Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani, WHO kutoka Cairo Misri limeonya kuwa mifumo ya afya katika eneo la Mashirika ya Kati inakabiliwa na shinikizo linaloongezeka kadri idadi ya majeruhi inavyoongezeka na watu wengi zaidi kulazimika kuyahama makazi yao.

Idadi ya vifo Iran, Israeli na Lebanon

Mamlaka zinaripoti vifo vya zaidi ya watu 1,300 na majeruhi 9,000 nchini Iran, huku Lebanon ikirekodi takribani vifo 570 na zaidi ya majeruhi 1,400. Nchini Israel, watu 15 wameuawa na zaidi ya 2,100 wamejeruhiwa.

Hatari za kimazingira pia zinaibua wasiwasi.

Nchini Iran, moto wa mafuta ya petroli na moshi kutoka miundombinu iliyoharibiwa unaweka jamii zilizo karibu katika hatari ya kuathiriwa vibaya na vichafuzi vyenye sumu, ambavyo vinaweza kusababisha matatizo ya kupumua, muwasho wa macho na ngozi, pamoja na uchafuzi wa vyanzo vya maji na chakula.

WHO imethibitisha mashambulizi dhidi ya vituo vya huduma za afya nchini Iran, na Lebanon yaliyosababisha vifo na majeruhi miongoni mwa wahudumu wa afya na kuendelea kuvuruga huduma ambazo tayari zilikuwa chini ya shinikizo.

 Wakati huohuo, makazi ya muda yaliyojaa watu waliokimbia makazi yao pamoja na miundombinu iliyoharibiwa vinaongeza hatari ya milipuko ya magonjwa na vitisho vingine vya afya ya umma, hasa kwa jamii zilizo katika mazingira hatarishi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *