Katibu Mkuu amesema hayo akizungumza na waandishi wa habari kwenye mji mkuu wa Lebanon, Beirut baada ya mazungumzo yake na Rais wa taifa hilo la Mashariki ya Kati Joseph Aoun.

Guterres ambaye amewasili Lebanon akitokea Uturuki alikokuweko kwa ziara ya kuonesha mshikamano na waumini wa dini ya kiislamu wakati wa mwezi huu mtukufu wa Ramadhani, ametoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano na kuimarishwa kwa mamlaka ya serikali.

Mtoto mchanga anawasha mikono yake juu ya moto mdogo uliojengwa kutoka kwenye vitalu vya saruji katika uwanja wa maegesho, na mahema na watu wengine waliohamishwa wanaonekana nyuma huko Beirut, Lebanon, Machi 9, 2026.

© WFP/Arete/Ali Yunes

Familia zilizofurushwa na vita hivi karibuni zinaishi katika mahema ya muda kando ya barabara nchini Lebanon.

Ingawa Marekani na Israeli zilishambulia Iran, Lebanon imejikuta imetumbukia kwenye mzozo huo baada ya wapiganaji wa Hezbollah kushambulia Israeli kwa madai ya kuchukizwa na uvamizi dhidi ya Iran.

Kwa mujibu wa serikali ya Lebanon, mashambulizi ya Israel kusini mwa Lebanon, eneo la Bekaa na vitongoji vya kusini mwa Beirut yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 570 na kuwajeruhi zaidi ya 1,400. 

Katibu Mkuu amesema, “nimekuja kama rafiki wa watu wa Lebanon, kuonesha mshikamano katika wakati huu mgumu sana kwa taifa hili. Ninajua kwamba watu wa Lebanon wanateseka sana.”

Amebainisha kuwa ziara hiyo inafanyika wakati wa vipindi viwili muhimu vya kidini: mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa waumini wa dini ya kiislamu na kipindi cha Kwaresima kwa waumini wa dini ya kikristo cha Kwaresima.

Katibu Mkuu amesema nyakati hizi zinapaswa kuwa za amani na mshikamano, lakini badala yake zinaendelea katikati ya mzozo na hali ya kutokuwa na utulivu.

halikadhalika amesikitishwa na suala kwamba Lebanon “imevutwa katika vita” ambavyo watu wake hawakuvitaka.

Guterres ametoa wito wa moja kwa moja kwa pande zote mbili kusitisha mapigano mara moja akisema, “wito wangu mkubwa kwa pande zote mbili ni kusitisha mapigano ili kumaliza vita na kufungua njia ya kupata suluhisho.”

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza na vyombo vya habari mjini Beirut, Lebanon.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza na vyombo vya habari mjini Beirut, Lebanon.

Amesema matumaini yake ni kwamba atakaporejea tena nchini humo, atakuta taifa ambalo uhuru wake na uadilifu wa mipaka yake vinaheshimiwa kikamilifu, na ambapo serikali pekee ndiyo yenye mamlaka ya kutumia nguvu.

Ametamatisha kwa kusema kuwa, “huu si wakati tena wa makundi yenye silaha. Huu ni wakati wa mataifa yenye serikali imara.”

Guterres azungumzia ukarimu wa raia wa Lebanon

Baada ya mazungumzo na Rais wa Lebanon, Katibu Mkuu amekutana pia na Spika wa Bunge Nabih Berri na kisha kuzungumza na waandishi wa habari.

Taarifailiyotolewa huko Beirut, Lebanon na msemaji wa Katibu Mkuu imemnukuu akirejelea kuwa vipindi hivi vya mfungo kwa waislamu na wakristu vinapaswa kuwa vya amani.

Na zaidi ya yote, amekumbuka ukarimu wa raia wa Lebanon, ukarimu ambao alishuhudia wakati yeye Guterres akiwa Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR.

Ninawapenda sana na kuwaheshimu watu wa Lebanon. Nilipokuwa Kamishna Mkuu wa Wakimbizi, nilishuhudia ukarimu wa watu wa Lebanon waliowapokea wasyria wengi sana na wapalestina wengi sana, na leo hii inaniumiza sana moyo kuona watu wa Lebanon wakiteseka kiasi hiki kikubwa,” amesema Guterres.

Amekumbuka hayo wakati huu ambapo kutokana na mapigano yanayoendelea kusini mwa Lebanon yamesababisha raia kuwa wakimbizi ndani ya taifa lao.

Watu 800,000 wamehama makazi yao, wengine 1,500 wamepoteza maisha, na hali ni ya kusikitisha na ya kutisha kabisa,” amesema Katibu Mkuu akisisitiza kuwa, “ujumbe wangu uko wazi sana: lazima tusitishe vita hii. Lazima kuwe na kusitishwa kwa mapigano mara moja.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *