Morogoro. Wakati sekta ya sanaa na ubunifu ikiendelea kukua kwa kasi na kutoa ajira kwa maelfu ya vijana nchini, wadau wameonya kuwa bila kuhakikisha uwepo wa kazi zenye staha, mchango wake katika kukuza uchumi wa Taifa unaweza kubaki kwenye takwimu zisizogusa maisha halisi ya wasanii.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Taasisi ya Sedeva, Izack Abeneko katika warsha ya siku tatu ya usambazaji wa matokeo ya utafiti kuhusu kuendeleza kazi zenye staha katika sekta ya utamaduni na uchumi wa ubunifu nchini Tanzania, iliyoandaliwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO).

“Mazingira ya kazi ya wasanii wengi bado siyo rasmi, ni ya ‘ndondo’. Msanii akipata kazi leo hawezi kujua ni lini atapata kazi nyingine. Serikali itengeneze mfumo utakaosaidia sheria zilizopo zitekelezwe kwa ufanisi na kuleta matokeo chanya kwa wadau wote wa sanaa,” amesema Abeneko.

Wadau walioshiriki warsha ya siku tatu ya usambazaji wa matokeo ya utafiti kuhusu kuendeleza kazi zenye staha katika sekta ya utamaduni na uchumi wa ubunifu nchini leo Jumatatu, Machi 3, 2026 mkoani Morogoro.

Utafiti huo umebainisha kuwa licha ya sekta ya utamaduni na ubunifu kuwa na mchango unaoongezeka katika pato la Taifa na ajira kwa vijana, ukuaji huo haujaambatana na ulinzi wa kijamii, mikataba rasmi wala mazingira salama ya kazi kwa wasanii wengi.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti na Masoko wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Mrisho Mrisho amesema warsha hiyo imeibua maeneo matatu muhimu yanayohitaji kupewa kipaumbele.

“Kwanza ni kazi zenye staha katika sekta ya sanaa, pili mfumo wa kisheria na sera, na tatu ni mapato ya wasanii. Tunahitaji kuona namna ya kurasimisha sekta yetu katika maeneo haya matatu ili wasanii waishi katika mazingira rasmi yanayowatambua,” amesema.

Ameongeza kuwa pamoja na usajili wa wasanii kupitia BASATA, bado kuna haja ya mifumo mingine ya ajira na ulinzi wa kijamii kuwatambua wasanii kama wafanyakazi halali.

Naye Mkurugenzi wa Afya na Usalama Mahali pa Kazi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Dk Kassim Kapalata amesisitiza umuhimu wa wasanii kujiunga na vyama vya wafanyakazi ili kulinda maslahi yao.

“Wasanii wanapaswa kujiunga katika mashirikisho ya vyama vya wafanyakazi ili waweze kutambulika kisheria. Wakiwa pamoja itawasaidia haki zao kutambuliwa kwa mujibu wa sheria na kurahisisha kufikiwa kwa dhana ya kazi zenye staha katika sekta ya sanaa,” amesema.

Wadau walioshiriki warsha ya siku tatu ya usambazaji wa matokeo ya utafiti kuhusu kuendeleza kazi zenye staha katika sekta ya utamaduni na uchumi wa ubunifu nchini leo Jumatatu, Machi 3, 2026 mkoani Morogoro.

Wadau hao wameitaka Serikali na taasisi husika kutumia matokeo ya utafiti huo kuweka mikakati itakayosaidia kurasimisha sekta ya utamaduni na ubunifu, ili ukuaji wake uwe na manufaa ya moja kwa moja kwa wasanii na uchumi wa Taifa kwa ujumla.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *