Taarifa iliyotolewa na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kulinda Amani nchini DRC, MONUSCO inasema takwimu zilizokusanywa na UNJHRO, mwaka 2025 zinaonesha kuwa jumla ya matukio 887 ya ukatili wa kingono unaohusiana na migogoro yalirekodiwa, yakihusisha waathirika 1,534. Kati yao, wanawake walikuwa 854 na wasichana 672.

Ubakaji unatekelezeka kimfumo

Ripoti hiyo inaeleza kuwa ubakaji unatumiwa kwa njia ya kimfumo kama silaha ya vita, hali ambayo pia inachangia kuibuka kwa kizazi cha watoto wanaozaliwa kutokana na ubakaji, ambao mara nyingi hukumbwa na unyanyapaa na kutengwa katika jamii.

Eneo la mashariki mwa DRC linaendelea kuwa kitovu cha ukatili huo, hasa katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, ambayo kwa pamoja yanachangia karibu asilimia 80 ya waathirika wote waliorekodiwa.

Waathiriwa pia wakumbwa na mateso kutoka kwa waasi na serikali

Kwa mujibu wa UNJHRO, asilimia 75 ya waathirika waliteswa na makundi yenye silaha. Kundi la  kundi la (M23) linatajwa kuhusika na idadi kubwa zaidi ya waathirika 439, likifuatiwa na makundi ya Wazalendo, CODECO, makundi mbalimbali ya Mai-Mai, pamoja na FDLR na ADF.

UNJHRO pia imeeleza wasiwasi kuhusu kuhusika kwa baadhi ya maafisa wa serikali katika ukiukwaji huo. Wanachama wa Armed Forces of the Democratic Republic of the Congo FARDC, Polisi ya Taifa ya Congo (PNC) na Wakala wa Taifa wa Ujasusi (ANR) wanatajwa kuhusika katika takribani asilimia 19 ya matukio yaliyorekodiwa.

Utumwa wa kingono na unyanyapaa kwa watoto

Ripoti hiyo pia inaangazia ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu kama vile utumwani wa kingono, ambapo wanawake na wasichana hushikiliwa mateka kwa muda mrefu, kubakwa mara kwa mara na wakati mwingine kulazimishwa kupata mimba.

Aidha, UNJHRO imeeleza kuwa watoto wanaozaliwa kutokana na ubakaji mara nyingi hukumbana na kukataliwa na familia, hukosa usajili rasmi wa kiraia, na kukabiliwa na hatari kubwa ya kutengwa kijamii au hata kuingizwa katika makundi yenye silaha.

Msaada wa kisheria ni changamoto

Wakati huo huo, licha ya asilimia 70 ya waathirika kupata huduma za dharura za matibabu, ni chini ya asilimia 2 pekee hupata msaada kamili unaojumuisha huduma za kisheria, kisaikolojia na kijamii.

Kwa mujibu wa UNJHRO, pengo hilo linaacha maelfu ya manusura bila msaada wanaohitaji ili kukabiliana na madhara ya muda mrefu ya kimwili na kisaikolojia ya ukatili walioupitia.

Wito wa kuchukua hatua

Kutokana na uzito wa hali hiyo, UNJHRO imetoa wito wa kuchukuliwa kwa hatua za haraka katika ngazi mbalimbali.

  • Mamlaka za kitaifa zimetakiwa kuharakisha hatua za kisheria dhidi ya wahusika wa uhalifu.
  • Kuhakikisha usajili wa kiraia kwa watoto wanaozaliwa kutokana na ubakaji ili kuvunja mzunguko wa kutengwa.
  • Makundi yenye silaha yametakiwa kusitisha mara moja mapigano, kuwaachilia bila masharti wanawake na wasichana walioko utumwani, na kukomesha utumwa wa kingono.
  • Jjumuiya ya kimataifa imetakiwa kuongeza msaada wa kifedha na kibinadamu ili kuhakikisha manusura wanapata msaada kamili na endelevu unaozidi huduma za dharura za matibabu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *