Moshi. Kaya 14 zenye jumla ya watu 39 katika Mtaa wa Viwanda, Kata ya Njoro, Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro zimekosa makazi baada ya nyumba zao kuzingirwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha kwa zaidi ya saa sita usiku wa kuamkia Machi 2, 2026.

Mbali na kupoteza makazi, familia hizo zinakabiliwa na uhaba wa chakula baada ya vyakula na mali zao kuharibiwa na maji. Waathirika wameiomba Serikali kuwapatia msaada wa dharura wa malazi, chakula na mahitaji mengine ya kibinadamu.

Baadhi ya wakazi waliozungumza Machi 3, 2026 wamesema mafuriko yameharibu magodoro, vitanda, nguo na vifaa vya shule vya watoto. Zuhura Mhezi amesema watoto wake wameshindwa kwenda shule baada ya sare na madaftari kusombwa na maji. “Sina chochote kilichobaki, watoto hawajaenda shule kwa sababu hawana vifaa,” amesema.

Mkazi mwingine, Asha Arubai, amesema eneo hilo hukumbwa na mafuriko kila mwaka kutokana na maji yanayotiririka kutoka maeneo ya juu. Ameeleza kuwa usiku wa tukio hawakulala kutokana na hofu, huku akiiomba Serikali kutatua tatizo hilo la muda mrefu. Naye Hussein Mohamed amesema familia yake wamehifadhiwa kwa jirani baada ya kushindwa kuokoa chochote.

Mjumbe wa serikali ya mtaa, William Kavishe, amesema nyumba kadhaa zimeathirika, baadhi ya kuta zimeanguka na kaya 14 hazina makazi. Diwani wa Njoro, Zuberi Kidumo, amesema tayari eskaveta imepelekwa kufungua njia zilizozibwa na maji ili kupunguza athari.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, amesema waathirika wengi wanaishi mabondeni na ndani ya mita 60 kutoka Mto Njoro. Ametaja maeneo hatarishi kuwa ni Pasua, Njoro, Mabogini, Majengo, Msaranga na Ng’ambo, na kuwataka wakazi wa mabondeni kuondoka mapema ili kuepusha madhara zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *