Ili kukabiliana na changamoto hiyo, WFP inaunga mkono serikali mbalimbali kuhakikisha watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanapata milo shuleni ili wawe na afya njema na wawe tayari kujifunza.
Programu za milo ya shule zimeonekana kuwa uwekezaji wenye faida kubwa kwa maendeleo ya binadamu, ambapo dola moja ya Marekani inayowekezwa inaweza kuleta faida hadi dola 35 katika jamii na uchumi.
Njaa na Elimu: Changamoto kwa watoto wengi
WFP inasema katika nchi zilizoathiriwa na migogoro, watoto wana uwezekano mara mbili zaidi wa kukosa shule kuliko wenzao wanaoishi katika nchi zilizo na utulivu.
Kwa watoto wengi, hasa wasichana, mlo shuleni ni msaada muhimu unaowafanya waendelee kubaki darasani badala ya kulazimika kuingia katika ndoa za utotoni au ajira za watoto.
Kwa sasa, watoto milioni 466 duniani kote wananufaika na programu za mlo shuleni zinazoungwa mkono na serikali na mashirika ya kimataifa.
Mwaka 2024 pekee, WFP iliwasaidia watoto milioni 20 katika nchi 61 kupitia mgao wa chakula cha kubeba nyumbani na misaada ya fedha kwa familia.
Msumbiji. Chakula cha mlo Shuleni kinachopandwa kwa bustani Nyumbani huko Tete.
Faida za milo shuleni
1. Kuboresha elimu
Mlo shuleni huongeza mahudhurio, umakini na uwezo wa watoto kujifunza. Hii huwasaidia kufikia uwezo wao kamili na hatimaye kuchangia maendeleo ya jamii zao.
2. Kuboresha afya na lishe
Programu hizi huwapatia watoto virutubisho muhimu na kuwafundisha tabia bora za ulaji. Pia husaidia kupunguza utapiamlo, upungufu wa virutubisho muhimu na hata matatizo ya uzito kupita kiasi au utipwatipwa.
3. Kuwawezesha wasichana
Upatikanaji wa chakula shuleni huwahamasisha wazazi kuwapeleka na kuwaacha wasichana shuleni, hasa wanapofikia umri wa balehe. Hali hii husaidia kupunguza ndoa na mimba za utotoni pamoja na hatari za umaskini wa maisha yote.
4. Kukuza uchumi wa ndani
Kupitia mfumo wa “chakula kinachotoka kwa wakulima wa ndani kwa ajili ya mlo shuleni”, wakulima wadogo hunufaika kwa kupata masoko ya mazao yao.
Hii huongeza biashara, kipato na ajira huku ikichochea kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi na lishe bora.
Uwekezaji katika “Mtaji wa Kibinadamu”
Mlo shuleni pamoja na huduma za afya zinazohusiana nao huchangia kujenga kile kinachoitwa mtaji wa kibinadamu yaani afya, ujuzi, maarifa na uwezo wa watu katika jamii. Takribani asilimia 99 ya gharama za programu hizi hulipiwa na serikali za kitaifa, huku WFP ikitoa msaada wa kiufundi.
Kwa miaka mingi, WFP imefanya kazi na zaidi ya nchi 100 kuanzisha programu endelevu za mlo shuleni zinazoendeshwa na serikali.
Zaidi ya nchi 50 tayari zimechukua jukumu kamili la kuendesha programu hizo, jambo linaloonesha mafanikio ya muda mrefu.
Mwanafunzi mdogo nchini Kambodia anafurahia wali wake ulioimarishwa ambao ni sehemu ya milo ya shule inayoungwa mkono na WFP.
Dira ya baadaye
Dira ya WFP ni kuona kila mtoto duniani anapata mlo wenye lishe shuleni ifikapo mwaka 2030. Ili kufikia lengo hilo, kipaumbele kinatolewa katika:
- Kuimarisha uwezo wa serikali kumiliki na kuendesha programu hizi.
- Kuunganisha mikakati inayozingatia usawa wa kijinsia na mabadiliko ya tabianchi.
- Kupanua ushirikiano wa kimataifa kupitia Muungano wa Mlo Shulen (SMC) unaoungwa mkono na zaidi ya serikali 100 na washirika zaidi ya 140.
WFP inaendelea kusisitiza umuhimu wa kuongeza uwekezaji katika mlo shuleni kama nguzo muhimu ya ulinzi wa kijamii, elimu na mageuzi ya mifumo ya chakula duniani.
Unaweza kufanya nini kusaidia?
WFP inasema watu binafsi wanaweza kusaidia kwa kujifunza zaidi kuhusu programu za mlo shuleni na kuunga mkono juhudi za kuhakikisha kila mtoto anapata chakula shuleni.
Misaada na michango pia inaweza kusaidia kutoa chakula kwa mamilioni ya watoto wa shule duniani.