
Mamia ya wanaharakati wanaopinga vita wamefanya maandamano makubwa huko Manhattan mjini New York wakilaani mashambulizi ya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Wapinzani hao wa vita na sera za Donald Trump walianza maandamano yao jioni ya jana katika Medani ya Columbus wakitangaza upinzani wao dhidi ya uchokozi na mashambulizi ya kijeshi ya Marekani na Israel nchini Iran.
Waandamanaji walikuwa wakipiga nara za “simamisha vita dhidi ya Iran”.
Baadhi ya waandamanaji hao walikuwa wamebeba picha za Kiongozi Shahidi Ayatullah Ali Khamenei huku wakipiga nara za “Anzisheni Intifadha ya Kimataifa”. Waandamanaji hao pia wamelaani siasa za kinafiki za nchi za Magharibi.
Maandamano kama hayo ya kupinga vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran pia yamefanyika katika maeneo na miji mbalimbali ya Marekani, nchi za Ulaya na barani Asia.
Waandamanaji wameeleza kuchukizwa kwao na sera za kibabe na uchokozi wa madola hayo mawili wakisema Iran ina haki ya kujibu uchokozi huo kwa mujibu wa sheria za kimataifa.