
Pamoja na hayo
Ingawa ongezeko hili la mahitaji linatoa fursa kubwa za ajira na maendeleo endelevu, Bi. DiCarlo ameonya kwamba uchimbaji wa madini hayo pia umehusishwa na ukiukwaji wa haki za binadamu, uharibifu wa mazingira na kuongezeka kwa mvutano wa kisiasa duniani. Amehimiza nchi zinazozalisha na zinazotumia madini hayo kuimarisha mifumo ya utawala na kanuni za usimamizi ili kuhakikisha rasilimali hizo zinachimbwa kwa uwajibikaji na kunufaisha jamii.
Hatari hizi zinaonekana zaidi katika maeneo yaliyoathiriwa na migogoro ambapo madini mengi muhimu yanapatikana. Zaidi ya asilimia 70 ya uzalishaji wa kobalti duniani unatoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wakati Myanmar ni mojawapo ya vyanzo vikubwa vya madini adimu ya ardhini, na Ukraine ina akiba kubwa ya titani na lithiamu. Katika baadhi ya maeneo, makundi yenye silaha hutumia uchimbaji haramu wa madini kufadhili vurugu na shughuli za kiuchumi zisizo halali.
Hatua za suluhisho
Bi. DiCarlo amebainisha vipaumbele vitatu vya kukabiliana na changamoto hii: kuhakikisha uchimbaji wa madini unaleta manufaa ya haki kwa wananchi wa maeneo husika, kuimarisha ushirikiano wa kimataifa ili kuboresha utawala na ufuatiliaji wa madini katika minyororo ya usambazaji, na kutumia diplomasia na upatanishi kuzuia migogoro inayohusiana na rasilimali za asili. Amesisitiza kwamba usimamizi wa haki na uwajibikaji wa madini muhimu unaweza kusaidia kuwaondoa mamia ya mamilioni ya watu katika umaskini huku ukichangia amani na maendeleo endelevu.