Ameongeza kuwa ongezeko hilo la mapigano lilianza baada ya Hezbollah kufanya mashambulizi dhidi ya Israel tarehe 2 Machi, na kusababisha mashambulizi ya kulipiza kisasi ndani ya Lebanon kutoka
Maafa yameongezeka
Bi. DiCarlo amesema mamia ya maroketi, makombora na ndege zisizo na rubani au deroni, zimerushwa katika mpaka tenganishi kati ya Israel na Lebanoni ujulikanao kama Blue Line, hali inayozidi kuihusisha Lebanon katika mgogoro mpana wa kikanda.
“Uamuzi wa Hezbullah kushambulia Israel umeivuta tena Lebanon katika vita ambayo haikuitafuta wala haiwezi kuimudu,” amewaambia wajumbe wa Baraza hilo.
Kwa mujibu wa serikali ya Lebanon, mashambulizi ya Israel kusini mwa Lebanon, eneo la Bekaa na vitongoji vya kusini mwa Beirut yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 570 na kuwajeruhi zaidi ya 1,400.
Vurugu hizo pia zimesababisha zaidi ya nusu milioni ya raia kuyahama makazi yao, hali inayofuta hatua ndogo ya utulivu iliyopatikana baada ya kusitishwa kwa mapigano mwaka 2024.
Wanajeshi wa amani wa UNIFIL wanafuatilia Mstari wa Bluu kusini mwa Lebanoni.
Hatari kwa utulivu wa jamii
DiCarlo ameonya kuwa mapigano mapya yanadhoofisha uthabiti ndani ya Lebanon na kuongeza mvutano kati ya jamii mbalimbali.
“Mapigano mapya katika msitari tenganishi au Blue Line yamefuta kwa kiasi kikubwa maendeleo yaliyopatikana katika miezi ya hivi karibuni na yanahatarisha utamaduni wa kuishi pamoja wa Lebanon,” amesema.
Mgogoro wa kibinadamu waongezeka
Wakati huo huo, mkuu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Tom Fletcher ameliambia Baraza hilo kuwa hali ya kibinadamu inaendelea kuzorota kwa kasi, huku zaidi ya watu 750,000 sasa wakiripotiwa kuwa wamekimbia makazi yao nchini humo.
“Huu ni wakati wa hatari kubwa kwa Lebanon na kwa ukanda mzima. Kuna ishara nyingi za onyo zinazoonekana,” amesema Fletcher akionya kuwa raia ndio wanaoathirika zaidi na mgogoro huu
Vituo vya malazi vimefurika
Fletcher ameongeza kuwa Idadi kubwa ya familia zilizokimbia makazi zinatafuta hifadhi katika vituo vya pamoja vilivyojaa pomoni.
Zaidi ya watu 120,000, wakiwemo maelfu ya watoto, wanaishi katika takriban vituo 580 ambapo huduma za msingi bado ni chache.
Umoja wa Mataifa unasema ukosefu wa usafi, hifadhi salama na vifaa muhimu unawaweka wanawake na wasichana katika hatari kubwa ya unyonyaji na ukatili, huku pia kuongezeka kwa hatari ya milipuko ya magonjwa.
Wahamiaji wanaopokea msaada
Mambo muhimu matatu ya kuzingatia
Fletcher amesisitiza kuwa tunahitaji ulinzi wa raia, kupunguza mzozo, kuacha mapigano mara moja, na mazungumzo na maafikiano halisi kuelekea suluhisho la amani, kwa mujibu wa Chta ya Umoja wa Mataifa.
Amesisitiza madai matatu muhimu
Mosi: raia wote katika eneo zima lazima walindwe na kuhakikisha wanapata msaada unaookoa maisha.
Pili: tunahitaji ufadhili wa kutosha kwa ajili ya hatua za kibinadamu yenye misingi thabiti na zilizopanuliwa. Lazima tusaidiwe kufika popote pale ambapo mahitaji yapo katika eneo hilo.
Tatu: tunahitaji kufufuliwa kwa diplomasia ya kimkakati, tulivu, yenye mantiki na yenye matumaini. Tunahitaji akili tulivu za kushinda changamoto hii.
Jumuiya ya kimataifa yanaongeza msaada
Licha ya hali hiyo mbaya, amesema Umoja wa Mataifa na washirika wa kibinadamu wanasema wanaongeza juhudi za kutoa msaada wa dharura, ikiwemo chakula, maji na huduma za afya kupitia kliniki za simu kwa familia zilizokimbia makazi yao.
Fletcher amewataka viongozi wa dunia kuchukua hatua za haraka kupunguza mapigano akisema, “Lebanon imechoka na vita vya wengine. Haiombi msaada, bali inahitaji pumzi ya kuendelea kuishi.”
Lacroix: Walindamani wanaendelea na wajibu wao Katikati ya mzozo
Mkuu wa Masuala ya Ulinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa Jean Pierre Lacroix ameliambia Baraza hilo la Usalama kuwa walinda amani wa Umoja wa Mataifa wa mpango wa UNIFIL katika eneo la Kusini mwa Lebanon bado wako kwenye ardhi hiyo licha ya kuongezeka kwa mapigano kando ya msitari tenganishi Blue Line.
Akihutubia Baraza la Usalama kwa njia ya video Lacroix amesema kuwa kubadilishana kwa risasi za moto kila siku kati ya Hezbullah na vikosi vya Israeli tangu mwanzoni mwa Machi kumeongeza hatari kwa kiasi kikubwa, huku maroketi, makombora, ndege zisizo na rubani na mashambulizi ya anga yakiendelea kurekodiwa.
Mkuu wa misaada wa Umoja wa Mataifa, Tom Fletcher, akizungumza kwenye mkutano wa Baraza la Usalama huko New York mtandaoni kutoka Geneva.
Usalama na ufuatiliaji unakabiliwa na changamoto
Mpango wa UNIFIL umerekodi mamia ya mashambulizi ya anga ya Israeli na mamia ya maroketi ya hizbullah katika siku za hivi karibuni, pamoja na kuingia kwa vikosi vya Israeli kaskazini mwa Blue Line, hali ambayo inaweka tofauti kati ya vikosi vya Lebanon na Israeli. Lacroix ameonya kuwa matukio haya ni ukiukaji wa azimio la Baraza la Usalama namba 1701 na yanaweza kuendeleza kutokuwa na utulivu katika nchi ya Lebanon na ukanda mzima.
Walinda amani wasaidia raia
Lacroix amesema kuwa licha ya hali mbaya ya usalama, UNIFIL inaendelea kusaidia jamii za ndani na operesheni za kibinadamu kusini mwa Lebanon.
Walinda amani wametoa msaada wa kuhamisha raia, wakiwemo watoto, wazee na watu wenye ulemavu, kutoka katika vijiji kadhaa vilivyoathirika. Hata hivyo amesema , usalama wa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa umekuwa katika hatari, mfanyakazi mmoja kutoka kundi la Ghana alijeruhiwa vibaya mwanzoni mwa mwezi huu baada ya shambulio lililosababisha mlipuko kwenye kambi ya Umoja wa Mataifa.
Amemalizia kwa kusema kwa kuwa mapigano yanaendelea, baadhi ya walinda amani wamebakiwa kwenye vituo vyao, na kuzuia uwezo wao wa kufanya doria na kufuatilia hali, huku UNIFIL ikiendelea na juhudi za kupunguza mvutano na kuwezesha upatikanaji wa msaada wa kibinadamu.