Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Esmeil Baqaei amesema Jumatatu kwamba mataifa kadhaa ya kikanda yamechukua jukumu laupatanishi katika suala zima la mawasiliano. Hata hivyo hakutoa maelezo zaidi kuhusiana na maudhui hasa ya mazungumzo hayo. Amesema tayari baadhi ya vipengele vimeshafanyiwa kazi na wanachokifanya sasa ni kuhitimisha maelezo ya kila hatua ya mchakato huo wa kidiplomasia, ambao wataukamilisha siku sijazo.
Jumatatu, taifa hilo aidha lilikana kupewa muda na Rais Donald Trump wa kufikia makubaliano hayo ya nyuklia, baada ya kiongozi huyo wa Marekani kusema amewapa muda wa kuingia kwenye mazungumzo, katikati ya kitisho hicho cha kuwavamia kijeshi. Baqaei amewaambia waandishi wa habari kwamba Iran ni taifa ambalo mara zote huchukua hafanya mambo yake kwa uaminifu na umakini katika michakato ya kidiplomasia, lakini kamwe haikubaliani na kupewa muda.
Lakini mwishoni mwa wiki, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi alikiri alipozungumza na kituo cha utangazaji cha CNN cha nchini Marekani kwamba hawana imani tena na mshirika huyo wa mazungumzo, huku akisisitiza hali ya kuaminiana ili kuufanikisha mchakato huo wa kidiplomasia.
Qatar na Iran wafanya mazungumzo ya kulegeza mvutano
Siku ya Jumamosi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar Mohammed Abdulrahman Al Thani alikutana na Araghchi na katibu mkuu wa Baraza la Usalama la Iran Ali Larijani mjini Tehran, na kwenye mazungumzo, Araghchi alisisitiza kwamba vita vitakuwa na athari kubwa kwa kila mmoja. Akasema Iran imejifunza kutoka kwenye vita vya nyuma na anaiona kwa sasa imejiandaa vizuri, ingawa hilo halimaanishi kwamba wanataka vita.
Viongozi hao walikuwa wakiangazia juhudi za kupunguza mvutano wa kikanda, hii ikiwa ni kulingana na wizara ya mambo ya nje ya Qatar, katikati ya kile kinachochochewa na matamshi makali kutoka pande zote mbili, huku kiongozi wa juu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei naye akisistiza kwamba ikiwa Marekani itaivamia Iran, huo utakuwa ni mzozo wa kikanda.
“Unapowasikia wakizungumza kuhusu vita, wakisema mambo kama vile ‘tutakuja na ndege hii au ndege ile na kufanya hili au lile,’ si jambo jipya. Wamarekani wametutishia mara kwa mara huko nyuma, wakisema ‘machaguo yote yako mezani,’ yakijumuisha chaguo la vita. Wamekuwa wakisema mambo haya kila mara. Vile vile, huyu Trump amekuwa akidai kwamba ameleta meli za kivita Iran. Watu wa Iran hawatachochewa na vitisho hivi, lakini taifa la Iran litajibu vikali dhidi ya yeyote anayewashambulia na kuwanyanyasa,” alisema kiongozi huyo wa juu.
Iran yawaita mabalozi wa umoja wa Ulaya
Katika hatua nyingine, Iran imesema hii leo kwamba imewaita mabalozi wa Umoja wa Ulaya kwenye Jamhuri hiyo ya Kiislamu, kupinga hatua ya umoja huo kukiorodhesha Kikosi cha Mapinduzi cha Iran kama kundi la kigaidi. Umoja wa Ulaya ulifikia hatua hiyo wiki iliyopita kutokana na hatua kali ilizochukua dhidi ya waandamanaji mwezi Januari, ambapo maelfu waliuawa na maelfu wengine walifungwa.
Baqaei amewaambia waandishi wa habari kwamba tayari wameanza kuwaita mabalozi siku ya Jumapili na wataendelea hadi leo Jumatatu na kuongeza kuwa tayari wamefanya mapitio ya hatua za kuchukua na kuongeza kuwa katika siku chache zijazo watafanya maamuzi ya kujibu hatua hiyo aliyoitaja kuwa haramu, isiyo na maana na mbaya kabisa iliyochukuliwa na Umoja wa Ulaya.
Jana Jumapili, spika wa bunge la Iran alisema taifa hilo kwa sasa pia linayachukulia majeshi yote ya Umoja wa Ulaya kama makundi ya kigaidi, akiangazia sheria ya mwaka 2019 ya taifa hilo.