Waziri wa Mambo ya Nje wa China amesisitizia ulazima wa faili la nyuklia la Iran kuondolewa kwenye wingu la vita.

Wang Yi ametoa sisitizo hilo katika mazungumzo aliyofanya kwa njia ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Jean-Noel Barrot na kueleza kwamba, jamii ya kimataifa inapaswa ipinge hatua yoyote ya ukiukaji wa sheria za kimataifa na kujiepusha na utumiaji wa vipimo vya upendeleo na undumakuwili.

Wang ameongeza kuwa, madola makubwa yenye nguvu yasitumie kuwa kwao na uwezo wa juu wa kijeshi kuanzisha mashambulio dhidi ya nchi zingine; na dunia isirudishwe kwenye “Sheria ya Msituni”.

Waziri wa Mambo ya Nje wa China amekumbusha kuwa, hatimaye baada ya yote, italazimu kuirejesha kadhia ya nyuklia ya Iran kwenye mkondo wa kisiasa na kidiplomasia na akasema, anatumai kwamba, kwa kufuata muelekeo wa insafu na wa kuzingatia uhalisia, Ufaransa itaungana na kushirikiana na China katika kuielekeza hali ya mambo upande wa kupunguza mivutano na kulinda misingi mikuu ya uhusiano wa kimataifa.

Katika mazungumzo hayo, Jean-Noel Barrot amebainisha mtazamo wa Ufaransa kuhusu hali ya hivi sasa ya Asia Magharibi na akasisitiza kwamba, katika mazingira yaliyopo inapasa pande zote zifanye jitihada za kupunguza mivutano na kutatua suala la nyuklia la Iran na tofauti nyinginezo kwa njia ya mazungumzo…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *