Vita vinaendelea kote Mashariki ya Kati huku athari zake zikienea mbali zaidi ya eneo hilo.
Kwa mujibu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa bei ya mafuta imepanda hadi takribani dola 100 kwa pipa baada ya mashambulizi dhidi ya meli na miundombinu ya nishati kuvuruga njia muhimu za usambazaji.
Mashambulizi na mashambulizi ya kulipiza kisasi kati ya Israel, Hezbollah na Iran yanaendelea, huku meli kadhaa zikiripotiwa kushambuliwa katika Mlango wa Bahari wa Hormuz na Ghuba ya Oman, hali inayotikisa uchumi wa dunia.
Wakati huo huo, mashirika ya Umoja wa Mataifa yanaongeza juhudi za misaada ya kibinadamu kadri watu wanavyoendelea kuyahama makazi yao na mahitaji ya raia kuongezeka.
Tehran, mji mkuu wa Iran.
Kuongezeka kwa mapigano mpaka wa Israel na Lebanon
• Kumekuwa na ongezeko la kasi la mapigano katika eneo la msitari tenganishi mpaka wa Israel na Lebanon linalojulikana kama Blue Line: Walinda amani wa Umoja wa Mataifa wameripoti ongezeko kubwa la mashambulizi, huku zaidi ya makombora 120 yakirushwa kutoka Lebanon kuelekea Israel, yakifuatiwa na mashambulizi ya anga na mizinga kutoka Israel.
• Mgogoro wa Lebanon wazidi kuwa mbaya: Mapigano yanayoendelea kati ya Israel na Hezbollah yanasababisha watu wengi kuyahama makazi yao na kuongezeka kwa vifo vya raia nchini Lebanon, huku mamia ya maelfu wakilazimika kukimbia makazi yao na mahitaji ya kibinadamu kuongezeka.
• Watoto wanalipa gharama kubwa: Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanaonya kuwa mgogoro huo wa kikanda unazidi kuwa janga kwa watoto, huku zaidi ya watoto 1,100 wakiripotiwa kuuawa au kujeruhiwa na mamilioni kukumbwa na kusitishwa kwa masomo na kulazimika kuhama makazi yao limesema Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia watoto UNICEF.
• Mashambulizi ya meli na kupanda kwa bei ya mafuta: Meli kadhaa zimeripotiwa kushambuliwa karibu na Mlango Bahari wa Hormuz na Ghuba ya Oman, huku bei ya mafuta ikipanda hadi karibu dola 100 kwa pipa, jambo linalozua wasiwasi kuhusu masoko ya nishati duniani na minyororo ya usambazaji.
Mfanyakazi katika ghala la UNICEF huko Denmark anatayarisha misaada itakayopelekwa Lebanoni.
UNHCR: Umoja wa Mataifa unawasaidiaje watu nchini Lebanon?
Takribani watu 815,000 wameyakimbia makazi yao nchini Lebanon kutokana na ghasia zilizoanza baada ya majeshi ya Israel kujibu mashambulizi ya makombora ya Hezbollah katika siku za mwanzo za vita vya Mashariki ya Kati tarehe 2 Machi, kwa kufanya mashambulizi ya anga na kutoa amri za kuhamisha watu kwa wingi Limesema Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR.
Hadi sasa, Shirika hilo, limetoa magodoro, mablanketi, matandiko ya kulalia na mahitaji mengine muhimu kwa takribani watu 67,000 waliolazimika kuyahama makazi yao ndani ya nchi, wanaoishi katika makazi ya pamoja takribani 300 kote nchini.
Malfu ya watu wamefurushwa ndani ya Iran
Hadi watu milioni 3.2 huenda sasa wamefurushwa ndani ya Iran huku mgogoro ukiendelea kuongezeka, linaonya shirika hilo la UNHCR.
Makadirio ya awali yanaonesha kuwa kati ya kaya 600,000 hadi milioni moja zimekimbia makazi yao, wengi wakiondoka Tehran na miji mingine mikubwa kuelekea maeneo ya kaskazini na vijijini wakisaka usalama.
UNHCR inasema idadi hiyo inaweza kuendelea kuongezeka kadri mapigano yanavyoendelea, ishara ya kuongezeka kwa kasi kwa mahitaji ya kibinadamu nchini humo.
Hata hivyo, mahitaji ni “makubwa sana,” anasema mkuu wa UNHCR nchini Lebanon, Karolina Lindholm Billing.
Familia za Waafghanistan ambao hivi karibuni waliwasili kutoka Iran wanakusanyika kwenye bandari katika Mkoa wa Herat, Afghanistan.
Afghanistan yajitayarisha na kurejea kwa wakimbizi kutoka Iran
Wakati huo huo katika eneo pana la kanda ya Mashariki ya Kati, mashirika ya misaada nchini Afghanistan yanajiandaa kwa uwezekano wa kuongezeka kwa watu wanaorejea kutoka Iran, huku hadi Waafghan 800,000 wakitarajiwa kuvuka kurejea nyumbani iwapo mgogoro utaendelea, kulingana na makadirio ya kibinadamu.
Mashirika ya misaada yanaonya kuwa vita vinavyoendelea pamoja na vizuizi vya mipakani vinatatiza usafirishaji na utoaji wa misaada, na kulazimisha Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kutafuta njia mbadala za usambazaji wakati usumbufu nchini Iran na kwenye mpaka wa Pakistan ukipunguza kasi ya usafirishaji wa chakula na msaada wa lishe unaookoa maisha.
Mamia ya makombora yavurumushwa usiku kucha
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Lebanon (UNIFIL) umeeleza wasiwasi mkubwa kuhusu kuongezeka kwa mapigano katika eneo la msitari tengalishi baina ya Israel na Lenabon ujulikanao kama Blue Line.
Walinda amani wamebaini zaidi ya makombora 120 yakirushwa kutoka eneo la Lebanon kuelekea Israel, yakifuatiwa na mashambulizi saba ya anga kutoka Israel pamoja na zaidi ya mashambulizi 120 ya mizinga ya ardhini kama hatua ya kulipiza kisasi.
UNIFIL imesema mashambulizi hayo ni ukiukwaji mkubwa wa Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa namba 1701, na imeonya kuwa ghasia hizo zinaendelea kusababisha watu zaidi kuhama makazi yao pamoja na uharibifu wa jamii zilizo mpakani.
Ujumbe huo umeongeza kuwa walinda amani bado wapo eneo la tukio wakifuatilia maendeleo ya hali hiyo, wakishirikiana na pande husika na kusaidia kurahisisha upatikanaji wa misaada ya kibinadamu, huku ukitoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano.
Picha ya satelaiti ya Mlango-Bahari wa Hormuz.
UNCTAD: Usumbufu mlango wa Bahari wa Hormuz na athari zake
Wakati huohuo Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo na Biashara UNCTAD leo limeonya kuhusu usumbufu katika mlango wa Bahari wa Hormuz Iran na athari zake kwa biashara na maendeleo duniani kutokana na vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati.
Athari kuu na mambo ya kuzingatia
• Usumbufu katika Mlango wa Bahari wa Hormuz unaonesha udhaifu wa njia muhimu za usafiri wa baharini ambazo ni nyembamba zinapokabiliwa na mvutano wa kisiasa wa kimataifa, na jinsi hali hiyo inaweza kusababisha mishtuko katika minyororo ya usambazaji na masoko ya bidhaa duniani.
• Kupunguza hatari kwa biashara na maendeleo ya dunia, ikiwemo hatari za mazingira, UNCTAD inasema kunahitaji kupunguza mvutano na kulinda usafiri wa baharini, bandari, mabaharia na miundombinu mingine ya kiraia, huku njia salama za biashara zikiendelea kudumishwa kwa kuzingatia sheria za kimataifa na uhuru wa usafiri wa majini.
• Athari za kiuchumi, kwa kiwango cha kimataifa na kwa kanda husika, zitategemea muda wa mvutano huo, ukubwa wake na eneo lake la kijiografia. Ufuatiliaji endelevu ni muhimu ili kutathmini hatari zinazoendelea kujitokeza na athari zake zinazowezekana.
• Athari za kijamii na kiuchumi kwa nchi zinazoendelea, Nchi nyingi zinazoendelea tayari zinakabiliwa na mzigo mkubwa wa kulipa madeni, nafasi ndogo ya matumizi ya kifedha ya serikali na upatikanaji mdogo wa fedha. Katika hali hii, kupanda kwa gharama za nishati, usafiri na chakula kunaweza kuongeza shinikizo kwa fedha za serikali na bajeti za kaya, hali ambayo inaweza kuongeza changamoto za kiuchumi na kijamii na kufanya iwe vigumu zaidi kufikia maendeleo endelevu, hasa kwa nchi zinazotegemea sana uagizaji wa nishati, mbolea na vyakula vya msingi.
Makazi ya wakimbizi wa ndani yashambuliwa Beirut: IOM
Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji IOM limeshutumu shambulizi lililosababisha vifo katika makazi ya wakimbizi wa ndani nchini Lebanon.
Wahamiaji wanaopokea msaada
Mkuu wa shirika hilo, Amy Pope, amesema ana wasiwasi mkubwa kufuatia taarifa za shambulizi hilo lililolenga watu waliokimbia makazi yao mjini Beirut.
Watu wanane wameuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa.
Nchini Lebanon, takribani watu 125,000 waliolazimika kuyahama makazi yao kutokana na vita vya Mashariki ya Kati sasa wanaishi katika makazi ya pamoja yanayoendeshwa na serikali. Watu wengine wengi bado hawana mahali salama pa kwenda na wanaendelea kuwa katika hatari kubwa ya kudhurika.
“Mahema na makazi ya muda hayatoi ulinzi wowote dhidi ya hatari za mashambulizi ya mabomu,” amesema Bi. Pope.
Baraza la Usalama lamulika vikwazo vya Iran
Na kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa New York Marekani leo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linakutana kujadili suala la Iran.
Wajumbe wa Baraza wanajadili kamati ya azimio namba 1737, inayosimamia vikwazo vya Umoja wa Mataifa vinavyohusiana na mpango wa nyuklia wa Iran.
Kamati hiyo inafuatilia utekelezaji wa hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na vikwazo vya uhamishaji wa teknolojia zinazohusiana na nyuklia na kufungia mali za watu binafsi na taasisi zinazohusishwa na shughuli za Iran za urutubishaji wa uranium