
Dodoma. Mbunge wa Makete na Mwenyekiti wa Bunge Bonanza, Festo Sanga, amewataka wananchi kujumuika na wabunge wao kushiriki Bunge Marathon itakayofanyika Julai 18, 2026 katika Viwanja vya Jamhuri jijini Dodoma, kwa lengo la kuhamasisha uchangiaji wa damu salama na kuimarisha afya.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Sanga amesema mbio hizo za msimu wa tatu zitahusisha kilometa 5, 10 na 21, zikitarajiwa kushirikisha wananchi, wabunge na wanariadha wa ndani na nje ya Tanzania.
Amesema kaulimbiu ya mwaka huu, “Njoo Ukimbie na Mbunge Wako,” inalenga kuimarisha afya za wananchi na kuimarisha uhusiano kati ya wabunge na jamii wanayoitumikia.
“Wanariadha kutoka Kenya na Uganda walishiriki msimu uliopita, na mwaka huu tunatarajia pia washiriki kutoka Ethiopia, hatua itakayoongeza ushindani na ubora wa mbio hizi,” amesema Sanga.
Ameongeza kuwa Bunge Marathon ni sehemu ya kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhimiza wananchi kushiriki michezo na mazoezi ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.
Kwa mujibu wa Sanga, msimu huu umeandaliwa zawadi kubwa zaidi kuwahi kutolewa katika mbio hizo. Alisema mshindi wa kwanza wa kilometa 5 atapata Sh5 milioni, wa pili Sh2 milioni na wa tatu Sh1 milioni.
Kwa upande wa kilometa 10, mshindi wa kwanza atazawadiwa Sh3 milioni, wa pili Sh2 milioni na wa tatu Sh1 milioni, huku mbio za kilometa 21 mshindi wa kwanza akijinyakulia Sh6 milioni, wa pili Sh3 milioni na wa tatu Sh1.5 milioni.
Sanga amesema zawadi hizo zinatolewa chini ya usimamizi wa Spika wa Bunge, Idd Zungu, na kwamba lengo ni kuvutia ushindani na kuongeza hadhi ya mashindano hayo nchini.
Amesema mbali na mashindano, washiriki wote watapata fursa ya kuchangia damu salama kupitia vituo vitakavyowekwa uwanjani, wakilenga kuvunja rekodi ya washiriki 5,200 waliokimbia mwaka jana.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Silent Ocean, Mohamed Soloka, ambao ni wadhamini wa mbio hizo, amesema kampuni hiyo imeunga mkono tukio hilo kwa kuwa linaunganisha michezo, afya na jamii.
“Rais amekuwa chachu kubwa katika kuhamasisha michezo na mazoezi nchini, hivyo nasi tumeona umuhimu wa kuunga mkono jitihada hizi. Bunge ni nguzo muhimu ya taifa, hivyo kushirikiana nalo kunatusaidia pia kufikisha ujumbe kwa Watanzania,” amesema Soloka.
Ametoa wito kwa wadau wa michezo na wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki Bunge Marathon ili kuimarisha afya na kuchangia damu salama.