Mahakama ya Watu ya Xiamen katika jimbo la pwani la Fujian imesema Tang alipokea mali kinyume cha sheria zenye thamani ya zaidi ya yuan milioni 137 (sawa na dola za Marekani milioni 19.71) kati ya mwaka 2006 na 2022.
Kwa mujibu wa uamuzi wa mahakama, Tang alitumia vibaya wadhifa wake kujinufaisha yeye na wengine katika maeneo mbalimbali, yakiwemo kuorodhesha kampuni katika soko la hisa, urejeshaji wa ardhi, mikopo ya benki na ushughulikiaji wa kesi za kisheria.
Mahakama ilisema kuwa “vitendo vya Tang vinaunda kosa la rushwa,” na kuongeza kuwa kiasi cha fedha kilichohusika kilikuwa “kikubwa kupita kiasi” na kimesababisha “hasara kubwa sana” kwa maslahi ya taifa na wananchi.
Mbali na kifungo cha maisha, Tang pia amenyimwa haki zake zote za kisiasa maisha yake yote, huku mali zake binafsi zote zikitaifishwa, kwa mujibu wa taarifa ya televisheni ya serikali ya China, CCTV.
Kampeni ya Rais Xi dhidi ya rushwa
Hukumu hiyo inakuja wakati Rais Xi Jinping akiendeleza kampeni kubwa ya kitaifa ya kupambana na rushwa, ambayo katika wiki za hivi karibuni imewanasa maafisa kadhaa wa ngazi za juu serikalini.
Mamlaka ya kitaifa ya kupambana na rushwa ilitangaza mwishoni mwa wiki kuwa imeanzisha uchunguzi dhidi ya Wang Xiangxi, Waziri wa Usimamizi wa Masuala ya Dharura — hatua inayotajwa kuwa nadra kwa waziri aliye madarakani kuwekwa chini ya uchunguzi.
Mwezi uliopita, China pia ilitangaza kuwa Zhang Youxia, mmoja wa majenerali wakuu wa jeshi, alikuwa akichunguzwa, katika kile kinachotajwa kuwa msako mkubwa zaidi hadi sasa dhidi ya uongozi wa juu wa kijeshi.
Historia ya Tang Yijun
Tang, mwenye umri wa miaka 64, alianza kazi yake katika jimbo la Zhejiang mashariki mwa China, ambako alihudumu kwa zaidi ya miongo mitatu na hatimaye kupanda cheo hadi kuwa Naibu Katibu wa Chama cha Kikomunisti wa jimbo hilo.
Baadaye alihudumu kama gavana wa jimbo la Liaoning kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Sheria mwaka 2020.
Tang aliwekwa chini ya uchunguzi mwezi Aprili 2024 kwa tuhuma za ukiukwaji mkubwa wa nidhamu na sheria — kauli inayotumiwa mara nyingi nchini China kumaanisha rushwa — na alifukuzwa kutoka Chama cha Kikomunisti baadaye mwaka huo.
