Kwimba. Watumishi wote wa idara ya afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza wamepatiwa mafunzo ya matumizi sahihi na salama ya gesi ya kupikia, sambamba na kuelimishwa madhara ya kiafya yanayotokana na matumizi ya kuni na mkaa.
Mafunzo hayo yametolewa na Kampuni ya Oryx Gas Tanzania yakilenga kuwawezesha watumishi hao kuwa na uelewa mpana kuhusu nishati safi ya kupikia na kuwa mabalozi wa matumizi yake kwa wananchi wanaowahudumia, wakiwemo wagonjwa.
Akizungumza Februari 27, 2026 wakati wa utolewaji wa mafunzo hayo wilayani Kwimba, Mkuu wa Mafunzo wa Oryx Gas Tanzania, Peter Ndomba amesema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za kampuni hiyo kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.
Amesema kundi la watumishi wa afya limechaguliwa kwa kuwa ndilo hukutana moja kwa moja na wananchi wanaopata matatizo ya kiafya yanayohusishwa na matumizi ya nishati isiyo safi.
“Oryx Gas tumeamua kutoa mafunzo haya kwa watumishi wa afya wa Wilaya ya Kwimba kwa sababu wananchi wanapopata matatizo ya kiafya huenda hospitali, hivyo watumishi hawa ndio hukutana nao kwanza. Tumewapa mafunzo ya kina kuhusu matumizi sahihi na salama ya gesi, pamoja na athari za kimazingira na kiafya za kuni na mkaa,” amesema Ndomba.
Amesema zaidi ya watumishi 267 wa sekta ya afya, wakiwemo wa Hospitali ya Wilaya ya Kwimba, walishiriki mafunzo hayo ya siku mbili kuhusu nishati safi ya kupikia.
Ndomba amesema mwitikio wa mafunzo hayo umekuwa mkubwa na ni mwanzo wa mpango wa kampuni hiyo kufikia taasisi mbalimbali, zikiwemo shule na majukwaa ya kijamii ili kuhamasisha matumizi ya nishati safi kwa jamii pana.
Aidha, ameushukuru uongozi wa Hospitali ya Wilaya ya Kwimba, Ofisa Mganga Mkuu wa Wilaya (DMO) na Mganga Mfawidhi kwa kutoa fursa ya kukutana na madaktari na wauguzi na kuwapatia elimu hiyo.
Amesema kuna haja ya watumishi hao kuifikisha elimu hiyo kwa wananchi, hasa wanawake wanaofika hospitalini wakiwa na matatizo ya kiafya yanayohusishwa na matumizi ya kuni na mkaa.
Kwa upande wao, watumishi wa afya wilayani humo waliishukuru Oryx Gas kwa mafunzo hayo, wakisema yamewajengea uelewa sahihi wa matumizi ya gesi na kuwawezesha kuwa mabalozi wa nishati safi katika jamii.
Muuguzi Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kwimba, Christian Mvula amesema mafunzo hayo yamewasaidia kuelewa matumizi salama ya gesi na umuhimu wa kuachana na kuni na mkaa.
“Tumepata elimu sahihi ya kutumia gesi kama nishati ya kupikia majumbani. Awali tulikuwa na uelewa tofauti na kulikuwa na nadharia nyingi kuhusu usalama na gharama za gesi. Sasa tumeelimishwa jinsi ya kuitunza na kuikagua ili kuepusha madhara, pamoja na madhara ya kuni na mkaa,” amesema Mvula.
Ofisa Muuguzi Salome Malale amesema licha ya kutumia gesi kwa zaidi ya miaka 15, hakuwa na uelewa wa kina kuhusu faida na changamoto zake.
Amesema jamii nyingi zinazotumia kuni na mkaa hukumbwa na matatizo ya kiafya, yakiwemo ya mapafu na macho, hali inayosababisha wagonjwa wengi kufika hospitalini.
“Elimu niliyoipata itanisaidia kutoa uhamasishaji kwa jamii kutumia gesi na kuachana na kuni na mkaa,” amesema Malale.
Mtumishi wa Hospitali ya Wilaya ya Kwimba, Robert Mayombya amesema mafunzo hayo yamemwezesha kuelewa vizuri matumizi ya nishati safi ya kupikia.
“Nimejifunza kutumia gesi badala ya kuni na mkaa. Nitaanza kutoa elimu kwa familia yangu na majirani ili waachane na kuni na mkaa na kutumia gesi,” amesema Mayombya.