HISTORIA mpya inaenda kuandikwa. Sasa ni rasmi Yanga imepata mzabuni aliyeshinda tenda ya kujenga uwanja wa klabu hiyo baada ya awali kutangaza mchakato huo na kutoa fursa kwa aliye tayari kuomba.

Kampuni ya GSM, ndiyo imetangazwa kushinda tenda hiyo ya ujenzi wa uwanja utakaofanyika maeneo ya Jangwani jijini Dar es Salaam, yalipo makao makuu ya Yanga, huku washindani wengine walioomba tenda hiyo wakifichwa.

Baada ya hesabu ndefu, klabu hiyo iligundua kwamba, inahitaji nyongeza ya ardhi na umiliki ambao Serikali iliipatia ndani ya siku 100 tangu walipotangaza nia ya kujenga uwanja huo, ndipo walipoanza mchakato wa kusaka mzabuni.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe, amesema kampuni ya GSM imeshinda kutokana na kufikia vigezo vilivyowekwa.

Ally amesema, mbali na GSM, kuna kampuni nyingine zimejitokeza kwa ajili ya kuweka mabango ya matangazo uwanja mzima pale utakapokamilika.

“Baada ya GSM kushinda, hatua inayofuata ni kuijulisha kampuni hiyo na umma, baada ya hapo pande zote mbili zitakutana ambazo ni klabu na mdhamini, ili kuweza kupanga mipango ya kuanza kazi hiyo.”

Amesema kuwa, licha ya kuwa na wadhamini mbalimbali, walichozidiwa na mdhamini mpya ni vigezo walivyoviweka katika nafasi hiyo ya ujenzi wa uwanja.

“Bado tupo kwenye mazungumzo ya mdhamini mpya, ndiyo maana kuna kamati ya utendaji na wapo wajumbe ambao wanaongozwa na rais wa klabu yetu, Hersi Said.

“Lakini wameongezeka wawili ambao ni Mwanasheria Alex Mgongolwa, ambaye ataisaidia klabu kwenye makubaliano hayo kwa upande wa sheria.

“Mjumbe wa pili ni Ivan Tarimo, ambaye atawasaidia kwa upande wa biashara kwani ana uzoefu mkubwa, hivyo ataongeza nguvu zaidi kwa upande wa kibiashara,” amesema Ally.

UWA 03

Aliongeza: “Kamati hiyo inakwenda kutekeleza majukumu makubwa mawili ambayo ni ya kisheria na kibiashara kati ya klabu ya Yanga na kampuni ya GSM.”

Hapo awali, Yanga ilitangaza kutaka mdhamini wa kimkakati, wawekezaji, wabia, makundi ya ushirikiano wenye sifa na uwezo wa kifedha, na walitakiwa kuwasilisha barua za kuonyesha nia kwa ajili ya kuendeleza eneo hilo la Jangwani/ Twiga Street (zamani Uwanja wa Kaunda), katika kiwanja cha wazi kwa lengo la kutekeleza mradi wa ujenzi wa uwanja wa kisasa chini ya mpango wa ushirikiano na ubia wa muda mrefu.

Yanga ambayo Februari 11, 2025 ilisherehekea kutimiza miaka 90 tangu ilipoasisiwa mwaka 1935, mwaka huu inaingia mwaka wake wa 91 na kwa miaka mingi imekuwa haina uwanja wake wa mechi, ukiacha Uwanja wa Kaunda, ambao ulitumika kwa mazoezi miaka ya nyuma kabla ya kubomoka kwa mafuriko ya maji pembeni ya makao makuu ya klabu hiyo.

Yanga inapanga kujenga uwanja mpya mahali ulipokuwapo Uwanja wa Kaunda baada ya miaka mingi ya kuhangaika huku na huko kukodi viwanja kwa ajili ya mechi zake za nyumbani na hata kwa mazoezi.

UWA 02

Katika miaka ya hivi karibuni imekuwa ikitumia viwanja vya Avic Town vya GSM kwa mazoezi na ilipewa eneo Kigamboni na alioyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ambaye sasa ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Eneo la Jangwani linatajwa kuvutia zaidi uwekezaji wa uwanja kwa kuwa liko ndani ya eneo la kibiashara la Kariakoo na linaweza kuipa klabu hiyo vyanzo vya mapato ya kulipia gharama za ujenzi huo, ambao hugharimu mabilioni ya pesa.

VIGEZO HITAJIKA

Muundo mkuu wa uwanja huo ni sehemu za kukaa watazamaji, uwezo wa uwanja unapaswa kuwa na viti 25,000 hadi 35,000 vya kuketi, asili ya pitch inapaswa kuwa ‘hybrid’ (mchanganyiko), mfumo wa uwanja wa kuchezea, mifereji ya maji na umwagiliaji.

Maeneo ya VIP/ huduma maalum, vyombo vya habari, matangazo na uendeshaji, mifumo ya usalama na  mifumo ya taa za uwanja.

Pia mifumo ya umeme na huduma nyinginezo, maegesho, barabara za kufikia, kazi za nje na upandaji miti/ulimaji (mahitaji ya mwisho yatatolewa wakati wa hatua inayofuata kwa washirika walioorodheshwa/ wanaovutiwa).

UWA 01

KITUO KINACHOFUATA

Wakati mchakato huo wa ujenzi wa uwanja ukimaliza jambo hilo la mzabuni, Yanga inayoshiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi, kwa sasa inajipanga kwenda nchini Morocco ambako itaanza safari leo ya kwenda kusaka alama tatu dhidi ya AS FAR Rabat, ambao katika mchezo wa kwanza waliwachapa bao 1-0.

Katika michuano hiyo, Yanga ipo Kundi C ikiwa inashika nafasi ya pili, ikiongozwa na Al Ahly ya Misri yenye pointi nane, huku Wanajangwani wakiwa na pointi tano sawa na FAR Rabat.

Yanga itakutana na FAR Rabat Jumamosi ya Februari 7, 2026 muda wa saa 4:00 usiku, kwenye Uwanja wa Olimpic ulioko Rabat Morocco.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *