Dar es Salaam. Serikali inatarajia kutegemea zaidi mapato ya ndani kufadhili bajeti ya mwaka ujao wa fedha 2026/27, hali inayoonesha mwelekeo wa kupunguza utegemezi wa misaada ya nje na kuimarisha uhimilivu wa fedha kitaifa.

Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2026/27 inatarajiwa kuwa Sh61.93 trilioni. Kati ya fedha hizo, mapato yote yanayotarajiwa kukusanywa, ikijumuisha misaada, ni Sh46.69 trilioni, sawa na asilimia 75.4 ya bajeti yote.

Mapato ya kodi yanakadiriwa kuwa Sh36.89 trilioni huku mapato mengine yakifikia Sh9.24 trilioni yakiwemo mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa ya Sh1.97 trilioni. Kwa ujumla, mapato ya ndani yanatarajiwa kufikia Sh46.13 trilioni, sawa na takribani asilimia 74.5 ya bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka huo wa fedha.

Ongezeko hili la ufadhili wa bajeti ya ndani linatarajiwa kuwa la juu zaidi katika kipindi cha miaka minne iliyopita kwani kwa mujibu wa bajeti ya Serikali mwaka 2022/23 makadirio ya makusanyo ya ndani yalikuwa asilimia 67.6, mwaka uliofuata ikiwa asilimia 70.7 na 2024/25 ilikuwa asilimia 72.6.

Vilevile, mwaka wa fedha unaoendelea wa 2025/26 Serikali ilikadiria mapato na matumizi kuwa Sh56.49 trilioni na makusanyo kuwa Sh40.47 trilioni sawa na asilimia 71.6 ya bajeti kuu.

Kwa upande mwingine, misaada kutoka kwa washirika wa maendeleo inakadiriwa kuwa Sh563.1 bilioni pekee, sawa na asilimia 0.9 ya bajeti yote, hali inayoonesha utegemezi mdogo wa misaada ikilinganishwa na mapato ya ndani.

Kwa mtazamo wa kina zaidi, mapato ya kodi pekee yanatarajiwa kugharamia asilimia 59.6 ya bajeti ya Serikali, jambo linaloonesha uzito mkubwa wa kodi katika uendeshaji wa shughuli za Serikali na utekelezaji wa vipaumbele vya maendeleo.

Hayo yameelezwa, Jumatatu Februari 2, 2026 na Waziri wa Fedha, Balozi Hamis Mussa Omary alipowasilisha bungeni mapendekezo ya mwongozo wa maandalizi ya mpango na bajeti ya Serikali katika kipindi cha muda wa kati 2026/27 hadi 2028/29.

Amesema ongezeko la mapato ya ndani linatarajiwa kuchangiwa na misingi imara ya uchumi jumla na utekelezaji wa mikakati mbalimbali ikiwemo kuhimiza matumizi ya mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) katika malipo na ukusanyaji wa mapato.

Pia, amesema Tehama inatumika katika kudhibiti misamaha ya kodi, kurasimisha sekta isiyo rasmi, kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kwa lengo la kuibua vyanzo vipya vya mapato.

Katika kipindi cha muda wa kati kuanzia 2026/27 hadi 2028/29, amesema Serikali inatarajia kukusanya na kutumia Sh204.09 trilioni, sawa na wastani wa Sh68.03 trilioni kwa mwaka, huku mapato yakikadiriwa kufikia wastani wa Sh52.48 trilioni kwa mwaka, sawa na ukuaji wa wastani wa asilimia 12.1.

“Hatua hizi zinaendana na malengo ya uchumi jumla yanayolenga mapato ya ndani kufikia asilimia 17.1 ya Pato la Taifa mwaka 2026/27 na wastani wa asilimia 17.2 katika kipindi cha muda wa kati, pamoja na kudhibiti nakisi ya bajeti isiyozidi asilimia 3.0 ya Pato la Taifa,” amesema.

Kwa ujumla, takwimu hizi zinaonesha kuwa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2026/27 imejengwa kwa msingi mkubwa wa mapato ya ndani, ishara ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha uhuru wa kifedha na uendelevu wa matumizi ya umma.

Mtazamo wa kiuchumi

Kwa mtazamo wa kiuchumi, bajeti hiyo inaashiria kuvuka hatua ya uchumi wa kusaidiwa na washirika wa maendeleo, kuelekea uchumi wa kujisimamia kwa mapato yake, kama inavyoelezwa na Mchambuzi wa Uchumi, Profesa Ibrahim Mwamadzingo.

“Hatua hii inakuwa muhimu zaidi ikizingatiwa baadhi ya washirika wa maendeleo wameanza kupunguza au kuahirisha misaada ya kibajeti. Umoja wa Ulaya (EU), ulitangaza kuahirisha mikataba mipya ya misaada,” amesema.

Kwa hali hiyo, Profesa Mwamadzingo amesema Serikali inalazimika kufanya uamuzi mgumu wa ama kuongeza utegemezi wa mikopo, jambo linaloongeza mzigo wa deni au kuongeza mapato ya ndani.

Amesema bajeti ya 2026/27 inapaswa kusomwa kama hati ya mpito wa kihistoria. Kwa mtazamo wake, lengo la kuongeza mapato ya ndani linapaswa kuangaliwa kama kipimo cha utayari wa Taifa kujitegemea kifedha.

Kwa miaka mingi mapato ya ndani yameshuhudia yakikua, lakini kwa kasi ambayo haikuendana na mahitaji ya matumizi ya Serikali. Sasa, kwa kuzingatia mabadiliko ya mazingira ya kimataifa na mahitaji ya ndani, hakuna nafasi tena ya kuchelewa,” amesema mchambuzi huyo.

Mtaalamu wa sera za uchumi na mipango, Dk Tabia Huza amesema changamoto si kukusanya mapato pekee, bali jinsi yanavyokusanywa.

Dk Huza amesema sekta isiyo rasmi, ambayo inachangia sehemu kubwa ya ajira na shughuli za kiuchumi nchini, imekuwa ikibaki nje ya wigo rasmi wa kodi kwa kiasi kikubwa.

Hata hivyo, ameonya urasimishaji wa sekta hiyo haupaswi kufanywa kwa mtazamo wa adhabu au shuruti, bali Serikali ijenge mazingira yanayofanya wajasiriamali wadogo waone faida ya kuwa sehemu ya mfumo rasmi kupitia upatikanaji wa mikopo, masoko na huduma za kijamii.

Hoja hiyo inaendana na kilichoelezwa katika mwongozo wa bajeti, Serikali ilipopendekeza kutumia rasilimali zilizopo, ikiwemo mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, kuboresha mazingira ya biashara na kuhamasisha urasimishaji.

Kwa mtazamo wa Dk Huza, mikakati hiyo inaweza kuwa chanzo cha mapato ya baadaye endapo itasimamiwa kwa uangalifu na kuzingatia uhalisia wa biashara ndogondogo.

Ukiacha mitazamo hiyo ya wachambuzi wa uchumi, Waziri wa Fedha, Balozi Omary amesisitiza matumizi ya mifumo ya kidijitali katika ukusanyaji wa mapato, akitaja itasaidia kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato na kuongeza uwazi.

Hata hivyo, Mtaalamu wa Uchumi na Biashara, Richard Mwekuyu, amesema mifumo ya ukusanyaji mapato inapaswa kuunganishwa kuanzia wizara, wakala, hadi mamlaka za Serikali za Mitaa ili kila shilingi inayokusanywa ionekane na kufuatiliwa.

Amesema mapato mengi yasiyo ya kodi bado yanapotea kwenye mifumo isiyounganishwa, hususan ada, tozo na huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi za umma.

“Bila uratibu wa mifumo hiyo, lengo la kujitegemea kwa mapato ya ndani linaweza kufikiwa kwa muda mfupi, lakini lisidumu,” ameeleza.

Kwa mtazamo wake, mageuzi ya mifumo ya mapato yanapaswa kwenda sambamba na mageuzi ya kiutawala.

Mwongozo wa bajeti unaelekeza kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji, kulinda wawekezaji wa ndani na kuhimiza sekta binafsi kushiriki zaidi katika uzalishaji.

Kwa tafsiri ya Mwekuyu, hatua hizo ndizo zitakazopanua msingi wa kodi kwa njia endelevu, badala ya kuzunguka kwenye walipakodi walewale kila mwaka.

Kwa kuangalia mwenendo wa miaka ya karibuni, ambapo mapato ya ndani yamekuwa yakifikia au kuvuka malengo yaliyowekwa, amesema lengo lililowekwa linawezekana.

Hata hivyo, amesema mafanikio hayo yatategemea zaidi mabadiliko ya kimuundo kuliko juhudi za taasisi moja. “Ni mtihani wa sera, taasisi, uaminifu wa walipakodi na uwezo wa Serikali kusimamia mageuzi kwa uthabiti,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *