Vyombo vya habari vinavyoendeshwa na serikali nchini Misri pamoja na maafisa wa usalama wa Israel, wamethibitisha kufunguliwa tena kwa kivuko hicho cha Rafah ambapo watu wachache tu wataruhusiwa kusafiri kutoka pande zote mbili na hakuna bidhaa zitakazoruhusiwa kuingia.
Utaratibu wa kuingia na kuondoka Gaza
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema nchi yake itawaruhusu wagonjwa 50 kwa siku kuondoka Gaza.
Afisa mmoja anayeshiriki mazungumzo ya kufunguliwa kwa kivuko hicho cha Rafah aliyezungumza kwa sharti la kutotambulishwa, amesema kila mgonjwa ataruhusiwa kusafiri na jamaa zake wawili, huku baadhi ya watu 50 walioondoka Gaza wakati wa vita wakiruhusiwa kurejea kila siku.
Kwa upande wake, msemaji wa ujumbe ulioko Israeli na Maeneo Yanayokaliwa, wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC), Patrick Griffiths, amesema wana matumaini kwamba kufunguliwa kwa kivuko cha Rafah kunaweza kumaanisha kwamba watu wanaweza kuunganishwa tena na familia zao.
”Tuna matumaini kwamba inaweza kumaanisha Wapalestina walioko Gaza na wanaohitaji kuhamishwa kwa dharura za kimatibabu wanaweza kufanya hivyo. Na tunatumai kuwa inamaanisha msaada zaidi wa kibinadamu unaweza kuingia Gaza, ambayo ni muhimu sana.”
Huku hayo yakijiri, wizara ya afya ya Misri imetoa taarifa leo na kusema hospitali 150 kote nchini humo zimetayarishwa kupokea wagonjwa wa Kipalestina na majeruhi ambao watahamishwa kutoka Gaza kupitia kivuko hicho cha Rafah.
MSF yashtumiwa kwa kukiuka taratibu za usajili mpya Gaza
Israel imesema jana kuwa inakusudia kusimamisha shughuli za shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) katika Ukanda wa Gaza. Wizara ya Israel inayosimamia uhusiano kati ya Israel na jamii za kiyahudi kote ulimwenguni imesema shirika la MSF limekiuka taratibu mpya za usajili kwa kushindwa kutoa orodha ya wafanyakazi wake wa Kipalestina Gaza.
Imesema utaratibu huo wa usajili unalenga kuwezesha kufanyika kwa shughuli halali za kibinadamu huku ukizuia matumizi mabaya ya mifumo ya kibinadamu kwa shughuli za uhasama na ugaidi.
Sheria hiyo inatumika kwa mashirika yote za kibinadamu yanayofanya kazi kwenye eneo hilo.
Katika maelezo yake, MSF imesema haijatoa orodha hiyo kwasababu mamlaka ya Israel ilishindwa kutoa hakikisho thabiti linalohitajika kuhakikisha usalama wa wafanyakazi wake.
Kundi hilo lazima sasa liondoke Ukanda wa Gaza ifikapo Februari 28.
Kamanda wa Hezbollah auawa
Jeshi la Israel limesema limemuuwa kamanda mmoja wa Hezbollah kusini mwa Lebanon.
Katika chapisho kwenye mitandao ya kijamii, limeandika kuwa limemuuwa Ali Dawoud Amich, aliyekuwa msimamizi wa kitengo cha uhandisi wa kundi hilo.
Taarifa hiyo imesema Ali alihusika na majaribio ya kukarabati miundombinu ya kigaidi ya Hezbollah katika eneo la Al-Dweir kusini mwa Lebanon na mashambulizi ya kigaidi dhidi ya jeshi hilo hivyo basi kukiuka maelewano kati ya Israel na Lebanon.