Washington, Marekani. Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema hana wasiwasi wowote iwapo Iran itaamua kujiondoa katika Kombe la Dunia la 2026, wakati mvutano wa kijeshi kati ya Marekani, Israel na Iran ukiendelea kushika kasi.

Akizungumzia suala hilo, Trump amesema, “Sijali kabisa. Nafikiri Iran ni nchi iliyoshindwa vibaya. Wanaendelea kwa shida.”

Kauli hiyo inakuja wakati Iran, ambayo imefuzu kushiriki Kombe la Dunia kwa mara ya nne mfululizo, ikitafakari uwezekano wa kususia mashindano hayo yatakayofanyika Marekani, Canada na Mexico.

Baadhi ya mashabiki wa timu ya taifa ya Iran, walipokuwa wakiishangilia timu yao. Picha na Mtandao

Iraq au UAE kuchukua nafasi?

Iwapo Iran itajiondoa, Iraq na Falme za Kiarabu (UAE) ndizo nchi zinazopewa nafasi kubwa ya kuchukua nafasi hiyo.

Iraq inaweza kufuzu iwapo itashinda mchujo wa mabara dhidi ya Bolivia au Suriname utakaopigwa Monterrey, Mexico. Endapo Iraq itafuzu moja kwa moja, UAE inaweza kuwa mrithi wa nafasi ya Iran kama timu inayofuata kwa viwango barani Asia.

Kwa mujibu wa kanuni za Kombe la Dunia 2026, iwapo nchi itajiondoa kutokana na sababu za dharura, FIFA ina mamlaka kamili ya kuamua hatua itakayochukuliwa, ikiwemo kuipa nafasi hiyo nchi nyingine.

Katibu Mkuu wa FIFA, Mattias Grafstrom, amesema suala hilo limejadiliwa lakini ni mapema kutoa maamuzi rasmi.

“Lengo letu ni kuhakikisha Kombe la Dunia linakuwa salama na kila timu inashiriki,” amesema.

Rais wa Marekani, Donald Trump (kushoto) mwingine ni rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Gianni Infantino. Picha na Mtandao

Hofu ya usalama 

Rais wa Shirikisho la Soka la Iran, Mehdi Taj, amesema ni vigumu kwa sasa kutazama mashindano hayo kwa matumaini kutokana na hali ya usalama.

Wakati huo huo, mapigano yameendelea kwa siku kadhaa, huku mashambulizi yakiripotiwa katika maeneo mbalimbali ya Mashariki ya Kati. Bei za nishati duniani zimeanza kupanda, huku mataifa yakihaha kuwaokoa raia wao waliokwama katika ukanda huo.

Trump anaamini vita hivyo vinaweza kudumu takribani wiki nne au chini ya hapo.

“Imekuwa mchakato wa wiki nne. Inaweza kuwa wiki nne au hata chini,” amesema.

Moja ya sehemu mashambulizi yanayoripotiwa kuendelea katika maeneo mbalimbali ya Mashariki ya Kati. Picha na Mtandao

Siku zinahesabika

Zikiwa zimesalia chini ya siku 100 kabla ya kuanza kwa Kombe la Dunia la kwanza lenye timu 48, sintofahamu juu ya ushiriki wa Iran inaendelea kuibua maswali.

Iwapo Iran itaamua kujiondoa rasmi, FIFA italazimika kufanya uamuzi wa haraka ili kuhakikisha ratiba ya mashindano haivurugiki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *