Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa uwepo wa wanajeshi wa nchi ajinabi katika kanda hii siku zote huwa sababu ya kushatadi mivutano.
Sayyid Abbas Araqchi ametuma ujumbe akiashiria uwepo wa wanajeshi wa nchi za kigeni katika eneo la Ghuba ya Uajemi na kuandika: Matokeo ya uwepo wa wanajeshi hao katika kanda hii siku zote ni kuzidisha mivutano.
Araqchi ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X kwamba: Marekani imeainishwa kwa rangi ya njano katika nusu ya Magharibi mwa dunia. Bahari kadhaa mbali katika upande mwingine wa dunia, mipaka ya Iran pia imeainishwa kwa rangi ya njano. Duara dogo jekundu linaonyesha Mlango-Bahari wa Hormuz.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameeleza kuwa: Uhuru wa urambazaji na safari salama za meli za kibiashara kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz ni muhimu kwa Iran kama ilivyo kwa majirani zetu. Uwepo wa wanajeshi wa nchi ajinabi katika eneo la Ghuba ya Uajemi siku zote umekuwa na matokeo kinyume na madai yao.

Marekani na nchi za Magharibi zinazoiunga mkono Ikulu ya White House zimekuwepo katika Ghuba ya Uajemi kwa miaka mingi kwa lengo la kudhibiti njia za usafirishaji wa nishati, kudhamini maslahi yao ya kisiasa na kijeshi na kuzishinikiza nchi huru za eneo la hilo. Hata hivyo, uwepo huu wa kijeshi siku zote umeandamana na taathira hasi na migogoro badala ya kudumisha “usalama.”
Uvamizi wa Marekani huko Iraq, Syria na Yemen ni mifano ya wazi ya “migogoro iliyotengenezwa” ili kudumisha ushawishi wa Marekani na Magharibi kwa ujumla. Maamuzi na uingiliaji huu wa nchi ajinabi vimemesababisha kupuuzwa mahitaji na utamaduni wa watu wa kanda hiyo na kuzidisha makabiliano ya kisiasa na kijeshi.
Ghuba ya Uajemi ni mojawapo ya kanda nyeti zaidi duniani kwa upande wa jiopolitiki, na ukosefu wa usalama katika Mlango Bahari wa Hormuz ambao ni kati ya njia kuu za kusafirisha nishati duniani unaweza kuathiri uchumi wa dunia hususan wa nchi za Magharibi.
Nchi za Ghuba ya Uajemi zina akiba kubwa zaidi ya mafuta na gesi duniani na hapana shaka kwamba ushirikiano wa kiuchumi kati ya Iran na majirani zake utaongeza mauzo ya nje na uwekezaji wa pamoja katika sekta ya nishati na petrokemikali, kupanua biashara ya kikanda na njia za usafirishaji na kuandaa fursa za ajira na ukuaji wa viwanda.
Mtazamo wa kidiplomasia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika miaka ya hivi karibuni umejikita katika mantiki kwamba usalama wa kweli unatoka ndani ya kanda husika na si kutoka nje. Iran imetangaza mara kadhaa kwamba Mlango Bahari wa Hormuz na usalama wa eneo hilo si kwa ajili yake pekee bali kwa jaili ya usalama wa nchi zote jirani.
Sera ya Iran inatokana na mazungumzo na ushirikiano wa pamoja ambao unatilia mkazo kujenga hali ya kuaminiana na kushirikiana katika nyanja za kuchumi na kiusalama kati ya nchi za Ghuba ya Uajemi.
Mojawapo ya malengo makuu ya sera za kigeni za Iran ni kupunguza ushawishi wa madola ya kigeni katika maamuzi ya kanda hii ambayo yanatokana na mtandao wa ushirikiano wa kiuchumi na kiusalama baina ya nchi za Ghuba ya Uajemi.
Kwa msingi huo, ushirikiano kati ya Iran, Saudi Arabia, UAE, Oman, Qatar, na Kuwait unaweza kuwa mbadala wa ushindani unaotegemea madola ya kigeni. Ushirikiano huo utapelekea kuimarishwa kujitawala na mamlaka ya kitaifa ya nchi za eneo hilo na hivyo kupunguza haja ya kuwepo majeshi ya nchi ajinabi katika Ghuba ya Uajemi.