Maraajii Taqlidi wa madhehebu ya Shia, ndani na nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, pamoja na Maulamaa wakubwa wa Kisunni wa hapa nchini na katika mataifa mengine ya Ulimwengu wa Kiislamu wametoa fatua ya Jihadi dhidi ya Marekani na utawala wa kizayuni wa Israel kufuatia uchokozi wa kidhalimu walioanzisha dhidi ya ardhi ya Iran.

Kufuatia uvamizi wa kijeshi ulioanzishwa siku ya Jumamosi ya mwezi 10 Ramadhani na tawala za kigaidi za Marekani na Israel, uliopelekea kuuawa shahidi Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu Shahidi Imam Sayyid Ali Khamenei pamoja na mamia ya raia wakiwemo watoto wa kike 165 wa skuli ya msingi ya mji wa Minab kusini mwa Iran, Maulamaa wa Kiislamu wa ndani na nje ya Iran wametoa fatua wakitangaza kuwa, kupigana Jihadi dhidi ya utawala wa kizayuni na mabeberu waistikbari wanaouhami na kuunga mkono utawala huo ni faradhi kubwa na muhimu ya dini.

Nchini Iran, Maraajii Taqlidi wa madhehebu ya Shia akiwemo Ayatullah Makarem Shirazi, Ayatullah Nouri Hamedani, Ayatullah Javadi Amoli na Ayatullah Seifi Mazandarani wametoa hukumu ya Jihadi dhidi ya wavamizi wa ardhi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran waliomuua shahidi Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Shahidi Imam Khamenei.

Katika upande mwingine Mashekhe na Maulamaa 660 wa Kiislamu wa madhehebu ya Sunni katika mkoa wa Sistani na Balochistan nchini Iran wakisisitiza kwamba, Jihadi ya kukabiliana na utawala wa kijinai wa kizayuni na waungaji mkono wake ni faradhi kubwa.

Wakati huohuo, Sayyid Kamal Haidari, Marjaa wa Waislamu wa madhehebu ya Kishia, Sheikh Nimr Ahmad Zaamut, mkuu wa Baraza la Kiislamu la Palestina na Sheikh Ghazi Hunainah, mkuu wa Umoja wa Maulamaa wa Kiislamu wa Lebanon, nao pia wametangaza hukumu ya Jihadi dhidi ya majeshi vamizi ya Kimarekani na Kizayuni…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *