Dar es Salaam. Unaweza kusema kuwa ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) hakujapoa, baada ya aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Tanzania Bara, Omar Dunga, kutarajia kuwasilisha malalamiko yake katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kupinga ushindi wa Mirambo Yusuf kuwa mwenyekiti wa chama hicho.

Hata hivyo, Mirambo amemjibu iwapo ana ushahidi, ni haki yake ya kidemokrasia kuwasilisha malalamiko, na hoja zake zitapimwa, huku akisisitiza ushindi wake ni halali na hauna mashaka.

“Haya ni maajabu, lakini niseme tu kwamba kama amejiridhisha, anaweza kwenda. Binafsi najua alikuwa Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara na alisimamia chaguzi zilizopita, hivyo anafahamu utaratibu. Hakuna shida,” amesema Mirambo.

Dunga, aliyekuwa mshindani wa karibu wa Mirambo, alipata kura 177 huku Mirambo akishinda kwa kura 256 kati ya wajumbe halali 448 waliopiga kura katika mkutano mkuu wa dharura uliofanyika Februari 21, mwaka huu.

Dunga amedai wajumbe wengi hawakuwa halali, hivyo hawezi kukubali kushindwa kwa kura za wajumbe mamluki.

Mchakato wa uchaguzi huo ulianza Februari 20, mwaka huu baada ya Baraza Kuu la Uongozi kuketi, ikiwa ni utekelezaji wa uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa wa kukitaka chama hicho kupata uongozi mpya kwa nafasi tatu za juu, kufuatia uongozi uliokuwepo kukosa uhalali.

Kwa mujibu wa msajili, katika uchaguzi uliofanyika Desemba 18 na 19, 2024, ushindi wa viongozi hao, ikiwemo aliyekuwa Mwenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba, haukuvuka nusu ya kura halali zilizopigwa na wajumbe. Hivyo, uchaguzi ulipaswa kurudiwa ili kukidhi matakwa ya kanuni na Katiba ya chama ya mwaka 1992.

Uamuzi huo wa msajili uliwagawa wanachama katika makundi mawili, moja liliunga mkono na kukubali kuingia katika mchakato mpya wa uchaguzi, huku kundi jingine likifungua kesi mahakamani kupinga hatua hiyo, likidai kuwa Msajili hakuzingatia haki ya msingi ya kuwasikiliza kabla ya kutoa uamuzi.

Baada ya kufanyika kwa uchaguzi huo Februari 21, ambao haukuhudhuriwa na ofisa yeyote kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Dunga ameeleza wasiwasi wake, akisema angejiridhisha kuhusu uhalali wa wajumbe walioshiriki.

Akizungumza na Mwananchi leo, Februari 25, 2026, Dunga amesema baada ya kufuatilia, amefanikiwa kukusanya ushahidi kuwa wajumbe wengi hawakuwa halali. Hivyo, anatarajia kuwasilisha malalamiko yake kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kupinga ushindi wa Mirambo, akidai kuwa ni batili kwa kuwa ulitokana na kura za wajumbe mamluki.

“Wajumbe wengi hawakuwa halali. Nimeangalia daftari la reja na kulinganisha na wajumbe walioshiriki kupiga kura, wengi si halali. Nimekusanya ushahidi kutoka kwa viongozi wa kanda tisa za chama chetu, na sasa nipo katika hatua za mwisho za kuwasilisha malalamiko yangu kwa Msajili wa Vyama vya Siasa muda wowote kuanzia sasa,” amesema.

Amesema siku ya uchaguzi alibaini dalili hizo kwa kuwa sura za wajumbe wengi zilikuwa ngeni kwake. Pia amedai hata haiba na aina ya mavazi yao havikuwa vya kawaida kwa utamaduni wa wajumbe wa chama hicho.

“Siwezi kukubali kuchezewa kwa Katiba ya chama chetu. Naenda kupinga ushindi uliomweka madarakani Mirambo na wenzake kwa kuwa walichaguliwa na wajumbe wasiokijua chama. Ni kama walikusanywa mtaani ili kutimiza akidi,” amesema Dunga.

Dunga amesema chama hicho kina jumla ya wajumbe 670, ambao taarifa zao zinapatikana kutoka wilaya mbalimbali nchini. Amesema kwa kuwa kikatiba hawana mfumo wa mikoa, amejiandaa kuwasilisha ushahidi wote kwa ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuanzia Jumatatu.

Siku ya uchaguzi huo uliofanyika Ukumbi wa Lekham, Buguruni, jijini Dar es Salaam, msimamizi wa uchaguzi huo, Said Miraji, alisoma orodha ya wajumbe walihudhuria hadi kura zinaanza kupigwa, alisema walikuwa wajumbe wa mkutano mkuu ni 533.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *