Katika mkutano huo muhimu wajumbe kutoka zaidi ya nchi 120 wamekusanyika kuadhimisha miaka 20 ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa na kuthibitisha tena dhamira ya pamoja kwa sheria za kimataifa, wakati dunia ikikabiliwa na kuyumba kwa hali ya usalama, vita na migogoro inayoibuka upya.
Akikiri hali ya sintofahamu ya kijiografia inayoambatana na migogoro katika maeneo mbalimbali ikiwemo Gaza, Myanmar, Ukraine, Sudan na kwingineko, Bwana. Guterres ameliomba Baraza kusimama kidete kulinda haki za binadamu, akionya kwamba ziko chini ya “mashambulizi makubwa na mara nyingi yakiongozwa na wale wenye mamlaka makubwa zaidi”.
Kuhusu Ukraine hasa, mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amebainisha kuwa kesho Jumanne tarehe 24 Februari itakuwa kumbukumbu ya miaka minne tangu kuanza kwa uvamizi kamili wa Urusi dhidi ya Ukraine, ambao umeua zaidi ya raia 15,000. Amesisitiza kuwa “Umeshapita muda wa kumaliza umwagaji damu”.
Kauli yake imefuatia ile ya Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk, ambaye ametaka haki na uadilifu viwe kiini cha usitishaji mapigano au makubaliano yoyote ya amani.
Kamishina Mkuu wa UN wa Haki za Binadamu akihutubia Baraza la Haki za Binadamu Gebeva Uswisi
Ukimya una madhara
Akirejea wasiwasi huo katika kikao hicho cha Baraza la Haki za Binadamu Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Annalena Baerbock amesisitiza kuwa haki za binadamu si “mchezo wa watazamaji tu ni jukumu kwa nchi wanachama wa Baraza, wawakilishi, mawaziri au maafisa wa Umoja wa Mataifa, kwani ukimya ni chaguo na una madhara”.
Bi. Baerbock ameongeza kuwa “Historia inatufundisha kuwa mifumo mikubwa mara chache huanguka kwa tukio moja la ghafla, hudhoofika polepole, kanuni baada ya kanuni, ahadi baada ya ahadi, huku wale waliopaswa kuilinda wakibaki kimya. Hadi siku moja, kile kilichoonekana kuwa cha kudumu hupotea.”
Katika hotuba yake ya ufunguzi, ameangazia hali inayoendelea ya wanawake wa Afghanistan ambao chini ya amri mpya ya Taliban, inaripotiwa kuwa wanaweza kupigwa na waume zao mradi tu hakuna alama zinazoonekana.
“Tunapaswa kukumbuka mara moja na kwa yote kuwa kuridhia ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu kamwe hakuleti ushindi,” amesema. “Tunashuhudia sio tu kurudi nyuma kwa haki za wanawake, bali pia haki za binadamu na kanuni na viwango vingine vilivyoaminika kuwa vya kudumu, ambavyo sasa vinahojiwa wazi, vinapuuzwa au vinakiukwa.”
Watoto wa Ukraine wamulikwa
Rais wa Baraza Kuu pia ametoa wito wa “dhamira ya wazi kutoka kwa kila Nchi Mwanachama kwamba utekaji wa watoto wa Ukraine ni uhalifu wa kivita,” akirejea kuhusu watoto waliotenganishwa na familia zao tangu mwaka 2014 wakati Moscow ilipoiteka Crimea wakiwemo wale waliokuwa wamehamishwa ndani ya maeneo ya Ukraine yaliyochukuliwa na wale waliohamishwa hadi Urusi.
Haki za binadamu ziko pamoja nawe
Suluhu ya mataifa mawili yaporwa
Kuhusu Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na Israel, ambako upanuzi wa makazi ya walowezi wa Israeli unaongezeka kwa kasi, Bwana. Guterres ameonya kuwa suluhisho la mataifa mawili “linaporwa mchana kweupe. Jumuiya ya kimataifa haiwezi kuruhusu hilo litokee.”
Na huku migogoro ikiongezeka na wachochezi wake kuendelea kutenda bila kuwajibishwa, Guterres amesisitiza kuwa hali hiyo inatokana na serikali kupuuza haki za msingi za binadamu zilizoainishwa katika sheria za kimataifa, wakati ambapo mahitaji yanaongezeka kwa kasi na ufadhili ukiporomoka.
Ukweli usiopendeza
“Tunaishi katika dunia ambako mateso makubwa ya watu yanafutwa kwa visingizio, ambako binadamu wanatumiwa kama karata za mazungumzo, ambako sheria za kimataifa zinachukuliwa kama kero tu,” amesisitiza.
Katika hotuba yake ya mwisho kwa Baraza la Haki za Binadamu kama Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kabla ya muhula wake wa pili wa miaka mitano kumalizika tarehe 31 Desemba, Bwana. Guterres amerejea wasiwasi wake wa muda mrefu kuhusu vichocheo vya ukosefu wa usalama na ukosefu wa usawa ambavyo vimewaacha wahamiaji “wakinyanyaswa, kukamatwa na kufukuzwa”, wakimbizi wakitupiwa lawama na jamii za LGBTIQ+ zikichafuliwa.
“Nchi zinazama katika madeni na kukata tamaa, na machafuko ya tabianchi yanaongezeka,” ameongeza, hasa kwa mataifa madogo na yaliyo hatarini yanayokosa uwekezaji wa kutosha.
Teknolojia ya Akili Mnemba inaendelea kwa kasi.
Mipaka ya mgawanyiko ya AI
Hata teknolojia na hasa akili mnemba au AI inazidi kutumiwa “kukandamiza haki, kuongeza pengo la usawa na kuwaweka watu waliotengwa katika hatari ya aina mpya za ubaguzi mtandaoni na nje ya mtandao,” ameonya mwanadiplomasia huyo mkuu wa dunia, kabla ya kutoa wito wa kuimarishwa kwa dhamira ya maadili ya mshikamano wa kimataifa yaliyoainishwa katika Mkataba wa Umoja wa Mataifa.
“Haki za binadamu si za Magharibi au Mashariki, Kaskazini au Kusini, si anasa, na hazijadiliwi. Ndizo msingi wa dunia yenye amani na usalama zaidi. Na Mataifa yanafungwa na wajibu wao chini ya Mkataba na sheria za kimataifa.”
Akifafanua zaidi hoja hiyo, Kamishina Mkuu wa Haki za Binadamu Türk amesema kuwa wakati baadhi ya serikali zinadhoofisha mfumo wa ushirikiano wa kimataifa, ukiukwaji wa sheria za kimataifa “lazima utajwe wazi, bila kujali wahusika”.
Ili kukabiliana na “utawala wa juu kwenda chini” wa sasa, Kamishna Mkuu huyo ametangaza uzinduzi ujao wa Muungano wa Kimataifa wa Haki za Binadamu wa Ofisi yake, utakaoleta pamoja Mataifa, biashara, miji, wafadhili, wanasayansi, wasanii, wanafalsafa, vijana na asasi za kiraia.
Bwana. Türk amesisitiza kuwa “Mustakabali wetu unategemea dhamira yetu ya pamoja ya kutetea haki za kila mtu, kila wakati, kila mahali”.