CSW70 yang’oa nanga ikisistiza haki, haki ya kisheria na hatua kwa wanawake na wasichana
Ufunguzi Mkutano wa 70 wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake duniani, CSW70 umefanyika katika ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na mgeni rasmi ni Katibu Mkuu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ambaye ameeleza furaha yake kuwa katika ukumbi uliojaa viongozi waliokataa kukubali ukosefu wa usawa kama jambo lisiloepukika
Katika hotuba yake Guterres amesema dunia bado inaongozwa zaidi na mfumo dume unaowapa wanaume nafasi kubwa ya mamlaka.
“Tunaishi katika ulimwengu unaotawaliwa na wanaume, na utamaduni unaotawaliwa na wanaume. Usawa wa kijinsia ni suala la mamlaka. Hakuna hatua hata moja mbele kwa haki za wanawake ambayo imewahi kutolewa. Bali imeshinda. Wameshinda vizazi vya wanawake na wasichana, watetezi na wanaharakati, viongozi wa jamii na watafuta haki. Umeshinda wewe wewe.”
Amesema hali hiyo imekuwa changamoto kubwa katika jitihada za kufikia usawa wa kijinsia katika taasisi nyingi duniani. Hata hivyo, ndani ya UN kumekuwa na maendeleo muhimu katika kuongeza uwakilishi wa wanawake katika nafasi za juu za uongozi.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu huyo, wakati alipoanza uongozi wake, alijiwekea lengo la kuhakikisha kunakuwa na uwiano sawa kati ya wanawake na wanaume katika ngazi za juu za uongozi wa Umoja wa Mataifa. Leo, amesema lengo hilo limefikiwa.
“Kwa mara ya kwanza katika historia ya Umoja wa Mataifa, wanawake sasa wanaunda nusu kamili ya nguvu kazi ya Umoja wa Mataifa katika vitengo vya kitaaluma na vya juu zaidi. Na kwa mara ya kwanza, tulifikia usawa katika uongozi mkuu. Tumefanya hivyo ikiwa ni miaka miwili kabla ya ratiba – lakini pia natambua imekuwa ni miaka 80 imechelewa.”
Katika hotuba yake, Katibu Mkuu wa António Guterres amesisitiza kuwa kufikia usawa wa kijinsia si suala la haki kwa wanawake pekee, bali ni hatua muhimu kwa maendeleo ya dunia nzima. Amesema jamii ambazo wanawake wanapata haki na fursa sawa huwa na maendeleo ya haraka zaidi, uchumi imara na taasisi zenye uwajibikaji zaidi, akisisitiza kuwa kuimarisha usawa wa kijinsia ni msingi muhimu wa kufikia maendeleo endelevu duniani.
Balozi Maritza Chan Valverde wa Costa Rica akizungumza katika Ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wakati wa ufunguzi wa Kikao cha 70 cha Kamisheni ya Hali ya Wanawake Duniani CSW70
Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema bado kuna kazi kubwa ya kufanya ili kuhakikisha wanawake wanapata haki na fursa sawa katika jamii duniani.
Ametaja maeneo matano muhimu ya kuharakisha haki na usawa kwa wanawake ambayo ni kuhakikisha haki sawa za kiuchumi kwa wanawake, kuimarisha uwakilishi wao katika maamuzi ya kisiasa, kupanua upatikanaji wa elimu na fursa za kazi, kuondoa ukatili dhidi ya wanawake na wasichana, pamoja na kulinda haki za wanawake katika dunia ya kidijitali.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Kikao hicho cha 70 cha Kamisheni ya Hali ya Wanawake Duniani CSW70 Maritza Chan Valverde amezungumzia maudhui ya mwaka huu ambayo ni “Haki, haki ya kisheria na Hatua kwa wanawake na wasichana wote nakusema kila mtu anajukumu la kufanya “Ondoa vikwazo na uhakikishe kwamba haki inakuwa ukweli halisi kwa kila mwanamke na msichana. Hakuna nchi yenye usawa kamili wa kisheria, na wanawake duniani kote bado wanashikilia 2/3 ya haki za kisheria ambazo wanaume wanazifurahia.”
