
“Kote duniani, tunasikia maneno mengi kuhusu amani, lakini tunaishuhudia kidogo sana amani hiyo,” amesema Guterres wakati wa sherehe nchini Uturuki alipokuwa akipokea Tuzo ya Kimataifa ya Amani ya Atatürk.
Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa “Sheria za kimataifa zinaendelea kusiginwa, siasa za nguvu zinaendelea kupanuka na usawa unaendelea kuporomoka. Teknolojia mpya, ikiwemo akili mnemba (AI), zinaweza kuharakisha vurugu badala ya kuzuia. Matumizi ya kijeshi yanaongezeka kwa kasi, huku misaada ya kuokoa maisha ikipungua kwa kasi.”
Gharama isiyokubalika
Katibu Mkuu ameonya kuwa raia wanabaki kulipa gharama, wakiwemo waliopoteza maisha na kuharibika kwa maisha na jamii, akitaja mgogoro unaoendelea Mashariki ya Kati kama mfano wa huzuni kubwa.
“Mashambulizi makubwa ya kijeshi yaliyoanzishwa na Marekani na Israel pamoja na mashambulizi ya kulipiza kisasi yanayofuatia kutoka Iran dhidi ya nchi nyingi ni tishio kubwa kwa amani na usalama wa kimataifa na yamesababisha mateso makubwa kwa raia,” amesema. “Kanda hii inaelekezwa ukingoni mwa kusambaratika.”
Matokeo yake ameongeza “yanaenea kote duniani kutokana na biashara kuvurugika, bei za nishati na chakula kuongezeka, na hali ya usalama na utulivu kudorora.”
Uhuru wa haraka unahitajika
“Kama kawaida, walio hatarini zaidi ndio wanaoumia kwanza na vibaya zaidi,” amesema.
“Kanda hii na dunia kwa jumla zinahitaji kwa dharura njia ya kutoka kwenye mgogoro huu.”
Kupunguza mvutano na mazungumzo ndiyo njia pekee ya kutoka katika hali hii, amesisitiza.
“Pamoja, tukumbatie amani’
Ziara hii ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Uturuki ni ziara ya mshikamano ya hivi karibuni kabisa kwa taifa hilo la Kiislamu kuashiria mwezi mtukufu wa Ramadan, ambayo imekuwa jadi ya kila mwaka ilijumuisha pia kupokea tuzo ya amani.
“Ziara hizi ni kielelezo chenye nguvu, kwangu na kwa dunia, cha rdhamira ya kweli ya Uislamu, huruma, jamii na huruma kwa wengine,” amesema.
“Ramadan hii, nilihisi kwa nguvu kwamba ziara yangu ya mshikamano lazima iwe hapa, nchini TUturuki. Nimekuja kuangazia dhamira ya kipekee na ukarimu wa wananchi wa Kituruki.”
Bwana Guterres amepokea tuzo hiyo kwa niaba ya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, akiheshimu jitihada zao za kutoa msaada wa kibinadamu na kujenga amani duniani, na pia kuomboleza vifo vya wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu, ikiwemo Gaza.
“Pamoja, tukumbatie fursa ya amani,” amesema.