
KOCHA wa timu ya Kundemba inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Zanzibar, Mohammed Seif Mzee, amefungiwa michezo mitatu mfululizo na kutozwa faini ya Sh1 milioni kwa kosa la kuhamasisha vitendo vya utovu wa nidhamu vya kupigwa kwa mwamuzi, Salum Salum Ali.
Uamuzi huo umetolewa na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Bodi ya Ligi Zanzibar (ZLB) katika kikao chake kilichofanyika Januari 27, 2026 kwa kupitia mwenendo wa matukio mbalimbali ikiwamo mchezo namba 133 kati ya Kundemba na Muungano Rangers uliochezwa Januari 26, kwenye Uwanja wa Mao B, Mjini Unguja.
Taarifa iliyotolewa leo Jumatatu ya Februari 2, 2026 na Ofisa Habari wa Bodi ya Ligi Zanzibar, Issa Chiwile imebainisha kuwa kamati hiyo ilipitia ripoti ya wasimamizi wa mchezo na kubaini katika mchezo huo kulitokea vurugu na ghasia ya kupigwa kwa mwamuzi Salum Mohamed Ali baada ya kukamilika kwa mchezo huo vitendo ambavyo ni makosa kisheria chini ya Sura ya 20 (1) 2 na 3.
“Kamati imetoa uamuzi kuwa kocha Mohammed amefungiwa kufundisha na kuongoza benchi la ufundi la timu hiyo kwa michezo mitatu mfululizo kwa kosa la kuhamasisha vitendo vya utovu wa nidhamu vya kupigwa kwa muamuzi,” imesema taarifa hiyo
Taarifa hiyo, imeeleza kuwa kocha huyo ametozwa faini ya Sh1 millioni kwa kosa la kutoa maneno yasiyofaa na kumpiga makofi mwamuzi kwenye vyumba vya kubadilishia nguo na adhabu hizo zimetolewa chini ya sura ya 20 ya kununi ya mashindano ya 2025-2026.
Pia, Mtunza Vifaa wa Kundemba, Nassor Mzaka Khalfan amefungiwa kujihusisha na kuhudhuria kwenye mechi zitakazoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF) kwa kipindi cha miaka miwili pamoja na faini ya Sh1 millioni kutokana na rekodi yake ya kuhamasisha vurugu mara kwa mara kwa timu hiyo inapocheza.
Naye, shabiki wa timu hiyo, Mohammed Ussi Chape amefungiwa kuhudhuria kwenye mechi zitakazoandaliwa na ZFF kwa kipindi cha miezi sita na kutozwa faini ya Sh500,000 kwa kosa la kumpiga ngumi mwamuzi wakati akitolewa uwanjani na walinzi.
Aidha, kamati hiyo imewasihi viongozi wachezaji na mashabiki kuzingatia mchezo wa kiungwana, kutafuta ushindi na kukubali kushindwa kwa kudumisha maslahi ya mpira na kukataa mambo yote yanayoondoa usalama wa mpira.
Ligi ya Daraja la Kwanza imekuwa na rekodi ya kufanya matukio ya aina hiyo ya kuwapiga waamuzi kwa kisingizio cha kutoridhishwa na matokeo au uamuzi uliotolewa na waamuzi wa michezo hiyo.