Hili ni jukwaa kubwa zaidi la kila mwaka la Umoja wa Mataifa linalojikita katika usawa wa kijinsia na haki za wanawake. Kinachotokea katika CSW huwa na mchango kwenye sheria, sera, ufadhili na uwajibikaji katika nchi mbalimbali na kwa vizazi tofauti.
Kinachomulikwa mwaka huu ni: Haki, Sheria na Hatua kwa Wanawake na Wasichana wote, ikienda sambamba na kauli mbiu ya mwaka huu ya siku ya wanawake duniani Machi 8.
Dunia inapaswa kuchagua ‘tamu’ au ‘chungu’
CSW70 inafanyika wakati muhimu: dunia inatakiwa kuchagua kuchukua hatua kwa pamoja na kuhakikisha usawa mbele ya sheria kwa wanawake na wasichana wote, au iruhusu dhuluma iendelee bila watekelezaji kuwajibishwa.
Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na Masuala ya Wanawake, UN Women linaziomba serikali, washirika, taasisi na jamii kote duniani kusimama kidete, kujitokeza na kuzungumza kwa ajili ya haki, sheria na hatua – ili wanawake na wasichana kote duniani waweze kuishi kwa usalama, na wazungumze kwa uhuru katika mazingira yenye usawa.
Mwanamke aliyekimbia makazi yake akiishi katika kambi ya wakimbizi wa ndani huko Kalemi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Fahamu kwa muhtasari kitakachojiri: Jumla ya mikutano 15 kufanyika
Jumla ya mikutano 15 inatarajiwa kufanyika wakati wa jukwaa hili la wanawake ambapo baadhi itaanza kabla ya tarehe 9 Machi 2026.
1. Mkutano na waandishi wa habari – Uzinduzi wa Kimataifa wa Ripoti ya Katibu Mkuu. (4 Machi 2026)
Mkutano huu umewasilisha ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa inayoonya kuwa mifumo ya sheria inazidi kushindwa kulinda wanawake na wasichana, na kuwaacha katika hatari ya unyanyasaji na ubaguzi.
2. Jukwaa la Vijana: (Sauti bila Mipaka) (4 Machi 2026)
Mkutano unaoongozwa na vijana ukileta pamoja wanaharakati vijana 200 kujadili majawabu ya kukabiliana na ukosefu wa haki wa kimfumo na kuhamasisha mageuzi ya kuhakikisha haki sawa kwa wanawake na wasichana.
3. Maadhimisho ya Umoja wa Mataifa ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake (9 Machi) (Saa 3 hadi saa 4 asubuhi)
Tukio la kimataifa litakaloangazia kaulimbiu “Haki. Uadilifu. Hatua kwa Wanawake na Wasichana Wote”, likiwaleta pamoja viongozi na watetezi wa haki ili kuhimiza upatikanaji sawa wa haki.
4. Ufunguzi wa CSW70 (9 Machi) Saa 4 asubuhi
Ufunguzi rasmi wa mkutano mkubwa zaidi wa kila mwaka wa Umoja wa Mataifa kuhusu usawa wa kijinsia, ukiwa na hotuba za viongozi wa dunia na kuanza kwa majadiliano kuhusu haki kwa wanawake na wasichana.
5. Mkutano wa Mawaziri wa G77 na washirika wanaoibuka (9 Machi)
Mawaziri na viongozi wa kifedha watajadili njia za kuongeza ufadhili endelevu kwa ajili ya usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa kiuchumi kwa wanawake.
6. Maadhimisho ya Miaka 45 ya CEDAW (9 Machi)
Hafla ya kumbukumbu ya miaka 45 ya Mkatab awa Kimataifa wa Kutokomeza Aina Zote za Ubaguzi dhidi ya wanawke (CEDAW), mkataba muhimu wa kimataifa unaoendeleza haki za wanawake na usawa wa kisheria duniani.
7. Kufikia Usawa wa Kijinsia katika Sheria za Uraia (10 Machi)
Tukio la ngazi ya juu litakalojadili sheria za uraia zenye ubaguzi wa kijinsia na kuzindua ramani ya kisheria ya kimataifa inayoonyesha mapengo hayo.
8. Mkutano wa wazi na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na asasi za kiraia (10 Machi)
Wawakilishi wa asasi za kiraia watapata nafasi ya kuzungumza moja kwa moja na Katibu Mkuu kuhusu changamoto na suluhisho za usawa wa kijinsia duniani.
9. Mjadala wa Mawaziri kuhusu wanawake wazee (11 Machi)
Mawaziri watajadili sera za kuimarisha usalama wa kiuchumi, haki na ulinzi wa wanawake wazee wakati idadi ya watu wanaozeeka inaongezeka duniani.
10. Mabunge na usawa wa kijinsia katika maamuzi (11 Machi)
Wabunge kutoka nchi mbalimbali watashirikiana kuhusu mikakati ya kuongeza uwakilishi wa wanawake na kuboresha mifumo ya haki inayozingatia usawa wa kijinsia.
Mwanaharakati wa wanawake kuhusu Ukeketaji au FGM anazungumza katika hafla ya elimu kwa jamii huko Tana River, Kenya.
11. Kuendeleza upatikanaji wa haki kwa wanawake (11 Machi)
Serikali na asasi za kiraia zitaangazia mageuzi na ubunifu unaofanya mifumo ya haki kuwa jumuishi zaidi, hasa katika maeneo yenye migogoro au changamoto.
12. Wanawake viongozi wakiongoza njia (11 Machi)
Viongozi wanawake watajadili jinsi uongozi jumuishi na utawala bora vinavyoweza kuimarisha mifumo ya haki kwa wanawake na wasichana.
13. Mkutano wa ngazi ya juu kuhusu ukatili dhidi ya wanawake na wasichana (12 Machi)
Mawaziri na wataalamu watajadili njia za kuzuia ukatili na kuimarisha msaada kwa manusura duniani.
14. Mazungumzo shirikishi na wawakilishi wa vijana (16 Machi)
Viongozi vijana watashiriki uzoefu na mawazo ya kuondoa vikwazo vya kisheria na kupanua upatikanaji wa haki kwa wanawake na wasichana.
15. Kufungwa kwa CSW70 (Machi 19 )
Kikao kitahitimishwa kwa wajumbe kupitisha makubaliano ya pamoja na kupitia hatua za kuendeleza usawa wa kijinsia.
Tanzania Women Ecocomic Empowerment Network” TAWEN, wasema mwanamke anapowezeshwa jamii nzima inanufaika.
Kuhusu Kamisheni ya Hali ya Wanawake (CSW) |
| CSW ni Kamisheni ya kiutendaji ya Baraza la Umoja wa Mataifa la Kiuchumi na Kijamii (ECOSOC) na ndicho chombo kikubwa zaidi duniani cha kutunga sera kinachojikita pekee katika kukuza usawa wa kijinsia, haki, na uwezeshaji wa wanawake na wasichana. UN Women, ambayo ni Sekretarieti, inaunga mkono vipengele vyote muhimu vya kazi ya Kamisheni hii. |