Arusha. Serikali imesema inaendelea kukamilisha maandalizi ya Mkakati wa Kitaifa wa Kukabiliana na Wanyamapori Wakali na Waharibifu (2025/26–2034/35) pamoja na kufanya tafiti za kimkakati ili kubuni mbinu mpya za kukabiliana na wanyamapori hao, hususan tembo.

Aidha, imeielekeza Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (Tawiri) kuendelea kuwafunga mikanda ya mawasiliano tembo viongozi ili kubaini mienendo yao na kuwadhibiti kabla ya kusababisha madhara kwa wananchi. Hatua hiyo itawezesha pia matumizi ya ndege nyuki (drone) kuchukua hatua za haraka kupunguza madhara kwa jamii.

Maagizo hayo yametolewa leo Jumanne, Machi 3, 2026, na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Ashatu Kijaji, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanyamapori Duniani kitaifa yaliyofanyika viwanja vya Nanenane, Njiro, mkoani Arusha.

Amesema wanyamapori ni rasilimali muhimu katika uchumi wa Taifa kupitia sekta ya utalii, inayochangia zaidi ya asilimia 25 ya fedha za kigeni na asilimia 17.1 katika pato la Taifa. Hata hivyo, sekta hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo migongano kati ya binadamu na wanyamapori wakali na waharibifu, hali inayoongeza mahusiano hasi na kusababisha kuzibwa kwa shoroba za wanyamapori kutokana na ongezeko la makazi bila mipango bora ya matumizi ya ardhi.

Changamoto nyingine ni kupungua kwa makazi ya wanyamapori kutokana na uvamizi wa maeneo ya hifadhi kwa ajili ya kilimo, ufugaji na uchimbaji madini, jambo linalopunguza maeneo ya malisho na mazalia. Pia zipo changamoto za ujangili na biashara haramu ya nyara na mazao ya misitu, ongezeko la mimea vamizi katika hifadhi na nyanda za malisho, pamoja na mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha ukame au mvua nyingi kupita kiasi, hali inayoathiri makazi ya wanyamapori, upatikanaji wa maji na miundombinu ndani ya hifadhi.

Waziri amesema kutokana na changamoto hizo, Serikali itaendelea kufunga mikanda ya mawasiliano kwa tembo viongozi. “Niwaelekeze Tawiri kukamilisha hatua ya kufunga mikanda katika Pori la Akiba Mkungunero. Mikanda hiyo itatuwezesha kupata taarifa kwa wakati na kuchukua hatua za haraka kwa kutumia drone, ili kupunguza madhara kwa wananchi,” amesema.

Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kufanya tafiti za kimkakati kubuni mbinu mpya za kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu, hususan tembo, pamoja na kutekeleza mkakati wa kupambana na ujangili ili kuhakikisha ujangili wa nyara na kitoweo unatokomezwa ifikapo mwaka 2033.

Amesema Tanzania inaendelea kuwa miongoni mwa nchi zenye idadi kubwa ya wanyamapori na imetenga zaidi ya theluthi ya ardhi yake kwa uhifadhi. Mtandao wa maeneo ya hifadhi unajumuisha Hifadhi za Taifa 21, Mapori ya Akiba 29, Mapori Tengefu 25, Maeneo ya Ardhioevu manne na Maeneo 40 ya Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori (WMA). Tanzania pia inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya simba, chui na nyati, na ni ya tatu kwa tembo duniani.

Waziri alisema idadi ya watalii imeongezeka kutoka milioni 5.36 mwaka 2024 hadi milioni 5.93 mwaka 2025, sawa na ongezeko la asilimia 10.73. Mapato ya utalii yameongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 3.9 hadi bilioni 4.4, sawa na ongezeko la asilimia 12.82.

Akizungumzia maadhimisho hayo, amesema yanakumbusha mchango wa mimea dawa na manukato katika afya ya binadamu, uchumi wa jamii na uhai wa mifumo ya ikolojia. Amesema mimea hiyo ina mchango mkubwa katika tiba asili, lishe, utamaduni na maendeleo endelevu.

Awali, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Nkoba Mabula, alisema maadhimisho hayo yalianza rasmi nchini mwaka 2014, na kaulimbiu ya mwaka huu inasisitiza kuwa afya ya binadamu, uchumi wa jamii na uhai wa ikolojia haviwezi kutenganishwa. Amesisitiza kuwa kuhifadhi mimea dawa ni kulinda afya ya sasa na ya vizazi vijavyo.

Ameeleza kuwa wizara kwa kushirikiana na wadau itaendelea kuimarisha uhifadhi wa misitu na maeneo ya hifadhi, kuhimiza tafiti za kisayansi kwa kushirikiana na vyuo na taasisi nyingine, kuendeleza usimamizi shirikishi wa misitu ili jamii zinufaike moja kwa moja, kudhibiti uvunaji holela wa spishi adimu kupitia vibali na ufuatiliaji, pamoja na kukuza upandaji miti kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *