Bi. McCain ameeleza dhamiara yake ya kuachia wadhida wake katika Shirika la WFP kwa moyo mzito kwani alirejea kazini Januari mwaka huu baada ya likizo ya matibabu kutokana na matatizo ya kiarusi yaliyompata, lakini amesema majukumu mazito ya uongozi yamekuwa yakizuia ahueni yake ya kiafya hivyo hana budi kuondoka.

Hata hivyo amesema uamuzi huo ni miongoni mwa maamuzi magumu zaidi aliyowahi kufanya katika maisha yake kwani kazi hii

“Imekuwa ya kipekee na bado itaendelea kuwa ya kipekee. Nimefanya uamuzi mgumu sana. Madaktari wangu na familia yangu wanataka nirudi nyumbani, bado sijapona kikamilifu. Nimejaribu kwa bidii kuwa na nguvu na kurudi kazini lakini ukweli ni kwamba sijapona.”

Wakati wa uongozi wake, Bi. McCain amesimamia mageuzi makubwa ya kuimarisha uwezo wa WFP kusaidia watu wanaokabiliwa na njaa katika maeneo ya migogoro na majanga ya tabianchi. Shirika hilo linatoa msaada wa chakula kwa mamilioni ya watu duniani wanaohitaji msaada.

Cindy McCain, Mkurugenzi Mtendaji wa WFP, anazungumza na mtoto katika hema la muda wakati wa ziara yake huko Deir al-Balah huko Gaza, akisisitiza juhudi zinazoendelea za msaada wa chakula kwa watoto wenye utapiamlo mkubwa.

© WFP/Ali Jadallah

Mkuu wa WFP, Cindy McCain, anatembelea Gaza Agosti 2025.

Chini ya uongozi wake, WFP pia imeongeza ushirikiano na wadau ili kuboresha teknolojia za kidijitali katika usambazaji wa chakula. Cyndy McCain anasema imekuwa heshima  kubwa kwa maisha yake kuhudumu katika shirika hili.

Na alitumai angekamilisha muda wake, lakini afya yake ndio imemuangusha hata hivyo amesisitiza kuwa

“Kitu kimoja ninachojua ni kwamba hii ni kazi yenye mahitaji makubwa sana. Na yeyote atakayechukua kazi hii lazima awe tayari kuipa si asilimia 100 tu, bali asilimia 150 kwa sababu ni kazi ngumu sana kutoipa hivyo. Hivyo, nataka kuondoka na hili. Nitawakumbuka, nakushukuru kwa urafiki wanu na nakushukuru kwa kila mnachofanya kwa WFP, nyie ni bora, asante.”

Sasa Bodi ya Utendaji ya shirika hilo la mpango wa chakula itaanza maandalizi ya uongozi wa mpito na wakati huo WFP imesema shughuli na mipango ya msaada itaendelea bila kuathiriwa.

Bi. McCain ameiongoza WFP tangu 2023, akisimamia mageuzi ya kuboresha ufanisi na kupanua wigo wa msaada wa kuokoa maisha.

Kuondoka kwake kunakuja wakati changamoto za njaa duniani zikiendelea kuongezeka, huku migogoro na mabadiliko ya tabianchi vikichochea uhaba wa chakula katika maeneo mengi duniani.

Pamoja na changamoto maafisa wa WFP wanasema shirika hilo linaendelea kujitolea kusaidia jamii zilizo hatarini huku mchakato wa kumpata kiongozi mpya ukianza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *