Wataalamu kutoka kote duniani wameelezea wasiwasi wa aina mbalimbali kuhusu jinsi AI inavyoathiri ajira na kuwasilisha mbinu mpya za kutumia teknolojia hizi kwa namna inayolinda haki na kukuza ustawi katika mtandao wa hivi karibuni ulioandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kazi Duniani ILO na Muungano wa Kimataifa wa Mawasiliano ITU.
“Suala kuu si kama AI itabadilisha kazi tayari inafanya hivyo,” amesema Sher Verick, mratibu wa ILO wa masuala ya kidijitali na AI. “Suala la msingi ni jinsi ya kuhakikisha kwamba mabadiliko haya yanaendeleza kazi zenye staha na haki ya kijamii.”
Katika mkutano wa kwanza wa Jopo Huru la Kimataifa la Kisayansi kuhusu AI uliofanyika Jumanne wiki hii mjini New York Marekani , Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesisitiza “jukumu kubwa la chombo hicho kipya katika kusaidia kuelekeza mwelekeo wa akili mnemba kwa manufaa ya ubinadamu.”
Amesema “Kwa kila mmoja wenu, mmetoka katika kanda na taaluma mbalimbali, mkiwa na utaalamu wa hali ya juu katika AI na nyanja zinazohusiana. Kwa pamoja, mnaakisi jambo ambalo dunia haijawahi kuliona hapo awali.”
Mkutano wa UN kuhusu Akili Mnemba kwa Maslahi Bora umeanza Geneva, Uswisi Julai 8 2025
Kuifanya AI iaminike
Akili mnemba sasa inatumika katika mifumo “yenye athari halisi kwa ustawi wa watu,” amesema Bilel Jamoussi, Naibu Mkurugenzi wa Ofisi ya Uratibu wa Viwango vya Mawasiliano ya ITU.
Hii inajumuisha maamuzi ya kuajiri na upatikanaji wa huduma. Amesisitiza umuhimu wa viwango na maendeleo ya ujuzi, akibainisha kuwa “viwango vya kiufundi husaidia kuifanya AI iaminike”, lakini jambo la kuamua ni namna jamii na serikali zinavyochagua kutumia teknolojia hizi.
Wafanyakazi wasioonekana
Kuna nguvu kazi “isiyoonekana inayoiendesha AI nyuma ya majibu ya chatbots, algorithimu za mitandao ya kijamii na mifumo mingine ya kiotomatiki ambayo watu wengi sasa wanaichukulia kuwa ya kawaida.”
Katika mtandao huo, Ben Richards wa UNI Global Union ameeleza kuwa “tunapozungumzia wafanyakazi katika mnyororo wa data, tunazungumzia makundi mawili makuu”:
- Wasimamizi wa maudhui wanaofanya majukwaa kuwa salama zaidi kwa kupitia maudhui hatarishi
- Wapachikaji na waainishaji wa data wanaounda uhalisia ili mashine ziweze kujifunza
Popote shirika lake linapozungumza na wafanyakazi hao, ameongeza, wanaelezea hali zinazofanana, “shinikizo kali, ufuatiliaji wa kudumu, mishahara midogo na madhara ya afya ya akili.”
Mikono Bandia au Prosthetics kutoka Bioniks Technologies, iliyoundwa kwa kutumia zana za AI.
Mshtuko wa kisaikolojia nyuma ya skrini
Makampuni makubwa ya teknolojia mara nyingi hutegemea wafanyakazi katika nchi za Kusini mwa Dunia kwa kazi ya usimamizi wa maudhui na uainishaji wa data.
Nchini India pekee, makumi ya maelfu ya watu wanajihusisha na kazi hiyo. Kwa wakazi wengi wa vijijini, hasa wanawake, matangazo ya kazi ya kufanya nyumbani yanayohitaji tu mtandao yanaonekana kuwa fursa adimu ya kipato na uhuru.
Hata hivyo, wanapoajiriwa, mara nyingi hawajui aina ya maudhui watakayotarajiwa kuyapitia. Wengi hulazimika kusaini mikataba ya kutofichua siri (NDA) inayowazuia kujadili kazi yao hata na wanafamilia.
Kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni ya vyombo vya habari, mwanamke mmoja kutoka kijijini nchini India alieleza kuwa hutazama mamia ya video kwa siku, zikiwemo za ukatili wa kingono, ajali za barabarani na watu wakifa.
Mwanamke mwingine kijana alisema alitakiwa kupitia maudhui yanayohusisha ukatili wa kingono dhidi ya watoto na kuainisha nyenzo za picha za ngono. Watetezi wa haki za binadamu wameibua wasiwasi kuhusu mazingira hayo ya kazi.
Muungano wa kimataifa kwa kazi salama
Bwana. Richards amebainisha kuwa shirika lake linajenga muungano wa kimataifa wa wasimamizi wa maudhui na kuhimiza kanuni za kazi salama zinazozingatia haki ya kujiunga na vyama vya wafanyakazi na kufanya majadiliano ya pamoja.
“Tunataka AI iongeze uwezo wa binadamu,” amesema, akisisitiza kuwa manufaa ya maendeleo ya kiteknolojia yanapaswa kugawanywa kwa haki.
Deepfakes ni picha, video, au sauti ambazo zimedhibitiwa au kuzalishwa kwa kutumia teknolojia za AI.
Kukimbizana na malengo yasiyowezekana
Wafanyakazi katika nchi mbalimbali pia wanakabiliwa na msongo unaoongezeka kutokana na usimamizi wa algorithimu, ambapo mifumo ya programu huamua kasi ya kazi, ugawaji wa majukumu na tathmini ya utendaji. Aina hii ya usimamizi inaweza kuongeza shinikizo na hata kuleta hatari za usalama.
Kulingana na ufuatiliaji wa vyama vya wafanyakazi, tayari kumekuwa na ajali za vifo zinazohusishwa na wasafirishaji “wakikimbizana na malengo ya utoaji yasiyowezekana yaliyowekwa na algorithimu.”
Utafiti wa mwaka 2025 uliochapishwa na Chuo Kikuu cha Cambridge umebaini kuwa karibu theluthi mbili ya madereva na wasafirishaji nchini Uingereza hufanya kazi katika hali ya wasiwasi kutokana na “maoni yasiyo ya haki na mabadiliko ya ghafla ya saa za kazi yanayoamuliwa na algorithimu. Zaidi ya nusu ya waliohojiwa walisema wanaweka afya na usalama wao hatarini kazini”.
Ingawa majukwaa hayatoi maelekezo ya moja kwa moja ya kuvunja kanuni za usalama, mfumo wa motisha ukiwemo adhabu, malipo ya ziada na upangaji wa oda kwa kipaumbele huunda mazingira ambayo wafanyakazi huhisi kulazimika kufanya maamuzi hatarishi ili kulinda kipato chao.
Kuelekeza AI kwa manufaa ya ubinadamu
Wasiwasi kama huo unaibuka katika nchi na sekta nyingine, mifumo ya kiotomatiki inaweza kupanga zamu, kuweka viwango vya mishahara au hata kufanya maamuzi ya kufukuza mtu kazi, mara nyingi ikiwa na uangalizi mdogo wa kibinadamu na njia finyu za kukata rufaa.
Wawakilishi wa vyama vya wafanyakazi wameonya kuwa kupeleka AI bila kinga madhubuti kunaweza kuimarisha matatizo ambayo tayari yapo, wakiongeza kuwa usimamizi wa algorithimu tayari unachangia kuongezeka kwa mzigo wa kazi, ufuatiliaji wa kidijitali, maamuzi yenye upendeleo na kupungua kwa uangalizi wa kibinadamu katika maamuzi ya ajira.
ILO na ITU zinaendeleza mipango ya kusaidia kuunda mbinu za kimataifa za kudhibiti athari za AI katika masoko ya ajira, ikiwemo jukwaa la AI for Good na Muungano wa Kimataifa wa Haki ya Kijamii.
Kwa mfumo wa Umoja wa Mataifa, changamoto kuu ni kuhakikisha kuwa akili mnemba inapanua uwezo wa binadamu badala ya kudhoofisha usalama na ustawi wa wafanyakazi. Hilo linahitaji kuhamisha msisitizo kutoka ubunifu wa kiteknolojia pekee hadi katika utawala unaozingatia haki za binadamu, usawa na maendeleo endelevu.