
Wajumbe wa Baraza wameangazia rasimu mbili za maazimio kuhusu hali hiyo, moja ikiongozwa na Bahrain na nyingine na Urusi.
Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linavyofanya kazi
Kwa kawaida azimio la Baraza la Usalama huanza na rasimu ya maandishi iliyoandaliwa na mwanachama wa Baraza mmoja au zaidi (wanaojulikana kama penholder au kwa lugha ya Kiswahili unaweza kusema mshikakalamu). Rasimu hii huainisha kile ambacho Baraza linapendekeza kufanya. Kwa mfano kutoa wito wa kusitisha mapigano, kuweka vikwazo au kuhimiza upatikanaji wa misaada ya kibinadamu.
Kabla ya kura yoyote kufanyika, rasimu hupitia mashauriano na mazungumzo. Katika hatua hii, wanachama wa Baraza hujadili maneno ya pendekezo mstari kwa mstari, wakipendekeza marekebisho, lugha mbadala au kutafuta muafaka.
Mazungumzo yanapokamilika na wadhamini wa rasimu wanaamini kuna uungwaji mkono wa kutosha, rasimu huchapishwa na kusambazwa “kwa rangi ya buluu” (ikimaanisha kuwa maandishi yamekamilika na yako tayari kupigiwa kura.
Baraza lina wanachama 15. Ili azimio lipitishwe, lazima lipate angalau kura tisa za kuunga mkono na lisipingwe kwa kura ya turufu (veto) kutoka kwa wanachama watano wa kudumu: China, Ufaransa, Urusi, Uingereza na Marekani.
Likipitishwa, azimio hilo huwa msimamo rasmi au tamko la Baraza la Usalama, chombo cha Umoja wa Mataifa chenye jukumu la kudumisha amani na usalama wa kimataifa.
Pendekezo la Bahrain laungwa mkono
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio lililoongozwa na Bahrain kuhusu mgogoro unaozidi kuongezeka katika Mashariki ya Kati.
Azimio hilo limepitishwa kwa kura 13 za kuunga mkono na nchi mbili kujizuia kupiga kura (China na Urusi). Azimio hilo “linalaani vikali mashambulizi makali” yaliyofanywa na Iran dhidi ya Bahrain, Kuwait, Oman, Qatar, Saudi Arabia, Falme za Kiarabu (UAE) na Jordan, na kuongeza kuwa “vitendo hivyo ni ukiukaji wa sheria za kimataifa na ni tishio kubwa kwa amani na usalama wa kimataifa.”
Azimio hilo pia linaitaka Iran kusitisha mara moja mashambulizi yote dhidi ya nchi hizo.
Rasimu hiyo iliwasilishwa na Bahrain kwa niaba ya wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba (GCC) – Bahrain, Kuwait, Oman, Qatar, Saudi Arabia na Falme za Kiarabu (UAE), pamoja na Jordan.
Rasimu hiyo pia iliungwa mkono kwa udhamini (co-sponsored) na zaidi ya nchi wanachama 130 wa Umoja wa Mataifa.
Pendekezo la Urusi lakwama
Rasimu ya azimio la Baraza la Usalama iliyopendekezwa na Urusi imeshindwa kupata kura za kutosha.
Rasimu hiyo kuhusu mgogoro wa Mashariki ya Kati imeshindwa kupitishwa baada ya kutopata idadi inayohitajika ya kura katika Baraza la Usalama.
Ili azimio lipitishwe, lazima lipate angalau kura tisa za kuunga mkono kutoka kwa wanachama 15 wa Baraza.
Rasimu hiyo imepata kura nne za kuunga mkono na kura mbili za kupinga, huku wanachama tisa wakijizuia kupiga kura.