Dar es Salaam. Kampuni ya Tanzania Securities Limited (TSL) imezindua mipango miwili mipya ya uwekezaji wa pamoja yenye ubunifu, ikilenga kuimarisha ushirikishwaji wa wananchi katika sekta ya kifedha na kupanua wigo wa fursa za uwekezaji nchini.

Akizungumza Machi 3, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa bidhaa hizo, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, aliyewakilishwa na Emmanuel Akaro, alitaja mifuko iliyozinduliwa kuwa ni Mfuko wa Imara na Mfuko wa KeshoTulivu.

Amesema mifuko hiyo inatoa fursa zenye utaratibu maalumu kwa wananchi kushiriki katika masoko ya mitaji kwa njia iliyo rahisi na yenye usimamizi wa kitaalamu.

Ametoa wito kwa Watanzania kujenga utamaduni wa kuweka akiba na kuwekeza kwa uwajibikaji, akibainisha kuwa hatua hiyo itaimarisha ustahimilivu wao wa kifedha, kukuza masoko ya mitaji na kuharakisha maendeleo endelevu ya uchumi.

“Ujuzi wa kifedha ndio msingi wa ustawi wa mtu binafsi na Taifa. Watu binafsi wanapoelewa namna ya kuweka akiba, kuwekeza na kudhibiti vihatarishi, wanakuwa katika nafasi nzuri ya kulinda maisha yao ya baadaye na kuchangia katika ukuaji wa uchumi. Taifa linalowekeza kwa busara hujenga utajiri si kwa ajili ya leo tu, bali kwa vizazi vijavyo,” amesema.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa TSL, George Shumbusho, amesema mifuko hiyo miwili ina muundo tofauti lakini imeunganishwa na lengo la kuwawezesha Watanzania kukuza, kulinda na kupanga utajiri wao kwa kujiamini.

Akifafanua, amesema Mfuko wa Imara ni mpango wa wazi uliobuniwa kutoa ukwasi wa juu na kupunguza vihatarishi, hivyo kufaa kwa wawekezaji wanaotafuta ukuaji wa mtaji wa muda mfupi kupitia mseto wa hati za madeni.

Ameongeza kuwa mfuko huo unawalenga wawekezaji wanaohitaji ukuaji wa mtaji huku wakitaka uwezekano wa kupata fedha zao kwa haraka, pamoja na kunufaika na usimamizi wa kitaalamu na udhibiti madhubuti wa vihatarishi.

Kuhusu Mfuko wa Kesho Tulivu, Shumbusho amesema ni mfuko wa wazi wenye uwiano ulioundwa kusaidia Watanzania kujenga uwekezaji wa muda mrefu kwa ajili ya kustaafu.

Amesema mfuko huo unatoa chaguo la uwekezaji wa miaka mitano, 10 au 15 na kuendelea, ukiwa na faida shindani za muda mrefu pamoja na njia rahisi za kuchangia, ikiwamo makato ya kiotomatiki kutoka kwenye mshahara.

Kupitia mfuko huo, wawekezaji wana uhuru wa kuchagua namna na wakati wa kupokea faida zao ama kila mwezi, robo mwaka, mwaka au kwa mfumo wa mchanganyiko kulingana na malengo yao ya kustaafu na mahitaji ya kifedha.

Naye mwakilishi wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Alfred Mkombo ameipongeza TSL kwa hatua hiyo, akisisitiza dhamira ya mamlaka hiyo katika kukuza soko la mitaji lililo thabiti, shirikishi na endelevu.

“Kuanzishwa kwa mipango ya uwekezaji wa pamoja kunaonyesha jinsi ubunifu unavyoweza kupanua ufikiaji wa fursa za uwekezaji huku ukidumisha ulinzi stahiki kwa wawekezaji,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *