Mkoa wa Puntland uko kaskazini Mashariki mwa nchi ya Somalia, katika ramani ya bara la Afrika mkoa huu uko katika ncha ya pembe ya Afrika. 

Kwa kawaida katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani mashirika hutuma picha na video za hali ilivyo huko mashinani, na video iliyotuma tarehe 24 Februari 2026 na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP kutoka Puntland inaonesha hali ya ukame huku baadhi ya mifugo ikiwa imekufa. 

Wakazi wa Puntland ni wafugaji na wakulima, kuna video moja inamuonesha mama na mtoto wake wakiwa na mbuzi wao watatu wanaowafuga, wameendea kusaka maji huku na kule, mtoto huyo anapanda mpaka kwenye kichuguu kuangalia kama huko mbaliiiii kuna dalili yoyote lakini hola, maana hata lambo la maji lililojengwa huko Mandhan limekauka kauuu.

Na hiyo ndio hali halisi ya Somalia, ndio maana WFP wiki iliyopita walitoa onyo wakisema kuwa msaada wake wa dharura wa chakula na lishe ambacho ndio kinachookoa maisha ya watu, uko hatarini kusimama iwapo hawatapata ufadhili wa haraka. 

Huko Puntland, Somalia, mimea inakauka, mifugo inakufa kutokana na ukame kwenye eneo hilo, kufuatia mfululizo wa miaka mitatu ya ukosefu wa mvua (Picha ya mwaka 2017).

UNDP Somalia/Said Isse

Huko Puntland, Somalia, mimea inakauka, mifugo inakufa kutokana na ukame kwenye eneo hilo, kufuatia mfululizo wa miaka mitatu ya ukosefu wa mvua (Picha ya mwaka 2017).

Naibu Mkurugenzi wa WFP nchini Somalia Marco Selva, amesema “Somalia iko ukingoni wa mgogoro wa kibinadamu. Kuna mambo mengi yanayozisha hali hiyo. Ukame unaojirudia. Somalia imekuwa ikipitia misimu mitatu bila ya mvua. Tunachokosa ni rasilimali, na tunahitaji rasilimali sasa hivi, tunahitaji kuweza kuzuia kuzorota zaidi kwa hali hii.”

Ukame, kuharibika mazao, mifugo kufa, na watu wengi kuyakimbia makazi yao ndio vinazidisha hali mbaya. 

Mbali ya WFP kusaidia katika upatikanaji wa maji na chakula kwa wananchi, lakini wameonya kuwa msaada wake wa kuokoa maisha nchini Somalia unaweza kusimama ndani ya wiki chache zijazo iwapo rasilimali mpya hazitapatikana mara moja.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watu milioni 6.5 nchini Somalia wanatarajiwa kukabiliwa na viwango vya juu vya njaa vya dharura au zaidi ifikapo mwezi Machi. Hili ni ongezeko la watu milioni 1.7 tangu mwezi Januari. Kati yao, watu milioni mbili wanakabiliwa na njaa kali.

Aidha, zaidi ya watoto milioni 1.8 wenye umri wa chini ya miaka mitano wanatarajiwa kukumbwa na utapiamlo mkali mwaka huu wa 2026, ambapo karibu watoto laki tano wanaweza kuwa katika hali mbaya zaidi ya utapiamlo mkali sana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *