RAIS Samia Suluhu Hassan amehimiza Watanzania washirikiane kulinda na kuhifadhi Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro kwa manufaa ya taifa na dunia. Kauli hiyo aliitoa jana Ikulu ya Chamwino, Dodoma, baada ya kupokea taarifa za Tume ya Kutathmini Mgogoro wa Ardhi katika eneo la hifadhi na utekelezaji wa zoezi la uhamaji wa hiari kwa wakazi wa eneo hilo.
Rais Samia alisema Ngorongoro ni maliasili adhimu, yenye bioanuai ya kipekee, vivutio vya utalii, historia ya mwanadamu wa mwanzo, na utamaduni wa jamii za asili. “Ngorongoro ni almasi yetu, mali ya Tanzania, na urithi wa dunia. Ni jukumu letu kulinda mfumo wa ikolojia unaounganisha hifadhi hii, Loliondo na Ziwa Natroni,” alisema. Aliongeza kuwa uhamaji wa hiari ulianzishwa ili kulinda mfumo huo na kuhakikisha manufaa ya utalii na urithi wa dunia unadumishwa.

Rais Samia alifafanua kuwa maeneo hayo pia ni muhimu kiasili kwa madini na rasilimali nyingine, na kuongeza kuwa Ngorongoro ina wanyama, ndege, misitu na volkano vyenye thamani kubwa ya kihistoria na kiikolojia. Pia, alisema wakazi wa eneo hilo ni rasilimali ya jamii, na ni lazima kushirikishwa katika utekelezaji wa mpango wa uhamaji na uhifadhi.
Alielekeza Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Moses Kusiluka, na Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, kuratibu utekelezaji wa mapendekezo ya tume hizo na kuhakikisha rasilimali zinazohitajika zinapatikana. Alisisitiza kuwa Serikali itashirikiana na wananchi na wadau katika hatua zote za utekelezaji wa mapendekezo hayo. SOMA: Migogoro 60 yapatiwa ufumbuzi Samia Ardhi Kliniki
