Dar es Salaam. Kwa kipindi kirefu, tasnia ya Bongo Fleva ilitawaliwa na sauti za wanaume, huku wanawake wakionekana wachache waliokuwa wakipambana kutafuta nafasi katikati ya ushindani mkali.
Lakini kadri muda ulivyokwenda, hali imebadilika kwa kiasi kikubwa. Ndani ya miaka ya hivi karibuni, wanawake wamechukua usukani, wakitoa vibao vinavyosumbua chati, vinavyochezwa kwenye redio, runinga, majukwaa ya kidigitali na kwenye shoo kubwa za ndani na nje ya nchi.
Mapinduzi hayo hayakuja kwa bahati mbaya. Ni matokeo ya kazi kubwa, uwekezaji, uthubutu na uelewa wa soko. Mwanamke wa sasa kwenye muziki anajua nini mashabiki wanahitaji, anajua namna ya kuonekana, kuwasiliana na hadhira na kutengeneza ‘brand’ ya muda mrefu.
Leo hii unaweza ukataja nyimbo kumi bora zilizochezwa kwa kipindi fulani na ukakuta nusu au zaidi ni za wasanii wa kike. Hii ni ishara kuwa mlango umefunguka, na walioupitia wameamua kuacha alama.
Hawa hapa ni baadhi ya wanawake ambao wamekuwa na ushawishi mkubwa katika soko la Bongo Fleva kwa miaka ya mitano mfululizo.
Ni vigumu kuzungumzia mafanikio ya wanawake kwenye muziki wa sasa bila kutaja jina la msanii Zuhura Othuman ‘Zuchu’. Tangu ajiunge na WCB 2020, amekuwa kama kiwanda cha vibao. Sukari, Honey, Kwikwi, Cheche, Litawachoma, Napambana, Utaniua na Jaro ni kati ya nyimbo zilizopata mapokezi makubwa ukiachilia mbali uhusiano wake na bosi wake ambaye kwa sasa ni mume wake Diamond Platnumz.
Amefanikiwa kuwa msanii wa kike mwenye nguvu ya kibiashara, kuvunja rekodi za watazamaji na kuwa na mashabiki wa rika zote.
Alitunukiwa tuzo ya Silver Play Button na mtandao wa kijamii wa YouTube kwa kuwa msanii wa kwanza wa kike Afrika ya Mashariki kwa kufikisha wafuasi zaidi ya 100,000 ndani ya wiki moja.
Ndani ya miaka mitano tangu atambulishwe kwenye lebo ya Wasafi, Zuchu alitunukiwa tuzo ya msanii bora chipukizi wa mwaka 2020 kupitia All Africa Music Awards AFRIMMA, miaka miwili baadaye atateuliwa kuwania tuzo za MTV EMAs akawa mwanadada wa kwanza kutoka Afrika Mashariki kushindania tuzo hiyo.
Mwaka huo huo, Zuchu alikuwa msanii wa kike kufikisha subscribers wengi zaidi kwenye YouTube katika Ukanda wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Miezi michache baadaye, aliandika historia nyingine kwa kuwa msanii wa kwanza wa kike Afrika Mashariki kufikisha zaidi ya stream milioni 100 kwenye jukwaa la Boomplay.
Faustina Charles Mfinanga ‘Nandy African Princess’ amedumu juu kwa muda mrefu kwa sababu ya utofauti wake na sauti yake ya kubembeleza ambayo ukiisikia tu ni utambulisho tosha.
Alianza kazi yake ya sanaa ya muziki mwaka 2016 kupitia wimbo wa Nagusagusa miezi michache tu tangu aliposhika nafasi ya pili kwenye mashindano ya kusaka vipaji ya Tecno Own the Stage yaliyofanyika Nigeria.
Mwaka 2017 akashinda tuzo ya All Africa Music Awards (AFRIMMA) katika kipengele cha Msanii Bora wa Kike Afrika Mashariki.
Tangu hapo nyota yake ilianza kung’aa kila anapotoa wimbo, mashabiki wanamsikiliza. Kupitia vibao kama Number One, Kiza Kinene, Usemi Sina, Nikuone, Do Me na sasa Asante, ameendelea kuonyesha kuwa anaelewa mashabiki wanataka nini na kwa wakati gani.
Nguvu yake jukwaani na uwezo wa kuimba live umemuweka kwenye hadhi ya kipekee, amekuwa mfano mzuri kwa wanawake wengi kwamba kuwa mama na mke hakuzuii kupambania ndoto za mwanamke.
Phina ni jina ambalo limepanda kwa kasi sana hivi karibuni. Alianza kazi ya sanaa ya muziki mwaka 2018 na ametamba na kibao kama Upo Nyonyo, SuperWoman, Sisi Ni Wale, Manu na nyingine zimempa nafasi ya kuwa miongoni mwa wanawake wanaotegemewa sana.
Ameunganisha sauti na muonekano kuwa mchanganyiko unaouza sana.
Ikumbukwe Phina alianza kupata umaarufu kupitia mashindano ya kutambua vipaji ya Bongo Star Search mwaka 2018.
Aliwahi kushinda tuzo za TMA kwenye vipengele mbalimbali ikiwemo ile ya mwanamuziki wa kike chipukizi mwaka 2021, Best Female Perfomer na Best Performer Collaboration mwaka 2022, hayo ni mafanikio makubwa kwa binti wa miaka 30, na ni funzo kwa wanawake wengine wenye vipaji vya kuimba.
Hip Hop sio muziki unaofanywa na wadada wengi kutokana na aina yake ukionekana kama muziki fulani mgumu na unafanywa zaidi na wanaume, lakini hali imebadilika kwa sasa, mabinti wadogo wanaufanya tena kwa ukubwa.
Miongoni mwao ni Rosary Robert ‘Rosa Ree’ ameendelea kusimama kama nembo ya wanawake anajulikana kwa ngoma zake kama Way Up, Dowtown, Mama Omolo, Champion ni baadhi ya kazi zilizompa heshima.
Rosa Ree alianza kupewa sikio kubwa baada ya kuachia ngoma kama
One Time (2016), Up in the Air (2017) ngoma zilizofanya vizuri na kumfungulia milango ya kujulikana.
Rosa Ree alishinda tuzo za East Africa Arts & Entertainment Awards (EAEA) kama Msanii Bora wa Kike wa Hip Hop 2022, hiyo ikiwa na maana kuwa muziki wake umetoka nje ya Bongo kwa sababu tuzo hizo ni kwa wanaofanya vizuri Afrika Mashariki.
Maua Sama ni miongoni mwa waimbaji wenye sauti inayobeba hisia ya mapenzi. Kupitia nyimbo kama Iokote, Wamekata, Nioneshe, pamoja na kolabo kadhaa, ameendelea kudhihirisha ubora wake na kukubalika kwa muda mrefu, huku ladha ya ngoma zake ikiwavutia wasikilizaji wake kila wanapomsikia.
Alianza kazi ya muziki mwaka 2013 baada ya kugunduliwa na rapa na mwanasiasa wa Tanzania Mwana FA. Wawili hao walishirikiana katika wimbo ‘So Crazy’ mwaka huo huo.
Mnamo mwaka 2015, Maua Sama alitoa wimbo wake wa kwanza rasmi ulioitwa “Let Me Know”, uliompa umaarufu zaidi kwa wasikilizaji wa muziki wa Tanzania.
Abigail Chams
Moja kati ya wasanii wenye umri mdogo wanaofanya vyema katika tasnia ya muziki akiweka rekodi ya kufanya ngoma na mastaa wakubwa wanaofanya vizuri kama Marioo na Konde Boy ‘Harmonize’.
Abigail ameonyesha mwelekeo wa soko la dunia. Uwezo wake wa kutumia vyombo vya muziki na kufanya kolabo na majina makubwa umemfanya aonekane kama daraja kati ya Bongo Fleva na soko la nje.
Amesaini mkataba na Sony Music Africa na alipata kutambulika kimataifa kufuatia uteuzi wake katika Tuzo za BET za mwaka 2025 kwenye kipengele cha Best New International Act, na hivyo kuwa msanii wa kwanza mwanamke kutoka Afrika Mashariki kupata uteuzi huo.
Mbali na muziki wake, Chams ni Balozi wa Vijana wa UNICEF, alikuwa balozi wa mpango wa Spotify EQUAL Africa mwaka 2023, na pia ni mwanzilishi wa mpango wa The Talk With Abigail Chams unaojikita katika afya ya akili na uwezeshaji wa vijana.
Jina halisi ni Yasirum Yasin Shaaban alianza kusikika kupitia Tiktok, baada ya kuanza kufanya challenges za nyimbo za wasanii wakubwa nchini Tanzania na India.
Ndipo Nandy alipokiona kipaji cha Yammi na kutambulishwa kama msanii mpya kwenye label ya the African Princess na ngoma tatu ikiwemo Ep na iliyoitwa THREE HEARTS.
Huu ni mfano mzuri kwa binti mdogo ambaye aliamua kutumia mitandao wa kijamii vizuri na mpaka sasa umekuwa chanzo cha umaarufu na kipato, lakini huwezi kuacha kumpongeza Nandy aliyemuinua mwanamke mwenzake na kumpa fursa kubwa zaidi.
WAMEBADILISHA MCHEZO
Kitu kikubwa walichokifanya ni kuonyesha kuwa wanaweza kuhimili presha ya soko. Wanaachia nyimbo mara kwa mara, wanafanya promosheni, wanapiga shoo na wanabaki kwenye midomo ya mashabiki kila siku.
Pia wamejifunza kutumia nguvu ya mitandao. Leo hii wimbo unaweza kuanza TikTok kabla hata haujapigwa redioni, na wanawake wamekuwa mabingwa wa eneo hilo.
Wewe kama Mwanamke au kijana unaesoma makala hii unaweza kujifunza kitu hata kama sio kwa wasanii wote lakini naamini kuna mmoja ambaye anaukosha moyo wako na hiyo ndio safari, lakini hakuna aliyeanzia juu hivyo usiogope anzia hapo hapo.