
Katika saa za alfajiri ya Jumatano, Julai 8, 2026, jeshi la Marekani, kwa kukiuka waziwazi vifungu vya 2 na 4 vya Hati ya Umoja wa Mataifa na kifungu cha kwanza cha makubaliano ya kusitisha vita, limefanya mashambulizi ya kichokozi katika vituo vya ufuatiliaji na usimamzi katika pwani ya kusini mwa Iran.
Mashambulizi haya yamefanyika sambamba na hatua nyingine ya uhasama ya Wizara ya Fedha ya Marekani ya kufutilia kibali cha kuruhusu mauzo ya mafuta ya Iran. Katika taarifa ya haraka, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imelaani vitendo hivi na kuvitaja kuwa ukiukaji wa wazi wa ahadi za Marekani. Imesema utawala wa Tump ndio utakaobeba dhima ya matokeo yoyote hasi ya hatua hizo. Mohammad Bagher Ghalibaf, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu na mkuu wa timu ya mazungumzo ya Iran, ameorodhesha katika mtandao wa kijamii wa X visa vingi vya ukiukaji wa wazi wa makubaliano ya kusitisha mapigano uliofanywa na Marekani, na kuandika: “Zama za mabavu na ulaghai zimekwisha. Mbinu hii haitaleta matunda yoyote. Hatutakubali kujisalimisha.”
Kinachotofautisha duru hii ya mapigano na mivutano iliyopita ni jaribio la wazi la Marekani la kuanzisha njia tofauti ya kupita meli katika Lango-Bahari la Hormuz na kudhoofisha udhibiti na usimamizi wa Iran katika njia asili ya maji. Meli za mafuta zilizoshambuliwa na Iran siku ya Jumanne zilikuwa zimepuuza taratibu za kiusalama zilizowekwa na Iran. Iran, ambayo imepewa jukumu la kudhamini usalama katika njia hii ya maji chini ya Mkataba wa Maelewano wa Islamabad, imetangaza kwamba “njia pekee salama ya kupita meli za biashara na za mafuta kwenye Lango-Bahari la Hormuz ni ile iliyoainishwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na kuonya kwamba njia yoyote mbadala “haikubaliki na ni hatari sana.”
Katika kukabiliana na mashambulizi ya kijeshi ya Marekani, vikosi vya wanamaji na anga vya IRGC, katika operesheni ya pamoja, vilishambulia maeneo 85 ya kijeshi ya Marekani, ikiwa ni pamoja na vituo vya Bandari ya Salman nchini Bahrain na Kituo cha Anga cha Ali Al Salem huko Kuwait, na kutungua ndege ya adui aina ya MQ-9. Huku ikilaani kitendo hicho cha uchokozi, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imezionya nchi zote jirani hususan zile za kusini mwa mwambao wa Ghuba ya Uajemi kwamba ushirikiano wowote na mchokozi katika kutenda jinai dhidi ya Iran utahesabiwa kuwa ni ushiriki katika jinai hizo.
Akizungumza pambizoni mwa mkutano wa kilele wa NATO mjini Ankara, Donald Trump alitoa matamshi yanayokinzana kwa kusema: “Tukifikia makubaliano na Iran, sidhani yatadumu” na wakati huo huo kutangaza kwamba usitishaji vita ulikuwa “umekwisha.” Alisema wapatanishi wanaweza “kuendelea na mazungumzo ikiwa wanataka kufanya hivyo.” Kauli zinazokinzana za Donald Trump zinadhihirisha wazi mkwamo wa kimkakati wa Washington. Wakati mmoja anazungumzia kumalizika usitishaji mapigano, na mwingine, kuhusu uwezekano wa kuendelea mazungumzo. Wakati huo huo anaitishia Iran na kudai kwamba hakuna makubaliano yoyote na Tehran yanayoweza kudumu. Mgongano huu wa wazi wa maneno unaakisi kushindwa kimkakati Marekani katika kufikia malengo yake kupitia mashinikizo ya kijeshi. Wakati huo huo, mikusanyiko mikubwa ya mazishi ya Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na Iraq imeongeza kuchanganyikiwa kwa Trump mbele ya ukakamavu na mapambano ya kihistoria ya taifa la Iran. Ni lazima pia tuzingatie kwamba, kutokana na kuwa na pwani ndefu zaidi kando kando ya Ghuba ya Uajemi, Lango-Bahari la Hormuz na Bahari ya Oman, Iran ina wajibu mkubwa zaidi wa asili wa kudhamini usalama katika njia hii muhimu ya maji kuliko nchi nyingine yoyote. Kwa Iran, usalama wa eneo hili unafungamana moja kwa moja na mamlaka yake ya kitaifa, umoja wa ardhi na usalama wake wa kimkakati.
Kinachojitokeza hivi sasa ni kuarifishwa upya suala zima la mfumo mpya wa usalama katika eneo. Ujumbe wa suala hili uko wazi kabisa: Ghuba ya Uajemi, Lango-Bahari la Hormuz, na Bahari ya Oman ni maeneo ambayo hayapasi kuruhusiwa kuwa kitovu cha vitisho dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Usalama wa eneo hili unapasa kuzidhaminia nchi zote zinazopakana na maji haya, usalama wao uliojengeka katika msingi wa kuheshimiana, kutoingilia masuala ya ndani ya upande wa pili pamoja na kuimarishwa ushirikiano wa kikanda. Vinginevyo, kuendelea kuwepo kwa majeshi ya kigeni katika eneo hakutaudhaminia upande wowote usalama wake. Hivyo, jambo ambalo Marekani inakataa kulikubali hadharani ni uhalisia wa kijiopolitiki wa eneo hili nyeti. Kutokana na eneo lake la kijiografia, uwezo wa kimkakati na wajibu wake wa kihistoria, Iran ni mhusika mwenye nafasi muhimu ya maamuzi kuhusu usalama wa Ghuba ya Uajemi na Lango-Bahari la Hormuz. Hakuna mfumo madhubuti wa usalama unaoweza kuundwa katika eneo bila ushiriki wa moja kwa moja na kuheshimiwa haki na maslahi halali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.