Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmail Baghaei amejibu taarifa ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ambaye bila kulaani uvamizi na mashambulizi ya kichokozi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, ameeleza wasiwasi wake juu ya vita hivyo kwa uchumi wa dunia.

Baghaei amemhutubu Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na kumwambia kuwa: Tuweke mambo bayana, hivi sio vita, bali ni kitendo cha uvamizi na uchokozi usio halali ulioanzishwa na madola mawili yanayomiliki silaha za nyuklia dhidi ya Iran.

Amebainisha kuwa, kwa mara ya pili ndani ya miezi tisa, Marekani na Israel zimeanzisha vita vya kichokozi dhidi ya Iran katikati ya mazungumzo hasasi ya kidiplomasia.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran ameendelea kumhutubu Guterres kwa kusema, “Una wasiwasi tu kuhusu taathira hasi (za vita hivi) kwa uchumi wa dunia, lakini vipi kuhusu raia wasio na hatia, wakiwemo malaika 175 waliouawa kinyama katika Jiji la Minab, na wengine wengi waliouawa na kuwachwa na ulemavu kote nchini Iran katika jinai za Marekani na Israel ndani ya siku saba zilizopita?”

Baghaei ameeleza bayana kuwa: Umoja wa Mataifa unabeba dhima ya kisheria na kimaadili ya vita haramu na vya kichokozi vya Marekani na Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Aidha mapema leo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran katika taarifa yake kwa taifa kupitia televisheni, amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislami ina haki na wajibu wa kuendelea kujihami na kulinda mamlaka yake ya kujitawala, hadi itakapohakikisha kuwa mashambulizi mengine dhidi yake hayakaririwi tena.

Amekariri kuwa, harakati za Iran zinazoshuhudiwa hivi sasa katika eneo la Asia Magharibi zinafanyika kwa msingi wa “kujihami” na kwamba Jamhuri ya Kiislamu haina uadui wowote na majirani zake na wala nia yoyote ya kuzishambulia nchi hizo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *