
Kundi la kwanza la Wapalestina lilianza kurejea katika Ukanda wa Gaza kupitia kivuko cha mpaka cha Rafah kati ya eneo hilo la pwani na Misri, baada ya kivuko hicho kufunguliwa tena kwa ajili ya harakati za watu.
Wapalestina waliingia Gaza Jumatatu asubuhi chini ya uangalizi mkali jeshi la Israel, kwa uratibu na Misri, pamoja na usimamizi wa Umoja wa Ulaya.
Kivuko hicho kilianza kufanya kazi Jumapili kwa majaribio baada ya kufungwa kabisa kwa zaidi ya miezi 18 kufuatia mzingiro uliowekwa na utawala dhalimu wa Israel.
Takriban Wapalestina 50 wanatarajiwa kuingia Gaza, huku takriban Wapalestina 150, wakiwemo wagonjwa wanaohitaji matibabu na waandamani wao, wakipanga kuondoka Gaza kupitia kivuko hicho kuelekea Misri.
Kwa mujibu wa maafisa wa afya wa Gaza, wagonjwa wengine wapatao 22,000 wa Kipalestina wanasubiri kufunguliwa kikamilifu kwa kivuko cha Rafah ili waweze kufika Misri kwa ajili ya matibabu.
Tangu Mei 2024, majeshi ya utawala wa Israel yamekuwa yakidhibiti upande wa Palestina katika kivuko cha Rafah.
Majeshi ya Israel yalifungua kwa muda kivuko hicho muhimu ili kuruhusu wagonjwa na Wapalestina waliojeruhiwa kuondoka Gaza kwa matibabu nje ya nchi wakati wa usitishaji mapigano wa muda mfupi Januari 2025.
Hata hivyo, majeshi ya Israel yalifunga tena kivuko cha Rafah.
Kwa mujibu wa ratiba, majeshi ya Israel yalipaswa kukikabidhi tena kivuko hicho muhimu kwa Wapalestina katika awamu ya kwanza ya makubaliano ya usitishaji mapigano yaliyosimamiwa na Marekani, yaliyoanza kutekelezwa Oktoba 2025. Hata hivyo, utawala wa Israel ulikaidi na kukiuka makubaliano hayo.
Tangu kuanzisha vita vya mauaji ya kimbari katika Gaza Oktoba 2023, utawala wa Israel umewaua takriban Wapalestina 72,000 na kuwajeruhi zaidi ya 171,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.
Aidha, karibu asilimia 90 ya miundombinu ya kiraia katika Gaza imeharibiwa katika mashambulizi makali yaliyotekelezwa na jeshi la Israel katika kipindi hicho.
Baada ya kusitishwa kwa mapigano, majeshi ya Tel Aviv yameripotiwa kukiuka makubaliano hayo kila siku, hali iliyosababisha kuuawa kwa Wapalestina wengine 523.
Haya yanajiri wakati ambapo wakazi milioni 2.4 wa Gaza wanakabiliwa na hali mbaya ya kibinadamu kutokana na mzingiro unaoendelea wa Israel, na wanahitaji msaada wa kimataifa kuwafikia katika eneo hilo lililoharibiwa na vita.