Jeshi la Ujerumani, Bundeswehr, limetenga zaidi ya euro bilioni 108, sawa na dola bilioni 129 za kimarekani, kwa matumizi mwaka huu.
Kiasi hiki kikubwa kinatokana na bajeti ya shirikisho pamoja na fedha maalum ambazo Ujerumani imechukua kama mikopo.
Lengo la Ujerumani ni kuimarisha pamoja na kuboresha jeshi la nchi hiyo Bundeswehr baada ya miongo kadhaa ya kupunguzwa kwa bajeti yake .
Lakini pia kuna dharura ya kwenda na wakati na Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius ana wasiwasi kuwa Urusi inaweza kuwa na uwezo wa kushambulia maeneo ya NATO mapema kabla ya mwaka 2029.
Kwa mara ya kwanza katika historia yake, Ujerumani inagharamia ununua wa maelfu ya ndege za kivita zisizo na rubani yaani drones.
Nchi hii ilikuwa imeepuka ndege hizi kwa sababu ya upinzani wa kisiasa, lakini uvamizi wa Urusi nchini Ukraine umeonyesha umuhimu wake.
Kampuni za teknolojia mpya, kama Stark Defence mjini Berlin na Helsing mjini Munich, zitapokea mkataba hadi euro milioni 300 kila moja, huku kampuni mpya ya Rheinmetall, ikishindwa kuvutia majaribio ya Bundeswehr.
Ndege hizi, zinazojulikana rasmi kama “loitering amunitions,” mara nyingi huitwa ndege za “kamikaze” kwa sababu huruka moja kwa moja na kushambulia eneo lililokusudiwa bila kukosea. Baadhi yake ni kwa ajili ya kusaidia kulinda mipaka ya mashariki ya mataifa ya NATO.
Maboresho sekta ya anga
Mpango huu unajumuisha vizuizi vya mawimbi au (jammers), tanki za kupambana na ndege zisizo na rubani kama Skyranger 30, na hata silaha za laser kwa jeshi la majini.
Skyranger, inayotengenezwa na kampuni ya Rheinmetall, inasubiriwa kwa hamu kutokana na hali kwamba kuna ndege zisizo za kawaida zinazoendelea kuruka juu ya Ujerumani, na hata katika maeneo ya makao ya jeshi la Ujerumani Bundeswehr.
Hata hivyo, haitatolewa hadi mwaka 2028, lakini itakuwa ni silaha kuu ya ulinzi wa anga wa jeshi la nchi hiyo. Silaha za laser zilizotengenezwa na kampuni ya Rheinmetall na MBDA tayari zimeshapatikana na sasa ziko kwenye orodha ya ununuzi.
Ujerumani pia imenunua helikopta, ndege za kivita, na ndege za ufuatiliaji na uchunguzi wa baharini.
Sehemu kubwa inapatikana kutoka kampuni za Ulaya, lakini baadhi ya manunuzi makubwa yanatoka Marekani.
Ujerumani imeagiza pia ndege 35 za kivita za F-35A kutoka kampuni ya Lockheed Martin ya nchini Marekani kwa karibu euro bilioni 10.
Ndege hizi zina uwezo wa kubeba mabomu ya nyuklia za Marekani katika dharura na zitashtua ndege za zamani za Tornado. Ujerumani pia inapata helikopta 60 za CH-47 Chinook kutoka Boeing kwa euro bilioni 7.3.
Katika ulinzi wa baharani, jeshi la majini la Ujerumani lilipokea ndege ya kwanza ya P-8A Poseidon kutoka Boeing msimu uliopita.
Ndege hizi zinaweza kulinda doria katika maeneo makubwa ya bahari na kugundua manowari kwa kutumia sensa za kisasa. Waziri Pistorius alisema zinaweza kusaidia Ujerumani katika ufuatiliaji katika maeneo ya NATO, ikiwa ni pamoja na eneo la Greenland.
Teknolojia ya akili Mnemba imezingatiwa
Kwa upande mwingine teknolojia ya matumizi ya akili mnemba pia inaonekana kuwa sehemu ya ulinzi.
Mradi wa Uranos KI unalenga kusaidia kikosi cha Ujerumani kilichoko nchini Lithuania kufuatilia maeneo makubwa kwenye mipaka ya mashariki ya NATO.
Akilimnemba pia itasaidia kuchambua data kutoka kwa sensa nyingi za ulinzi pamoja na kurahisisha mfumo mzina wa ufuatiliaji na kugundua mapema ndege za adui zisizo na rubani. Maelezo ya mradi hata hivyo kw upande wake hayajulikani kwa sababu za kiusalama.
Kwa upande wa mfumo wa ulinzi wa majini hata hivyo miradi yake haijakwenda vizuri kama ilivyotarajiwa kwa sababu meli kubwa aina ya Frigate F126 ya kivita iliyokuwa imepokelewa hapo awali kutoka Uholanzi imekumbwa na changamoto za kiufundi. Kiwanda cha meli cha Uholanzi, Damen Naval, kilishindwa kukamilisha meli hizi, licha ya kuwa euro bilioni 1.8 tayari zimeshatolewa na Ujerumani.
Ujerumani pia inaboresha kiwango cha sae na vifaa vya kijeshi kwa wanajeshi 460,000. Hivi sasa, jeshi lake Bundeswehr lina wanajeshi 184,000.
Uboreshaji huu na zana mpya vinatolewa ili kuhakikisha kila mwanajeshi ana vifaa vya kupambana. Waziri Pistorius alisema, “Hatuwezi tu kuvalisha wanajeshi wapya nguo za michezo kama suluhisho la muda.
Ujerumani inafanya mabadiliko makubwa ya kijeshi kwa haraka, ili kukabiliana na hali yoyote inayoweza kujitokeza siku za usoni kwa usalama wake.
