Akihojiwa na Assumpta Massoi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, Bi. Kabyemera amesema, “mwaka 2023 Tanzania ilitunga sera mpya ya ardhi iliyokuwa ni maboresho ya sera ya awali na kuondoa hitaji la kuzingatia mila na desturi kwenye masuala ya haki za kumiliki ardhi.”
Amesema walichukua hatua hiyo kwa kuwa sera hiyo imeweka msisitizo wa kutumia sheria kwa sababu sheria haina ubaguzi kwani mwanamke ana haki sawa ya kumiliki ardhi kama mwanaume.
“Licha ya kuwa na sera nzuri, kama haieleweki kwa wananchi ni kazi bure. Sasa hivi tumeanza mkakati maalum wa kufanya elimu kwa umma, kuwaelimisha wanawake waweze kutambua zile haki, lakini waweze pia kuzitumia kwa sababu huwezi kutumia kitu ambacho ukielewe vizuri,” amesema Bi. Kabyemera.
Uhamasishaji kwa umma
Naibu Katibu Mkuu huyo ambaye alikuwa anazungumza baada ya kuongoza kikao cha kando kilichoandaliwa na Tanzania kujadili haki ya ardhi kwa wanawake na wasichana, alitaja kampeni iliyopatiwa jina Samia Ardhi Clinic, iliyofanyika katika mikoa yote 26 ya Tanzania wiki iliyopita wakati wa maadhimisho ya siku ya wanawake duniani.
“Wizara tuliendesha kliniki hiyo na tulipata fursa ya kutoa elimu kwa wanawake na hii iliendeshwa nchi nzima kwenye ofisi zetu za ardhi. Tuliwafuata wananchi kwenye maeneo yao na kuanza kutoa elimu pamoja na kutoa huduma nyingine za sekta, lakini kubwa msisitizo ulikuwa ni kwenye elimu,” amesema na kuongeza kuwa, “kwa kuwa ilikuwa ni Samia Ardhi Clinic tulilenga wanawake, basi msisitizo mkubwa ulikuwa ni kwenye kufundisha kuhusu sera, lakini na sheria ambazo zinamlinda mwanamke kwenye kupata haki yake ya kumiliki ardhi,” amesema Bi. Kabyemera.
Mambo yaliyoulizwa zaidi na wanawake
Wanawake walikuwa na uelewa mdogo zaidi kuhusu haki ya kumiliki ardhi kwa kuzingatia hasa mil ana desturi.
“Sote tunafahamu kule vijijini wanawake wanatambua kuwa baba ndio kichwa cha familia kwa kuwa anajua kila mali ni haki ya baba kuisimamia. Lakini kumbe mwanamke kupitia sera na sheria ana uwezo na unaruhusiwa kabisa kumiliki mali yako mwenyewe, lakini vilevile unaweza kumiliki kwa pamoja pamoja na baba,” amesema Afisa huyo.
Hivyo basi wanawake walitamani wajue taratibu gani wazitumie kuweza kumiliki hii mali ambayo ni ya muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi na jamii.
Washiriki katika hafla ya kando ya Mkutano wa CSW70 inayojadili haki za ardhi za wanawake, makazi, na upatikanaji wa haki nchini Tanzania
Halikadhalika walitamani sana kujua taratibu za upatikanaji wa hatimiliki. “Unaweza ukawa na ardhi, lakini ardhi yako ili uimiliki lazima uwe na nyaraka au hati mkononi inayothibitisha kwamba hii ni mali yangu.”
Hivyo walipatiwa elimu mpya ya upatikanaji wa hizo nyaraka na vile vile na huduma. “Kama una ardhi yako unataka kupata hiyo hati na tayari ilikuwa imeshapita taratibu za upimaji na upimaji, basi pale pale hati zilikuwa zinatolewa ndani ya hiyo kliniki.”
Nafasi ya mashirika ya kiraia kama LANDESA
“Kwa kweli niseme kwanza nichukue nafasi hii kuwashukuru na kuwashukuru sana taasisi hizi ambazo sio za kiserikali kwa kuwa wamekuwa mstari wa mbele kushirikiana na Serikali kuhakikisha kwamba hizi huduma zinafika kwa wananchi,” amesema Bi. Kabyemera.
Amekiri kuwa serikali ipo lakini peke yake haiwezi kufanya kila kitu. “Hawa nao wamekuwa na mchango mkubwa. Wameeleza jinsi ambavyo wameweza kurahisisha kazi na kuzingatia sera na sheria. Wao wako kule mashinani kwa wananchi na wamerahisisha kwa kutengeneza mifumo ya kidigitali,” amesema Naibu Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Ametanabaisha kuwa hata serikali ya Tanzania nayo “tumerahisisha upatikanaji wa huduma zetu kidigitali. Sasa hivi unaweza ukapata hati yako ndani ya siku moja ukaenda na nyaraka zako zimekamilika. Ukafika pale ukaingiza kwenye mfumo wa eArdhi. Awali tulikuwa na mfumo unaitwa ILMIS ulikuwa unafanya kazi Dar es Salaam peke yake. Sasa eArdhi inafanya kazi kwenye mikoa mitano.”
Lucy Kabyemera, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi na Makazi nchini Tanzania aliyeongoza kikao hicho na kumpatia ufafanuzi wa mambo kadhaa ikiwemo mabadiliko ya sera.
Vipi changamoto?
Bado hatujaweza kumfikia kila mwanamke mpaka huko chini. Kwa hiyo bado tuna kazi kubwa ya kufanya uelimishaji. “Lakini hatuwezi kufanikiwa kumuelimisha mwanamke peke yake bila kumuelimisha mwanaume ili aone umuhimu wa kuunga mkono hatua hizo. Na tunawaelimisha kwa kuwapatia mifano hai ya pale changamoto zinapotokea.
Wanawake nao wabadili fikra
Lakini kingine pia ni kubadilisha mtazamo hata kwa wanawake. “Kuna wanawake bado wanaamini kwamba baba ndio kichwa. Kwa hivyo bila kutumia nguvu ya ziada kuwaonesha umuhimu itakuwa ni changamoto pamoja na kwamba mifano wanaiona, lakini ya kwamba inawezekana mwanamke akamiliki ardhi.”