
Katika ujumbe uliotolewa mapema leo Alkhamisi, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) Brigedia Jenerali Esmail Qaani ametoa shukrani kwa taifa na serikali ya Iraq kwa maandalizi mazuri ya mazishi ya Kiongozi aliyeuawa shahidi wa Mapinduzui ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei na watu wa familia yake.
“Leo, taifa la Iraq limetengeneza hamasa itakayodumi milele; wanaume na wanawake, vijana kwa wazee – Shia, Suni, Wakurdi, Wakristo na Waislamu, pamoja na wasomi wa kidini, wanazuoni wa ngazi za juu, makundi ya kikabila yenye hadhi kubwa, na maafisa – wote wamekusanyika kumuaga mtu ambaye alisabilia maisha yake yenye baraka katika kutumikia Umma wa Kiislamu, ulimwengu unaokandamizwa na kudhulumiwa na kutetea maslahi na matukufu ya Kiislamu,” amesema Brigedia Jenerali Esmail Qaani.
Ameongeza kuwa, mazishi ya Kiongozi aliyeuawa shahidi “yametumika kama onyesho lenye nguvu la umoja wa Waislamu na dhihirisho la chuki dhidi ya ubeberu na Uzayuni wa kimataifa, pamoja na kutoa wito wa kulipiza kisasi cha damu ya shahidi aliyetukuka na mashahidi wote wa Umma wa Kiislamu.”
Vilevile, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi amewashukuru wananchi wa Iraq, serikali na mamlaka mbalimbali za kidini, kikabila na kiusalama kwa kuwezesha shughuli “adhimu” ya mazishi ya Kiongozi marehemuu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Katika ujumbe uliotolewa leo Alkhamisi, Araqchi amesema mahudhurio ya mamilioni ya watu na ukarimu mkubwa ulioonyeshwa na Wairaqi ni “dhihirisho lisilo na kifani la utu na udugu wa Kiislamu.”
Sayyid Abbas Araqchi amesema shughuli hiyo imeonyesha uhusiano mkubwa wa kidini, kihistoria na kitamaduni kati ya mataifa haya mawili jirani, akiongeza kuwa uhusiano huo umebaki imara kupitia kujitolea kwao kwa pamoja kwa Imam Hussein (AS), na kuonyesha tena ukweli wa kudumu kwamba “Kumpenda Hussein Kunatuunganisha.”
Araqchi amesema matukio ya Najaf na Karbala yamefungua “ukurasa mwingine ya dhahabu” katika uhusiano wa Iran na Iraq, uliojengwa juu ya maadili ya pamoja ya Kiislamu na urafiki wa kudumu kati ya mataifa haya wawili.
Ripoti za awali za vyombo vya habari vya Iraq zinasema zaidi ya watu milioni 7 wameshiriki katika mazishi ya Ayatullah Ali Khamenei katika miji mitakatifu ya Najaf na Karbala.
Ndege iliyokuwa imebeba miili ya Shahidi Ayatullah Khameni na wanafamilia wake imeondoka kwa kuchelewa huko Najaf asubuhi ya leo Alhamisi kufuatia mahudhurio makubwa ya kihistoria ya watu wa Iraq katika shughuli hiyo.
Kujitokeza kwa wingi kwa watu katika mazishi ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Seyyed Ali Khamenei, nchini Iraq kumepelekea kuchelewa shughuli ya mazishi katika mji mtakatifu wa Mashhad, kaskazini mwa Iran.