Dar es Salaam. Mwanamuziki nguli, hayati Oliver Mtukudzi kafanya mambo makubwa katika muziki. Mathalani, sanaa aliyotumia katika uandishi wa wimbo wa Todii, na aina ya mdundo mwororo uliojaa kubembeleza na hisia mfano wivu wa kimapenzi ni burudani tosha. Lakini, kinachozungumzwa ndani ya biti hilo ni tofauti.

Lejendari huyo alizaliwa Septemba 22, 1958 na umauti ukamkuta Januari 23, 2019 katika jiji kuu la Harare nchini kwao Zimbabwe, sababu ya kifo chake ikitajwa kuwa ni ugonjwa wa kisukari.

Kwa mujibu wa Wikipedia, alianza muziki 1977 akiimba na kupiga gitaa, ambapo alishirikiana na kampuni ya Putumayo World Music na Tuku Music. Pia kacheza filamu na baadhi alizohusika nazo ni Jit iliyotoka 1990, Neria (1993), Shanda (2002, ikarekebishwa 2004), Sarawoga (2009) na Nzou NeMhuru Mudanga (2012).

Baada ya albamu yake ya Dzangu Dziye kufanya vizuri 1998 mwaka 1999 alitoa albamu ya Tuku Music na ndani yake ndimo ulimo wimbo wa Todii unaotumika zaidi katika mambo ya kijamii hasa yanayohusu afya.

Japokuwa hayupo duniani nyimbo zake kama Todii na Neria zinaendelea kuvuta hisia ingawa hazijaimbwa kwa Kiingereza, lugha ambayo ingekuwa rahisi kueleweka zaidi.

Mtukudzi, aliyesifika kwa upole na unyenyekevu aliimba zaidi nyimbo za kitamaduni zilizovuka mipaka hadi nchi nyingine zisizotumia Kizimbabwe. Mwananchi linakuletea alichomaanisha katika wimbo wa Todii uliojaa hisia kali zinazolazimisha sikio kutenga muda kuusikiliza.

MAANA YAKE

Wimbo wa Todii unazungumzia maumivu ya kiwango gani ukijua mtu anapopata ugonjwa utakaosababisha kifo na  ukijua amepata maambukizi ya Ukimwi. Mtukudzi alilenga zaidi kuelimisha jamii kuhusiana na ugonjwa huo.

Katika video ya wimbo huo inaonyesha watu makaburini wakizika, wakiwa wamejawa na huzuni na kipande kingine kinamuonyesha Mtukudzi akiingia katika nyumba fulani kuwapa pole wafiwa.

Neno “hooo Todii Senzeni” kwa Kiswahili linamaanisha “utafanya nini?”; Zvinorwadza sei kurera rufu mumaoko ikimaanisha “inauma kiasi gani kumtunza mtu unayejua hatima yake ni kifo”; Uchadii uinawo utachiwana maana yake ni “ukijua ana Ukimwi”; Bva zvapabata pamuviri pasina raramo akimaanisha kifo kimeonekana wazi.

Baadhi ya albamu zake nyingine ni Shanje na Pfambi alizotoa 1981, Maungira na Please Ndapota (1982), Nzara, Oliver’s Greatest Hits 1983. Inaelezwa wakati wa uhai wake alitoa albamu zaidi ya 40.

Baadhi ya tuzo alizotuzwa mwanamuziki huyo ni pamoja na ile ya Kora ya mtayarishaji bora wa Ndakuwara 2002, National Arts Merit Awards (NAMA) aliyochukua 2004 kama mwanamuziki bora wa kiume katika kipengele cha  Lifetime Achievement Award 2003. Pia alituzwa na Reel Award katika lugha bora ya Kiafrika 2003.

Uandishi wa mashairi yake unatoa somo kwa wanamuziki wengine kama anavyoeleza mkongwe wa Bongofleva, 20 Percent aliyewahi kutamba na nyimbo kama Tamaa Mbaya, Maisha ya Bongo na Binti Kimanzi, kwamba unaleta heshima katika maisha.

“Wasanii wengi wanaimba nyimbo zisizoishi, zinazovuma kwa muda mfupi kisha zinapotea. Lakini, tuna wajibu wa kuacha alama kwa jamii. Tutoe funzo na burudani,” anasema msanii huu ambaye jina lake kamili ni Abbas Hamis.

Msanii mwingine wa Bongofleva, Kheri Sameer Rajabu maarufu Mr Blue anasema: “Wasanii wengi wa sasa unakuta anaingia studio anatoa wimbo kwa siku moja. Kiukweli, inatakiwa mashairi yaishi kwa jamii; mfano mzuri ni Mtukudzi, ujumbe wake wa Todii unaishi na utaishi.” 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *