
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR, kupitia taarifa yake iliyotolewa leo jijini Geneva, Uswisi, limebainisha kuwa kaya kati ya 600,000 na milioni 1 zimepoteza makazi yao, huku wengi wakikimbia miji mikubwa kama Tehran kuelekea maeneo ya vijijini na mikoa ya kaskazini kutafuta usalama.
“Hali hii imeleta hofu kubwa ya kuongezeka kwa mahitaji ya kibinadamu kadiri uhasama unavyozidi kusambaa katika maeneo mbalimbali,” imesema taarifa hiyo.
Madhara kwa wakimbizi na msaada wa UNHCR
Mkurugenzi wa Programu za Dharura na Msaada wa UNHCR, Ayaki Ito, kupitia taarifa hiyo amesema mzozo huo pia umezikumba familia za wakimbizi zinazohifadhiwa nchini humo, hususan raia wa Afghanistan, ambao wapo katika hali ya hatari zaidi kutokana na mazingira yao duni na ukosefu wa usaidizi, hivyo familia hizo zinaondoka katika maeneo yaliyoathiriwa vibaya kufuatia kuongezeka kwa ukosefu wa usalama na ugumu wa kupata huduma muhimu.
Licha ya changamoto hizo, UNHCR imesisitiza kuwa inaendelea kurekebisha huduma zake ili kuwafikia watu wote wenye uhitaji kupitia vituo vyake vya mapokezi na huduma za simu za usaidizi. Bwana Ito amebainisha kuwa wanafanya kazi bega kwa bega na mamlaka za kitaifa nchini Iran ili kuimarisha maandalizi ya kupokea wimbi kubwa zaidi la watu wanaohama.
Wito kwa pande zote za mapigano
UNHCR inasisitiza pande zote zinazopigana kuhakikisha kuwa raia wanalindwa na msaada wa kibinadamu unaweza kuwafikia wahitaji bila kuwepo kwa vikwazo vyovyote, na kuhakikisha mipaka inabaki wazi kwa wale wanaotafuta usalama, kwani hatua hizi ni muhimu na zinapaswa kuzingatiwa kulingana na majukumu ya kimataifa ili kulinda maisha ya watu wanaokimbia mapigano.