye timu.
Pamba Jiji imekuwa na kiwango bora msimu huu baada ya kuvuna pointi 17 ambapo Jumatatu hii, watakuwa uwanjani ugenini kuwakabili JKT Tanzania waliopo nafasi ya pili kwa pointi 21.
Akizungumza na Mwanaspoti, Baraza amesema wachezaji wote waliopo kikosini kila mmoja analo jukumu la kuipambania timu, akieleza kuwa falasafa yake ni kuwapa nafasi wote kuonyesha uwezo na kipaji.
Amesema katika michezo miwili ya mwisho hajafurahishwa na kasi ya mastraika kutokana na kutofunga idadi kubwa ya mabao, akieleza kuwa mchezo ujao dhidi ya JKT Tanzania, anahitaji kuona utofauti.
“Sina staa kwenye timu, wachezaji wote nawapa nafasi, simtegemei mtu mmoja, lazima wote watimize wajibu waoneshe utofauti na sijaona kasi ninayoitaka kwenye ufungaji mabao, nataka kuona mabadiliko,”€ amesema Baraza.
Kocha huyo raia wa Kenya ameongeza kuwa licha ya matokeo waliyonayo, ushindani ni mkali kutokana na timu zote kuonyesha upinzani akibainisha kuwa hali hiyo inawapa nguvu kuendelea kupambana.
Kwa upande wake kiungo wa timu hiyo, Shassir Nahimana amesema vita ya namba ni kubwa kikosini kutokana na wachezaji wote kuwa bora, akieleza kuwa mkakati wao ni kutafuta ushindi kila mechi.
Amesema malengo yao ni kumaliza ndani ya nafasi nne za juu akikiri ugumu kwenye ligi na kwamba ushirikiano walionao ndani ya timu unawapa matumaini ya kutamba kufikia malengo.
“Hatuna ugenini wala nyumbani, tunahitaji matokeo mazuri popote, Pamba Jiji wachezaji wote ni bora, tunashinda wote na kufungwa wote, tunao ushirikiano na malengo ni kumaliza ndani ya nafasi nne za juu,” amesema nyota huyo raia wa Burundi.