1. Yastaajabisha viongozi kuhaha kukandamizi taasisi za kimataifa za haki – Türk
Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu Volker Türk ameonya kuwa shinikizo linaongezeka duniani kote dhidi ya haki za wanawake, uhuru wa kiraia na taasisi za kimataifa akitoa wito kwa serikali kujitolea upya katika ushirikiano, uwajibikaji na utawala wa sheria.
Mambo hayo matatu ninayoangazia ni sehemu tu ya hotuba yenye kurasa 12 aliyoitoa Kamishna Türk mbele ya wajumbe wanaoshiriki mkutano wa 61 wa Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu huko Geneva, Uswisi, hotuba iliyorambaza dunia nzima ikimulika hali tete ya haki za binadamu Ulaya, Amerika, Asia na Afrika kwamba zinasiginwa na chaguzi zinakiuka taratibu.
Mathalani, “mamlaka nchini Cameroon na Uganda zilitumia nguvu kupita kiasi, zikawakamata wapinzani wa kisiasa na wakosoaji, na kuweka vikwazo vikali dhidi ya nafasi ya kiraia kabla, wakati na baada ya uchaguzi. Katika hatua inayokaribishwa, Tanzania ilianzisha Tume ya Kitaifa kuchunguza ukiukwaji uliofanyika wakati wa uchaguzi wa mwezi Oktoba.”
Volker Türk, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, anatoa taarifa yake ya kimataifa kuhusu kikao cha 61 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa katika Palais des Nations mjini Geneva.
Kuhusu haki za wanawake, Türk amesema wanawake na wasichana wanakabiliwa na ubaguzi na vurugu vinavyozidi kuongezeka, akitolea mfano Afghanistan ambako amesema mfumo wa utengaji uliowekwa dhidi ya wanawake unafanana na ubaguzi wa rangi — lakini umejengwa juu ya jinsia badala ya rangi.
Akirejelea kashfa za unyanyasaji zilizotikisa dunia kama kesi ya Jeffrey Epstein, amesema, “unyanyasaji wa kutisha kama huu unawezeshwa na mifumo inayowanyamazisha wanawake na wasichana, na kuwalinda wanaume wenye nguvu dhidi ya uwajibikaji.”
Wakati huu ambapo mizozo inashamiri kila kona ya dunia, Kamishna Mkuu ameshangazwa na baadhi ya viongozi kutochukua hatua kudhibiti mizozo, “badala yake, baadhi yao wanashambulia taasisi zilizoundwa kutulinda — Umoja wa Mataifa, Mahakama ya Kimataifa ya Haki; Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, Baraza hili, na mifumo yake. Ningependa waelekeze muda na nguvu zao katika changamoto halisi — kwa mfano, mashindano ya matumizi ya silaha za nyuklia yanayoendelea kushamiri mbele ya macho yetu.”
Ameonya kuwa kupuuzwa kwa sheria za kimataifa kunachochea migogoro zaidi na mateso kwa raia.
Akizungumzia uchumi wa dunia, Türk amesema sekta binafsi ina jukumu muhimu katika kubadili mwelekeo wa sasa akitanabaisha kwamba, “kuna dhana potofu ya muda mrefu kwamba biashara na haki za binadamu ziko pande tofauti za mapambano. Hili si kweli.
Kuna ushahidi wa kutosha unaoonesha kwamba kampuni zinazoheshimu haki za binadamu pia hufanya vizuri zaidi kifedha.”
Türk amezihimiza serikali kujitolea upya katika ushirikiano, uwajibikaji na utawala wa sheria akisema kuwa haki za binadamu na utawala wa sheria huzuia wenye nguvu kufanya wanachotaka na kwamba mashambulizi dhidi ya haki za binadamu na taasisi za kidemokrasia hatimaye yanatishia amani na uthabiti wa dunia.
Mkurugenzi Mtendaji wa WFP Cindy McCain (katikati), akizungumza na wafanyakazi katika kambi ya wakimbizi nchini Chad.
2. “Nitaachia ngazi” WFP baada ya miezi mitatu: Cindy McCain
Kiongozi wa shirika kubwa zaidi la msaada wa chakula duniani ametangaza kujiuzulu. Bi. Cindy McCain, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP amesema atajiuzulu wadhifa wake huo baada ya miezi mitatu ili kuzingatia afya yake, akisema bado hajapona kikamilifu baada ya kupata kiharusi mwaka jana 2025.
Bi. McCain ameeleza dhamiara yake ya kuachia wadhida wake katika Shirika la WFP kwa moyo mzito kwani alirejea kazini Januari mwaka huu baada ya likizo ya matibabu kutokana na matatizo ya kiarusi yaliyompata, lakini amesema majukumu mazito ya uongozi yamekuwa yakizuia ahueni yake ya kiafya hivyo hana budi kuondoka.
Hata hivyo amesema uamuzi huo ni miongoni mwa maamuzi magumu zaidi aliyowahi kufanya katika maisha yake kwani kazi hii
“Imekuwa ya kipekee na bado itaendelea kuwa ya kipekee. Nimefanya uamuzi mgumu sana. Madaktari wangu na familia yangu wanataka nirudi nyumbani, bado sijapona kikamilifu. Nimejaribu kwa bidii kuwa na nguvu na kurudi kazini lakini ukweli ni kwamba sijapona.”
Wakati wa uongozi wake, Bi. McCain amesimamia mageuzi makubwa ya kuimarisha uwezo wa WFP kusaidia watu wanaokabiliwa na njaa katika maeneo ya migogoro na majanga ya tabianchi. Shirika hilo linatoa msaada wa chakula kwa mamilioni ya watu duniani wanaohitaji msaada.
Chini ya uongozi wake, WFP pia imeongeza ushirikiano na wadau ili kuboresha teknolojia za kidijitali katika usambazaji wa chakula. Cyndy McCain anasema imekuwa heshima kubwa kwa maisha yake kuhudumu katika shirika hili.
Na alitumai angekamilisha muda wake, lakini afya yake ndio imemuangusha hata hivyo amesisitiza kuwa
“Kitu kimoja ninachojua ni kwamba hii ni kazi yenye mahitaji makubwa sana. Na yeyote atakayechukua kazi hii lazima awe tayari kuipa si asilimia 100 tu, bali asilimia 150 kwa sababu ni kazi ngumu sana kutoipa hivyo. Hivyo, nataka kuondoka na hili. Nitawakumbuka, nakushukuru kwa urafiki wanu na nakushukuru kwa kila mnachofanya kwa WFP, nyie ni bora, asante.”
Sasa Bodi ya Utendaji ya shirika hilo la mpango wa chakula itaanza maandalizi ya uongozi wa mpito na wakati huo WFP imesema shughuli na mipango ya msaada itaendelea bila kuathiriwa.
Bi. McCain ameiongoza WFP tangu 2023, akisimamia mageuzi ya kuboresha ufanisi na kupanua wigo wa msaada wa kuokoa maisha.
Kuondoka kwake kunakuja wakati changamoto za njaa duniani zikiendelea kuongezeka, huku migogoro na mabadiliko ya tabianchi vikichochea uhaba wa chakula katika maeneo mengi duniani.
Pamoja na changamoto maafisa wa WFP wanasema shirika hilo linaendelea kujitolea kusaidia jamii zilizo hatarini huku mchakato wa kumpata kiongozi mpya ukianza.
Meja Tigist Ferede, Fundi wa magari mwanamke kutoka nchini Ethiopia anayehudumu na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Sudan Kusini, UNMISS.
3. Fundi wa magari mwanamke wa UNMISS atunukiwa nishani ya Umoja wa Taifa
Fundi wa magari mwanamke kutoka nchini Ethiopia anayehudumu na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Sudan Kusini, UNMISS, Meja Tigist Ferede ametunukiwa nishani ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, kwa kusimamia jukumu muhimu la wanawake katika operesheni za kulinda amani nje ya kushika bunduki. Tupate taarifa zaidi kutoka kwa Rashid Malekela.
Katika karakana yenye kelele za injini na migongano ya zana za kazi hapa katika kambi ya Yambio jimboni Equatoria Magharibi, mwanamke mmoja shupavu, Meja Tigist Ferede mwenye umri wa miaka 46, anabadili mtazamo wa kazi zilizotawaliwa na wanaume. Meja Ferede ni fundi mitambo wa magari (makanika) kutoka kikosi cha Ethiopia, amekuwa nguzo muhimu kwa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Sudan Kusini (UNMISS). Yeye hashiki mtutu na kusimama mstari wa mbele kwenye doria, bali anahakikisha kila gari linalotoka kambini liko imara kwa ajili ya safari ndefu na zenye hatari, kwani hitilafu ndogo ya gari inaweza kuzuia uokoaji wa raia walio hatarini.
“Nimetumikia jeshi kwa zaidi ya miaka 20. Hii ni misheni yangu ya pili katika Umoja wa Mataifa. Misheni yangu ya kwanza nilienda Sudan. Ilikuwa na changamoto kutokana na hali mbaya ya hewa na mwingiliano na jamii ya wenyeji haukuwa rahisi, lakini nilipokuja hapa kwa misheni yangu ya pili, imekuwa rahisi zaidi kwa sababu hali ya hewa ni nzuri na watu ni wakarimu. Kila gari ninalotengeneza limebeba matumaini. Yanapofika salama, najua nimetimiza wajibu wangu kwa ajili ya amani. Nawapenda watu wa hapa kwa sababu sote ni Waafrika, haswa kwa Sudan Kusini, tuna mambo mengi yanayofanana kwani ni majirani zetu.”
Ni katika gwaride maalum la kutunuku medali. Kutokana na mchango wake huo mkubwa, ametunukiwa nishani ya heshima ya Umoja wa Mataifa, hapa anaeleza furaha yake.
“Leo ni siku ya kipekee kwa sababu tumepokea nishani ya Umoja wa Mataifa kwa huduma yetu nchini Sudan Kusini, hivyo, nina furaha kwa hatua hiii. Kuvaa nishani hii kunanikumbusha kuwa hakuna jukumu dogo katika kulinda amani.”
Viongozi wa jimbo la Equatoria Magharibi wametambua mchango mkubwa wa walinda amani hao katika kuleta utulivu kwenye maeneo yenye machafuko ikiwemo Tambura. Kaimu Gavana wa jimbo hilo, Marona Joseph, amewapongeza askari hao.
“Nimetambua wazi kuwa mmechangia katika kuimarisha amani, hasa katika eneo la Tambura na maeneo mengine mliyoko. Serikali ya jimbo inapoomba msaada wenu, mmekuwa mkijibu kwa haraka sana.”
Ushirikiano huu kati ya walinda amani na serikali, umekuwa chachu ya kurejesha usalama kwa wananchi. Kamanda mkuu wa vikosi vya UNMISS, Luteni Jenerali Mohan Subramanian amesisitiza umuhimu wa kuwaheshimu walinda amani wote, raia na wanajeshi, wanaofanya kazi bila kuchoka.
“Idadi kubwa ya watu ambao wangekuwa wamefariki tangu mwaka 2021, sasa wapo hai kutokana na kazi nzuri iliyofanywa kikosi cha Ethiopia. Hadi sasa, askari 142 wa Ethiopia wamepoteza maisha yao wakitumikia bendera ya Umoja wa Mataifa, na tunapaswa kukumbuka kujitolea kwao.”
Jenerali huyo amewakumbuka pia askari tisa waliofariki wakiwa kazini ndani ya misheni ya UNMISS.
Uwepo wa Meja Ferede na wote wanaohakikisha “magurudumu ya magari ya amani” yanazunguka nchini Sudan Kusini, unatoa faraja, msaada, na matumaini kwa jamii zilizokumbwa na vita. Meja Ferede amethibitisha kuwa amani haijengwi tu kwa bunduki, bali pia kwa spana na injini zinazofanikisha huduma zinawafikia walio na uhitaji.