Ajali hiyo ilitokea Jumamosi wakati wahamiaji hao walipokuwa wakijaribu kufika Ugiriki kupitia njia hatari ya Bahari ya Mediterania.

Watu 20 waliokolewa, wakiwemo watoto wanne. Miili ya wanaume watatu na mwanamke mmoja ndio imepatikana hadi sasa.

Boti hiyo iliondoka Tobruk, Libya, tarehe 19 Februari na kupinduka takribani maili 20 majini kusini mwa Kali Limenes, kisiwa cha Krete. Walionusurika ni wanaume 16 na watoto wanne.

“IOM inaomboleza kupotea kwa maisha katika tukio jingine la kutisha katika Bahari ya Mediterania,” msemaji wa shirika hilo amesema. “Tunatoa wito wa kuimarishwa kwa juhudi za utafutaji na uokoaji katika Bahari ya Mediterania ya Kati ili kuokoa maisha na kuhakikisha wahamiaji wanashushwa salama, pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kikanda.”

Mwanzo mbaya zaidi wa mwaka

Kwa mujibu wa Mradi wa Wahamiaji Waliopotea wa IOM, takriban wahamiaji 606 wameripotiwa kufa maji au kutoweka katika njia ya Bahari ya Mediterania katika miezi miwili tu ya kwanza ya mwaka 2026.

Huu ni mwanzo mbaya zaidi wa mwaka kuwahi kurekodiwa tangu IOM ianze kukusanya takwimu hizo mwaka 2014.

“Takwimu hizi zinaonesha hali ya dharura inayoendelea katika Bahari ya Mediterania,” msemaji huyo wa IOM ameonya. “Bila hatua za haraka na za pamoja, idadi ya vifo itaendelea kuongezeka.”

Mitandao ya usafirishaji haramu yalaumiwa

IOM imeonya kuwa mitandao ya biashara haramu ya binadamu na usafirishaji haramu wa wahamiaji inaendelea kuwadhulumu watu katika njia ya Mediterania ya Kati.

Makundi hayo hunufaika kwa kuwasafirisha wahamiaji katika boti zisizofaa baharini, huku wakiwaweka katika hatari kubwa ya dhuluma na ukiukwaji wa haki zao.

“Ushirikiano thabiti wa kimataifa na mikakati inayozingatia ulinzi wa wahamiaji ni muhimu kukabiliana na mitandao hii ya kihalifu,” ameongeza msemaji huyo. “Ni lazima pia kupanua njia salama na halali za uhamiaji ili kupunguza hatari na kuokoa maisha.”

Tukio hili la karibuni linaongeza shinikizo kwa nchi za Ulaya na washirika wao kuimarisha operesheni za uokoaji na kushughulikia mizizi ya safari hatari zinazowalazimu maelfu ya watu kuvuka bahari kila mwaka kwa matumaini ya usalama na maisha bora.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *