Akihutubia mkutano maalum wa Bodi ya IAEA leo katika mji mkuu wa Austria, Vienna, Bwana Grossi, amebainisha kuwa hadi kufikia sasa hakuna dalili za kuharibiwa kwa mitambo yoyote ya nyuklia ya Iran, ikiwemo Kituo cha Nishati ya Nyuklia cha Bushehr, Kinu cha Utafiti cha Tehran na vituo vingine vya mzunguko wa mafuta ya nyuklia lakini akasisitiza akisema hebu nikumbushe tena maazimio ya awali ya Mkutano Mkuu yanayosema kwamba mashambulizi ya silaha dhidi ya vituo vya nyuklia hayapaswi kamwe kufanyika na yanaweza kusababisha kuachiliwa kwa mionzi yenye madhara makubwa ndani na nje ya mipaka ya nchi iliyoshambuliwa.

Wakati huo huo katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva,Uswisi leo nchi za Ghuba zilizoathiriwa na mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Iran yaliyohusisha makombora  na ndege zisizo na rubani zimelaani mashambulizi dhidi ya mamlaka yao na kuhimiza Iran kusitisha “ongezeko lolote la uhasama” linaloweza kuhatarisha uthabiti wa kikanda.

Nalo Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani limesema, kuna dalili kwamba raia 550 wameuawa nchini Iran tangu nchi hiyo iliposhambuliwa Jumamosi. Maeneo yaliyolengwa ni pamoja na Hospitali ya Gandhi ya Tehran ambayo ilipata uharibifu jana Jumapili.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus ameandika katika mitandao ya kijamii akisema, “hii inakumbusha kwamba juhudi zote lazima zichukuliwe ili kuzuia vituo vya afya visihusishwe katika mzozo unaoendelea. Vituo vya afya vinalindwa chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu,”

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR nalo limeeleza wasiwasi  mkubwa kuhusu kuongezeka kwa mapigano katika eneo la Mashariki ya Kati, likionya kuwa hali hiyo inaweza kuwa na madhara makubwa kwa raia na kusababisha wimbi jipya la watu kulazimika kuyahama makazi yao katika eneo ambalo tayari linakabiliwa na changamoto kubwa.

Katika taarifa iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi, UNHCR imesema kuwa nchi nyingi zilizoathiriwa tayari zinahifadhi mamilioni ya wakimbizi na watu waliokimbia makazi yao ndani ya nchi zao.

Tangu kuanza kwa mashambulizi ya Marekani na washirika wake dhidi ya Iran, Umoja wa Mataifa umeendelea kuifuatilia hali kwa ukaribu na kuhimiza diplomasia badala ya misuli. Katika kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Jumamosi, tarehe 28 Februari, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres aliwaambia wajumbe hakuna mbadala wa mazungumzo kwenye hiki kinachoendelea sasa cha mashambulizi ya kijeshi yanayofanywa na  Marekani, Israel na Iran. “Hali ya sasa inaleta tishio kubwa kwa amani na usalama wa kimataifa.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *