Kuongezeka huko kwa mapigano kunakuja huku hatari za ulinzi kwa raia na wahudumu wa misaada zikiongezeka, ambapo wahudumu watatu wa kibinadamu waliuawa kati ya tarehe 7 na 16 Februari katika majimbo ya Jonglei na Upper Nile, kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu  na Masuala ya Dharura OCHA.

Ufikiaji wa baadhi ya maeneo yaliyoathiriwa vibaya zaidi bado hauko sawa licha ya ahadi mpya za mamlaka kuruhusu operesheni za misaada.

Ijumaa iliyopita, Mratibu wa Misaada ya Dharura Tom Fletcher aliwasili nchini humo kwa ziara ya siku tano ili kuhamasisha umakini wa kimataifa kuhusu kile alichokieleza kuwa ni mgogoro unaozorota na kuripotiwa kidogo.

“Hapa Sudan Kusini, mnakutana na dhoruba kamili ya mabadiliko ya tabianchi, migogoro, ukosefu wa usawa na umaskini,” amesema Bwana. Fletcher alipowasili. “Kwa sasa, watu hapa Sudan Kusini wanahisi kuwa hakuna anayewasikiliza.”

Wimbi la watu kuhama makazi yako

Mapigano kati ya Vikosi vya Ulinzi vya Watu wa Sudan Kusini  ambbalo ni jeshi la taifa na wanamgambo wa Jeshi la Ukombozi wa Watu wa Sudan–Upinzani SPLA-IO, yaliyoanza tena mwishoni mwa Desemba, yamesababisha wimbi kubwa la watu kuyahama makazi yao katika maeneo ya kati na kaskazini mwa Jonglei.

Kwa mujibu wa mamlaka za Sudan Kusini, karibu watu 280,000 wamekimbia makazi yao katika kaunti nane, wengi wao wakielekea majimbo ya Upper Nile na Lakes.

Familia nyingi zinaishi katika maeneo ya wazi au katika makazi ya muda, zikiwa na mahitaji ya dharura ya chakula, huduma za afya na mahitaji ya msingi. Masoko na shughuli za kilimo zimevurugika, na kuziacha baadhi ya jamii bila au kuwa na upatikanaji mdogo sana wa chakula.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP limeongeza misaada ya chakula, lakini mapigano na ukosefu wa usalama ikiwemo uporaji wa misafara ya misaada vinakwamisha juhudi hizo.

Mkuu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Tom Fletcher (kushoto) anatembelea Hospitali ya Kaunti ya Akobo katika Jimbo la Jonglei nchini Sudan Kusini.

Mkuu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Tom Fletcher (kushoto) anatembelea Hospitali ya Kaunti ya Akobo katika Jimbo la Jonglei nchini Sudan Kusini.

Watu wamenasa katikati ya mapigano

Katika eneo la Akobo, kusini mwa jimbo la Jonglei, Bwana. Fletcher alitembelea hospitali ya eneo hilo ambapo angalau wagonjwa 93 waliokuwa na majeraha ya risasi walikuwa wamehudumiwa kufikia tarehe 18 Februari.

“Raia hawapaswi kamwe kuwa shabaha,” amesema baada ya kukutana na waathiriwa waliomjumuisha mtoto wa miezi 18 na nyanya mwenye umri wa miaka 70.

Katika hospitali hiyo, muhudumu wa misaada alisimulia kwamba “Baba alipigwa risasi. Mama alitekwa.” Bibi huyo alitembea kwa siku saba kutafuta msaada. Alipoulizwa kama amepata chakula, Bwana. Fletcher alisema “Hakuna chakula.”

Ameongeza kuwa baadhi ya jamii zinakaa “wiki kadhaa bila msaada wanaouhitaji,” akieleza “simulizi za kusikitisha za ukatili wa kingono, njaa kali na watoto wanaowasili wakiwa wamepoteza kila kitu.”

Kipindupindu chasambaa

Mapigano hayo yameathiri vibaya huduma za afya. Vituo 13 vimeripotiwa kuharibiwa au kuporwa, na kusababisha vifo vitatu na majeruhi mmoja miongoni mwa wahudumu wa afya. Katika baadhi ya kaunti, vituo vingi vimeharibiwa au kusitisha huduma.

Wakati huo huo, kipindupindu kinaendelea kusambaa. Kati ya tarehe 11 na 17 Februari, wagonjwa wapya 106 na vifo vitatu wameripotiwa katika kaunti tano. Tangu mlipuko huo uanze Septemba 2024, zaidi ya wagonjwa 98,000  na vifo 1,624 vimeripotiwa kote nchini.

Ufikiaji na uwajibikaji

Ingawa mamlaka zimerudia maelekezo ya kuruhusu upatikanaji wa misaada bila vikwazo, utekelezaji wake bado hauko thabiti. Misafara ya misaada imezuiwa katika baadhi ya maeneo, na vikwazo vya kiutendaji vimepunguza usafiri.

Bwana. Fletcher amesema changamoto hiyo inaenda zaidi ya misaada ya dharura, akihoji “Tunawezaje kufanikisha mchakato wa amani? Tunawezaje kumaliza mgogoro huu? Tunawezaje kutoa usalama kwa watu hapa? Lakini pia, tunawezaje kuvuka kelele, kelele za upotoshaji na kutowajibika?.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *