
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka na jamii ya kimataifa ili kukomesha mauaji ya halaiki katika Ukanda wa Gaza.
Esmail Baghai Hamaneh, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, amelaani vikali mashambulizi ya kikatili ya utawala wa Kizayuni katika maeneo ya Ukanda wa Gaza, ikiwemo kituo cha polisi, mahema ya wakimbizi wa Kipalestina, na maeneo ya makazi, ambayo yamesababisha kuuawa shahidi watu zaidi ya 30, wakiwemo watoto 6.
Akiashiria kuendelea kuuawa watu wa Gaza licha ya kutangazwa usitishaji mapigano mwezi Oktoba 2025 na kuuawa shahidi Wapalestina 524 katika siku 110 zilizopita, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: “Kuendelea uhalifu wa utawala wa Kizayuni huko Gaza na Ukingo wa Magharibi na kuendelea kuzuiwa kuingia chakula na dawa katika ukanda huo ni ishara wazi ya kuendelea sera ya mauaji ya kimbari ya miaka 80 huko Palestina kwa usaidizi na ushirikiano wa Marekani na baadhi ya madola ya Ulaya, ikiwa ni pamoja na Ujerumani na Uingereza.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, huku akitoa rambirambi kwa familia za mashahidi na watu wa Palestina, amebainisha jukumu la pamoja la jamii ya kimataifa, hasa Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu wa umoja huo, na pande zinazodhamini usitishaji mapigano, kuuwajibisha utawala vamizi wa Israel kwa uhalifu na ukiukwaji wake wa mara kwa mara wa makubaliano ya kusitisha mapigano.
Baghaei amesema kuna haja ya kuchukuliwa hatua za haraka za kukomesha mauaji ya kimbari na kuwashtaki wahalifu, kuondolewa kabisa vikosi vamizi kutoka Ukanda wa Gaza, kuingia bila vikwazo misaada ya kibinadamu, kufunguliwa tena mpaka wa Rafah, na kuanza mara moja mchakato wa ujenzi mpya huko Gaza.